“Ha! Dada ako amefikia huko?” uliuliza upande wa pili lakini sasa simu alikuwa nayo Beka…
“Haloo mkubwa…” alianza kusema Beka…
SASA JIRUSHE NAYO…
Ee, ni nini kimetokea mkubwa?” alihoji mume wa dada wa Aisha huko aliko…
“Hamna kitu bwana, unajua wametofautiana hawa, sasa mke wangu akahisi labda mimi natembea na mkeo, yaani shemeji yangu, inawezekana kweli we unavyoona?” aliuliza Beka.
“Hamna shemeji, nimewakuta kabisa kitandani, wako kama walivyozaliwa, asikudanganye huyo,” alisema kwa sauti ya juu Aisha iliyomfikia wa upande wa pili naye akajibu…
“Mimi sijui kitu bwana Beka, nyie ndiyo mpo huko. Kama ni kweli au si kweli mnajua wenyewe. Lakini sina cha kusema. Huyo mwanamke nilimwacha kwa mambo hayo ya kusaliti, yeye hata vijana wadogo kiumri kwake anataka kutembea nao, ndiyo tatizo lake kubwa,” alisema mume wa shemeji wa Beka kisha akakata simu.
Beka alionekana kushtuka sana simu kukatwa, akajikuta ameduwaa na simu ya Aisha mkononi, naye mwenyewe akaikwapua na kuminya namba nyingine.Beka aliduwaa zaidi, dada mtu yeye machozi hadi kwenye ncha ya kidevu. Kutoka moyoni alikiri kwamba amekuwa akimtendea mdogo wake ubaya uliopitiliza. Kuna sauti ilikuwa ikimwambia…
“Sasa wewe, wanaume wote hao umewaona hawafai hadi kuamua kutembea na shemejio, mume wa mdogo wako wa kuzaliwa tumbo moja, baba mmoja mama mmoja? Kumbe we hufai!”
Hii sauti ilimuuma sana dada mtu huyo, akatamani ardhi ipasuke ili yeye azame ndani yake na kuachana na aibu ya dunia hii.
Aisha aliweka simu sikioni baada ya kumaliza kubonyeza namba akatulia kidogo kusikiliza, kisha akasema…
“Eee shikamoo mama…mama dada nimemfumania na mume wangu, hivi kweli mama dada anaweza kunifanyia…” kabla hajamaliza kusema, Aisha aliangua kilio, dada yake akaiwahi simu na kuiweka sikioni yeye kisha akaongea na mama yake….
“
Kwa nini umempokea kwanza mtu asiyekuwa na heshima?” dada mtu alimkuta mama yake anamalizia kusema hayo…
“Mama, ni mimi…”
“Umefanya nini huko wewe?”
“Mama si kweli, ni mawazo yake tu huyu….”
“Mama kweli, nimewakuta kitandani hawana nguo,” alisema Aisha kwa sauti ya juu, mama yake akaisikia…
“Unasema anakusingizia, mbona anasema amekukuta kitandani kabisa?”
“Ah! Mama bwana, usimsikilize huyu…”
“Nijibu, amewakuta kitandani au hajawakuta kitandani?” aliuliza kwa hekima mama mtu…
“Mimi sikumbuki mama kama nilikuwa kitandani na mume wake.”
“Hukumbuki?”
“Ndiyo.”
“Unaugua kichaa siku hizi?”
“Kivipi?”
“Yaani ushindwe kukumbuka kitu kama hicho?” alisema mama mtu huyo na kukata simu kwa hasira. Alitetemeka, akajikuta anaishiwa nguvu, akakaa chini.
“Hivi kweli kabisa huyu mtoto anaweza kufanya hivi kwa mume wa mdogo wake? Si afadhali mdogo wake ndiyo angemfanyia yeye hivi, tungesema akili za kitoto?
“Halafu ni kweli kabisa wamefumaniwa, hata maelezo yake yanaonesha. Eti sikumbuki, anamdanganya nani?”
“Dada kifupi sitaki kukuona humu ndani kuanzia sasa hivi,” alisema mdogo mtu huyo huku akimtumbulia macho ya hasira. Alionekana kutaka kumvaa wakati wowote ule…
“Kwa hiyo niende wapi?” aliuliza.
“Sijui, kwani umetokea wapi? Unakuja hapa unasema umeachwa kumbe umejiacha mwenyewe, kama hii tabia umekuja nayo kutoka kwako si ndiyo maana mumeo alikupiga chini.”
Mara, simu ya mama yao iliingia kwenye simu ya dada mtu, akaipokea kwa uvivu na kujifikiria sana…
“Eee mama…”
“Sikia, panda gari njoo huku, baba yako anasema uje haraka sana,” mama akakata simu.
Mara simu ya Aisha ikaita, akaipokea haraka sana baada ya kubaini ni ya mama yake…
“Haloo mama…”
“Baba yako anasema uje huku haraka sana. Sasa utakuja lini mwanangu?”
“Mimi nitakuja kesho mama, nitatoka huku asubuhi sana.”
Mazungumzo yote hayo, Beka alikuwa akiyasikia, moyo ulimwenda kwa kasi akiwa haamini nini kimetokea. Moyoni alijuta sana, alijua anampoteza mkewe hivihivi anaona…
“Da! Shetani bwana, kweli ana nguvu. Lakini naamini Mungu ana nguvu zaidi kwani yeye kaweka sheria zake tu, ningezifuata haya yote yasingetokea,” alisema moyoni Beka. Mwishowe akasema…
“Ah! Mi naliacha liserereke lenyewe tu, nitafanyaje sasa?”
***
Usiku wa siku hiyo ulikuwa mrefu sana kwa wote watatu, pengine hata na wazazi wao kule kijijini.
Kila mmoja aliwaza la kwake na hatima yake. Aisha alipata wakati mgumu zaidi kwani aliwaza afanye nini ili yaliyotokea yawe kama hayakuwahi kutokea na aendelee kuishi na mumewe, Beka?
“Yaani kama ananisaliti kwa dada yangu, basi kwa marafiki zangu ni zaidi,” alisema moyoni Aisha akiwa amelala akiangalia juu, yaani alilala chali.
“Hivi, lakini mimi kosa langu nini? Kama mke mwenyewe namuomba unyumba hataki, ningefanyaje sasa?” aliwaza Beka naye akiwa amelala akiangalia juu.
Aisha alishindwa kuvumilia, akamwita mumewe…
“Beka…”
“Nini?”
Sasa Beka alianza kuwa mkorofi f’lani hivi kwa mkewe baada ya kuwaza yake…
“Yaani mi nakuita unasema nini?”
“Ulitaka niitikiaje?”
“Kwani siku zote unaitikiaje?”
“Hebu niambie unachotaka kusema…”
Itaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment