Social Icons

Friday, 13 December 2013

MABILIONI YA USWIS KAA LA MOTO


WABUNGE wa Chadema, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na Godbless Lema (Arusha Mjini), jana waliwasha moto bungeni wakitaka Serikali iwasilishe bungeni ripoti ya fedha zilizofichwa nchini Uswiss na kwingineko duniani.

Wabunge hao walitaka ripoti hiyo jana walipokuwa wakichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala pamoja na taarifa ya Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake, Zitto alisema pamoja na kwamba Serikali imekuwa ikisema inashindwa kurejesha nchini fedha hizo kwa kuwa inabanwa na sheria za kimataifa, sababu hizo haziwezi kukubaliwa kuwa Serikali ndiyo haitaki kusaini mikataba hiyo inayowezesha kubadilishana taarifa.

“Hizi sababu kwamba tunabanwa na sheria za kimataifa siyo za kweli bali kikwazo kilichopo kinasababishwa na Serikali ambayo haitaki kusaini mikataba ya kimataifa.

“Hili tatizo la fedha kufichwa nje ni kubwa kwani Uswiss kwenyewe kuna kama shilingi bilioni 316 na katika Kisiwa cha Jersey kuna kama trilioni moja.

“Pia, Serikali ieleze ni kwa nini haijasaini mikataba hiyo ya kimataifa ya kubadilishana hizo taarifa,” alisema Zitto.

Wakati Zitto akisema hayo, Lema naye alisema kama Serikali haiwezi kuwataja kwa majina walioficha fedha hizo nje ya nchi, wampe yeye awataje.

Pamoja na hayo, alimtaka Zitto awasilishe majina hayo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwa yanajulikana.

“Suala hili la fedha za Uswiss lifanyiwe kazi kwani kitendo cha kukaa kimya kinazidi kuwaumiza wananchi.

“Majina ya wahusika yanajulikana na mheshimiwa Zitto ameshasema anayo, sasa ayakabidhi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kama naye hataki kuyapokea, basi tutajua anahusika na wizi huo.

“Kama Serikali inaogopa kuyataja hayo majina, mnipe mimi nitayataja, nipeni nitayataja kwa sababu sihitaji kinga kufanya hivyo,” alisema Lema.

Chanzo:- Rai

No comments:

 
 
Blogger Templates