“ Ndiyo.” “Kwa hiyo nikale na wewe kwako?” “Hapana leo tutakwenda hotelini.” “Hakuna tatizo.” “Basi kaendelee na kazi yako.” Subira alitoka huku moyo wake ukicheka alitamani kupiga vigelele, hakukaa alimpigia simu mzee Mukti ili kumjulisha kilichoendelea.
“Basi binti kazi imekwisha, jioni njoo tumalize kazi kabisa.” “Sawa mzee wangu.” Subira alijiandaa kutoka na bosi wake kwenda kupata chakula cha mchana, alifanya kazi iliyobakia haraka ili asibakishe kiporo. Baada ya muda Thabit alimpigia simu ajiandae watoke wakapate chakula cha mchana.
Alikwenda maliwatoni kujitengeneza akiwa pamoja na kuupodoa uso wake ili azidi kuonekana mpya kwa bosi. Thabit alitoka na kumpitia Subira aliyekuwa tayari amejiandaa, walitoka hadi kwenye gari, Kabla ya kuondoka Thabit alimuuliza Subira: “Twende wapi?” “Sijui, utakapotaka wewe.”
“Nimekupa upendeleo chagua unapopaona panafaa wewe.” “Mmh! Basi Steers.” “Hakuna tatizo.” Thabit aliwasha gari kuelekea Steers kwa ajili ya chakula cha mchana na sekretari wake.
Walipofika waliagiza chakula na kuanza kula, muda wote moyo wa Thabit ulikuwa ukimsukasuka kutokana na kumpenda sana Subira. Alijikuta akishindwa kuzuia hisia zake japokuwa alikuwa akikumbuka masharti aliyopewa na jini Nargis.
“Subira unajua wewe ni mzuri?” Thabit alisema huku akipeleka kijiko cha chakula mdomoni. “Nitajuaje wewe ndiye unayeuona,” Subira alijibu kwa tabasamu la mtego. “Unajua Subira lazima niseme ukwe…” Thabit alinyamaza baada ya kusikia sauti ya mkewe aliyosema muda mfupi kabla ya kuondoka kurudi ujinini.
Alitulia akiwa kama anaangalia tivii baada ya kuona marudio ya siku ambayo mkewe Nargis alipomuamsha ili amuage na kumkuta akilia. “Mbona macho yamevimba?” “Acha tu, Thabit sikupenda kuwa mbali na wewe kwa kipindi kirefu, kitendo walichonifanyia wazazi wangu kimeniumiza sana.
Kama walikubali uwe mume wangu kwa nini hawataki tukae wote kipindi cha kujifungua na kulea watoto wetu?” Nargis alianza kulia tena. “ Hatuna budi kukubaliana nao, hata mimi najua nitateseka sana, miaka kumi ni mingi sana Nargis, nitakuwa mpweke sana.
Pamoja na kukupenda lakini ulikuwa mtu muhimu sana katika maisha yangu, nilikuzoea sana nitacheka na nani nitacheza na nani?” Thabit alijikuta akizungumza sauti ya kilio kutokana na kutengana na mpenzi wake Nargis. “Hilo hata mimi linaniumiza, lakini naomba uniombee nijifungue salama.”
“Nitakuombea siku zote.” “Thabit naondoka nikiwa nimekuachia utajiri mkubwa ambao hutaumaliza mpaka unakufa, unajua kiasi gani nilivyopigana na majini wenzangu na wanadamu kukulinda. “Nina dhambi ya kuua majini na wanadamu kwa ajili yako.
Nimewatia wanadamu na majini vilema ambavyo watakufa navyo kwa ajili yako. “Thabit naondoka nakuacha peke yako, kwa utajiri ulionao una mtihani mzito kwa wanadamu kila mwanamke atakutaka, wapo watakaokuendea kwa waganga ili wakupate.
Kipindi changu cha kujifungua sitaweza kutoka mpaka miaka kumi hivyo sitakuwa karibu na wewe tena. “Mpenzi naomba usinisaliti nimechoka kubeba dhambi za wanadamu na majini kwa ajili yako.
N akuomba baada ya kuondoka kaa mbali na wanadamu, mafuta niliyokuachia siku ukinikumbuka sana jipake usiku wakati wa kulala utaniota usingizini lakini hatutaonana mpaka miaka kumi ipite,” Nargis alisema kwa hisia kali.
“Nakuahidi kuwa muaminifu kwako, sitakusaliti nakupenda sana Nargis, nilitamani niwapokee wanangu wakati wa kuzaliwa lakini sina jinsi. Nenda mpenzi wangu ukijua nakupenda kuliko kiumbe chochote kilichoumbwa na Mungu. Nakuahidi kukusubiri hata kwa miaka mia moja,” Thabit alimuahidi Nargis.
“Kweli Thabit?” Nargis alimuuliza Thabit huku akimkazia macho yake makubwa lakini yenye urembo wa aina yake. “Kweli kabisa.” “Hutanisaliti?” ulimuuliza tena. “Siwezi.” Thabit alijikuta amehama kimawazo kitu kilichomshtua Subira.
“Vipi bosi?” “Ee...ee...eeh,” Thabit alishtuka na kujikuta akifuta uso kwa mikono kama anaondoa kitu na kutuliza macho kwa Subira huku mapigo ya moyo yakienda mbio. Alitikisa kichwa kujiweka sawa huku uzuri wa Subira ukijaa tena machoni mwake.
“Bosi mbona hivyo una nini?” Subira alimuuliza akiwa amemkazia macho huku akirudisha kijiko chenye chakula kwenye sahani. “Mmh! Achana nayo tuendelee na yetu, vipi mbona huli?” Thabit alisema huku akichota chakula na kupeleka mdomoni.
“Nakula,” Subira alijibu huku akichota chakula. W aliendelea kula kimyakimya hakukuwa na mazungumzo yoyote mpaka walipomaliza na kuondoka. Walipofika ofisini Thabit alionekana amechoka hakukaa alimuaga Subira kuwa anatoka kidogo.
Baada ya kutoka Subira alijiuliza maswali mengi juu ya hali ya bosi wake kugeuka vile wakati alikuwa amechangamka na kumpa matumaini hasa pale alipoonesha kumuulizia kuhusu uhusiano wake.
Itaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment