Social Icons

Monday, 16 December 2013

VITA YA MAU MAU YANUKIA

MWAKA 1961 baada ya Tanganyika kupata uhuru, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitabiri hali yetu ya baadaye kuhusu ardhi akisema “Katika nchi yetu, ambamo Watanganyika ni masikini na wageni ni matajiri,kama wazalendo [wananchi] wataruhusiwa [au kulazimika chini ya sera kandamizi] kuuza [au kuweka rehani] ardhi yao, inawezekana kwamba, katika miaka 80 au 100 ijayo, ardhi yote ya Watanganyika itakuwa mikononi mwa matajiri wa kigeni; na wananchi watageuzwa kuwa vibarua wakazi [Maskwata, Manamba] katika ardhi ya mababu zao”.

Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, utabiri huu ungeanza kutimia kati ya mwaka 2041 na 2061, lakini kwa bahati mbaya unatimia haraka na mapema mno, kuanzia mwaka 1992, pale tulipofungua milango  kwa sera za soko huria na uwekezaji usiojali, ikiwa ni miaka 80 kabla ya  muda aliotabiri  Mwalimu.

Kwa Mwalimu, muda wa utabiri huo ulikuwa kama kipindi cha kusubiri siku ya kiama, na alijitahidi sana kufanya siku hiyo iepukike; siku ambayo watu watajiona kuporwa au kulazimika kuuza ardhi yao na kugeuzwa Maskwata; akaandika akisema: “Siku inakuja ambayo watu watachagua kifo kuliko fedheha; na Ole wao wale watakaoiona siku hiyo!.  Na Ole wao watakaoifanya siku hiyo isiepukike.  Natumaini na kusali kuwa siku hiyo haitofika”.

Kufanya siku hiyo iepukike, Mwalimu alianzisha sera za ubinadamu na zenye kujali utu:  alianzisha sera ya Ujamaa na Kujitegemea na Azimio la Arusha, ambalo lilipigwa teke mwaka 1992 kwa Azimio la Zanzibar wakati yeye alikwishaondoka madarakani.  Kuanzia hapo, siku ya kiama ikawa inanyemelea kuja kwa kasi ya kutisha!.

Tunashuhudia wageni wakipewa ardhi kubwa kubwa kwa jina la “uwekezaji” bila uwekezaji katika nchi ambayo idadi ya watu inaongezeka kwa kasi ya kutisha.  Hakika enzi za Mamwinyi wamiliki ardhi wasio wakazi (absentee Landlords) bila kutumia ardhi zinarejea hapa  kwetu, kwa ujinga wetu.

Migodi ya wageni inameza sehemu kubwa ya ardhi kwa uvunaji madini kwa pupa nasi kuachiwa mashimo kwa pato la mrahaba kiduchu. Uanzishaji maeneo ya hifadhi mpya za wanyama umeshika kasi kana kwamba wanyama ni muhimu na bora zaidi kuliko wananchi; huku mbuga asilia na wanyama pori waliomo “wakimilikishwa” wageni na kutamba watakavyo, ukiwamo uwindaji wa kuchakaza na utoroshaji wa wanyama nchi za nje.

Kutokana na kuzidi kupungua kwa ardhi kwa ajili ya matumizi ya wananchi kwa sababu ya uwekezaji tajwa hapo juu, wakulima na wafugaji sasa wanapigana na kumalizana wao kwa wao kugombea ardhi bila kujua kwamba kisababishi na adui wao mkubwa ni ubepari wa kimataifa uliolakiwa nchini na watawala wetu kwa shamra shamra kwa jina la “uwekezaji” usiojali na wa kiporaji.

Kufikia hapo, historia ni mwalimu mzuri kutufanya tuweze kutabiri kwa usahihi hatima yetu kwa yote haya: tunatabiri vita mithili ya vita ya Mau Mau iliyotokea nchini Kenya miaka ya 1950, na ishara za siku ya kiama ni dhahiri, kama tutakavyoona hivi punde.

Ishara ya kwanza, mbali na yanayotokea leo ambayo pia ni muhimu, ni hili kusudio la serikali la kurekebisha Sheria ya Ardhi ya Vijiji iweze kugeninishwa (alienate) kwa wawekezaji katika Kilimo, ikiwa ni pamoja na kuitoa kwa Benki ya Ardhi inayotarajiwa kuundwa chini ya mpango wa muda mfupi wa programu ya “Kilimo Kwanza”, maarufu kama “Mapinduzi ya Kijani”.

Mpango huo unaitika kwa masharti ya wakoloni wetu wapya – mashirika ya Bretton Woods, yakiwamo Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Shirika la Biashara la Dunia (WTO).  Chini ya sera za wakubwa hao, ni sharti kwa nchi mwenyeji kubinafsisha kwanza ardhi ya wakulima wadogo wadogo ili iweze kupata misaada ya Kilimo; na ili pia iweze kurekebishiwa (to reschedule) madeni yake kwa nchi wafadhili zinazounda “Paris Club”.

Chini ya utaratibu huu, ardhi ya umma huporwa au kuuzwa kwa bei ya kutupa; au kukodishwa kwa mashirika ya kuhodhi ya kimataifa (multinationals), na fedha kidogo inayopatikana hutumika kulipia madeni ya nje.  Na hiyo Benki ya Ardhi tunayoliwazwa kwamba itaanzishwa, ni sehemu ya Mtandao wa Benki ya Dunia ambayo si kwa ajili ya mwananchi wa kawaida.

Kinachotokea hivi sasa nchini mwetu kuhusu ardhi, kilianza hivi hivi nchini Kenya miaka ya 1940, na hatimaye kuzua vita ya wananchi dhidi ya wageni wavamizi wa ardhi maarufu kama vita ya Mau Mau.  Uporaji ardhi (land alienation) wa aina hii si mgeni barani Afrika na ni chanzo cha vita tangu enzi za uvamizi wa Afrika (scramble for Africa) na vita vya uhuru huko Afrika Kusini, Zimbabwe na kwingineko.

Maasi ya kwanza nchini Kenya yalikuwa mwaka 1940 baada ya wananchi zaidi ya milioni moja wa Kabila la Kikuyu, walioishi karibu na Nairobi walipoporwa ardhi na Wazungu, zaidi ya maili 100 za mraba na kupewa jina la “Kenya Whitelands”, yaani ardhi ya weupe Kenya.  Mtafaruku ukazuka kwa Wakikuyu kudai ardhi yao chini ya Chama chao – “Kikuyu Central Association” (KCA) ambacho Jomo Kenyatta alikuwa Katibu Mkuu wake wa kwanza, huku kauli mbiu “Rejesha Ardhi Iliyoporwa” (RAI) ikitawala.

Wakati huo huo, eneo la Rift Valley lilivamiwa kwa ajili ya makazi ya wazungu na wafugaji wa kimasai kutupwa nje. Kuanzishwa kwa kilimo cha mashamba makubwa eneo hilo kulifungua milango kwa Wakikuyu walioporwa ardhi zaidi ya “Whitelands” na kuanza kumiminika kwenda Rift Valley kuajiriwa kama vibarua – wakazi (Squatters) au maskwata na nguvu kazi rahisi.

Kufikia mwaka 1940, idadi ya maskwata iliongezeka kufikia 250,000, wakati idadi ya wazungu wahamiaji nayo iliongezeka kwa kasi kufikia 40,000 katika kipindi cha miaka mitatu tu, wakiwamo askari wa kizungu waliokimbilia Kenya baada ya vita ya pili ya dunia nao wakatengewa ekari 250,000 zaidi, kama ambavyo sisi hivi leo tunavyowapatia ardhi askari wa lililokuwa Jeshi la Makaburu kabla ya uhuru wa Afrika Kusini kwa jina la uwekezaji.

Hili halikuingia akilini mwa Wakikuyu; wakaanzisha mapambano dhidi ya uvamizi huu kwa kula viapo vya jadi vya siri.  Ndipo matukio ya uasi yalipoanza kuibuka kwa nguvu; mifugo ya wazungu ikahujumiwa na kulemazwa kwa wingi; na kwa mara ya kwanza mwaka 1948 Mkuu wa Wilaya ya Rift Valley aliripoti shughuli za “Mau Mau”, neno ambalo kwa Kikuyu halikuwa na maana yoyote ila kifupi cha maneno ya Kiswahili, “Mzungu Arudi Ulaya, Mwafrika Apate Uhuru” – MAU MAU.

Mwaka 1950, MAU MAU kilipigwa marufuku; lakini walichokuwa wakipambana nacho Wazungu si MAU MAU, bali msisimko wa wananchi kuwa huru na kurejeshewa ardhi yao.

Baada ya Kenyatta kurejea kutoka Uingereza na kuongoza Chama cha Kizalendo cha “Kenya African Union” (KAU) kilichoanzishwa mwaka 1944 kupigania haki za Mwafrika, hapo si Maskwata wa Rift Valley pekee waliokuwa kwenye vuguvugu la maasi tu, bali chuki ilikuwa imeenea miongoni mwa Wakikuyu wote wa vijijini kufuatia kuanzisha kilimo cha shuruti cha matuta pamoja na kukatazwa kulima mazao ya biashara.

Huko vijijini, viongozi wa jadi waliwasaliti watu wao, kama ambavyo baadhi ya Viongozi wetu wanavyotusaliti, kwa kuungana na wageni kupora ardhi na kujipambanua na tabaka la waporaji hao badala ya kujipambanua na wenye kuonewa.  Kwa kupokonywa ardhi, wanyonge hao wakafurika mjini Nairobi kutafuta maisha na kujikimu, wakiishi kwenye “magheto” kwa dhiki na uhalifu ukaongezeka.

Kuongeza tatizo juu ya tatizo, askari wa kiafrika waliokuwa wakirejea kutoka mstari wa mbele wa vita ya Pili ya Dunia wakiwa na matumaini ya maisha mapya, walipigwa na butwaa na kujenga hasira walipobaini kuwa ardhi waliyotumainia iliporwa na wageni. Kilichokuwa mbele yao ni adha ya Sheria ya vizuizi vya maeneo (Pass law), ukosefu wa ajira na makazi na mfumuko wa bei. Viapo vya siri vikashika kasi vijijini na mjini Nairobi; Kamati Kuu ya kusimamia na kuongoza hujuma, machafuko na ghasia dhidi ya Serikali ya Kikoloni ikaundwa kuashiria mwanzo wa mapambano.

Ishara hizi hazikumsitua Gavana, Sir Phillip Mitchel ambaye alijihusisha zaidi na maslahi ya Wazungu wenzake badala ya malalamiiko ya Waafrika, kama ambavyo tu viongozi wetu wasivyositushwa na ishara za kilio na mfurukuto wa wanyonge kwa kuwa viongozi wanajihusisha zaidi na tabaka la “walio nacho”, wawekezaji pamoja na harakati za kubakia madarakani kuanzia uchaguzi mmoja unapomalizika hadi unaofuata badala ya kusimamia mipango ya maendeleo ya wananchi wanaodai kuwaongoza.

Kadri ghasia zilivyoongezeka na kuzuka kwa mauaji, huku watu wengi zaidi wakilishwa viapo vya siri; ndipo Gavana mpya, Evelyn Baring, kwa kushauriwa na wasaidizi wake, alipotambua “yumkini si shwari tena”; akawatia ndani viongozi wote 150 wa KAU na kutangaza hali ya hatari, hatua iliyotafsiriwa na wafuasi wa MAU MAU na KAU kuwa ilikuwa ni  kutangaza vita dhidi ya wazalendo.

Katika hali ya kufadhaika, wakulima wa kizungu wa Rift Valley waliwafukuza maskwata zaidi ya 100,000, na maskwata hao wakaungana sawia na MAU MAU na kuelekea moja kwa moja misitu ya Aberdares na Mlima Kenya kuungana na wapiganaji wenye silaha kuendeleza mapambano. Siku chache baadaye, taarifa za kuuawa kwa masetla wa kwanza wa Kizungu zikasikika sambamba na kuuawa kwa Waafrika wasaliti wa umma 32 kwa kuyasaliti mapambano.

Hatimaye, Oktoba 1959, Serikali ya Uingereza, kwa kushindwa kudhibiti MAU MAU, ililazimika kuruhusu ardhi ya “Whitelands” kwa matumizi ya watu wa makabila na mataifa yote.  Kenya ilipopata uhuru mwaka 1963, serikali mpya, kwa msaada wa Uingereza, ilinunua sehemu kubwa ya ardhi ya “Whitelands” na kuihamishia kwa wazalendo ili kuwapunguzia tatizo la ardhi.

Vivyo hivyo, mashamba ya wazungu yaliweza kununuliwa na Wakenya hivi kwamba kufikia mwaka 1971, ekari zipatazo 1,500,000 za mraba zilikuwa zimenunuliwa kwa matumizi ya familia 500,000.

Hadi miaka ya karibuni, ni asilimia tatu tu ya ardhi iliyokuwa “Whitelands” ilikuwa bado mikononi mwa Wageni, huku zoezi la kuwarithisha wazalendo likiendelea.

Zimbabwe wamefanya vivyo hivyo, na Afrika Kusini pia ambako inatarajiwa kuwa, kufikia mwaka 2014, ardhi yote ya wazungu na migodi yote, itakuwa mikononi mwa wazalendo kama wawekezaji; tofauti na hapa kwetu ambapo wageni wameruhusiwa kuvuna wasichopanda, na wazalendo kubezwa kwamba hawana mitaji.

Haiingii akilini, kwamba wawekezaji, kwa mfano, katika nishati (IPTL/Richmond) wanakuja na “briefcase” tupu, kisha tunawapa mikataba wanayoitumia kukopa fedha kwenye Benki zetu wenyewe na kuwekeza, hatimaye tunawapigia magoti tukilia umasikini.  Huu ni uzandiki na usaliti mkubwa kwa umma.

Wahenga walisema, historia hujirudia; kwamba ipo siku umma wa kitanzania utakaporejea viapo vyake vya jadi (umoja) vya siri vilivyoleta uhuru, kuashiria vita vya ukombozi awamu ya pili, pale sera za soko huria na uwekezaji usiojali zitakapozalisha “Maskwata” kwa wingi; pale jeshi la vijana wanaomaliza elimu ya juu na sekondari litakapoanza kurejea kwa wananchi, lakini lisiwe na ardhi ya kuendeshea maisha; pale ambapo ardhi yote itakapokuwa mikononi mwa “Masetla” wa kigeni na makuwadi wao wa nchini kama tabaka, na Wazalendo kuwekewa vizuizi (Passlaw) waonekane manamba ndani ya ardhi ya mababu zao.

Pale ambapo jeshi la “mafukara” hawa litakapoungana na “Maskwata” wa sera za uwekezaji usiojali na kuelekea msitu wa “ukombozi mpya” kula kiapo cha siri kwa jina la “Uzalendo”.  Ole wao kina “Evelyn Baring” na mawakala wao wa ndani, Ole wao wasaliti wa umma; pale ghadhabu ya umma itakaponasa wahanga wa kwanza kuashiria mwanzo wa MAU MAU ya Mtanzania.

Hapo ndipo watakapojua kwamba ardhi yetu si ya “Walter Delamare” na wale wanaotutaka tule nyasi; bali ardhi yetu ni mali ya jamii pana ya Wazalendo, wakiwamo waliotutangulia mbele ya haki, walio  hai na ambao hawajazaliwa.

Chanzo:- Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates