“Hii si bure lazima kuna mkono wa mtu,” alisema mmoja wa wafanyakazi.
“Wameona sisi ndiyo tunafanya vizuri hivyo lazima wametuendea mbali, moto gani usiounguza sehemu yoyote zaidi ya bidhaa za dukani, wanataka tukale wapi?” msichana mmoja alihoji huku akilia.
Endelea...
“Nendeni nyumbani ili nitafakari kisha kesho nitawajulisha kinachoendelea, kuna kontena kumi za bidhaa zinaingia kesho usiku ambazo zilikuwa za maduka mengine nitapunguza baadhi ya makontena na kuleta hapa ili muendelee na kazi,” Thabit aliwaambia wafanyakazi wake waliokuwa wamechanganyikiwa.
“Tutashukuru bosi,” walijibu kwa pamoja.
Subira muda wote alikuwa akilia kitu kilichomfanya Thabit ambembeleze.
“Mpenzi nyamaza tutarudisha kila kilichopotea.”
“Lazima tuhangaike yasije tokea tena,” Subira alitoa wazo mbadala.
“Tutafanya hivyo.”
“Basi tumtafute mtaalamu wa kulinda mali zetu.”
“Tutamtafuta wapi?”
“Mi namjua.”
“Basi tutakwenda.”
“Tena leo hiihii.”
“Hakuna tatizo, twende tukaangalie sehemu nyingine, maana mpaka sasa moyo wangu hauna amani. Moto wa leo umenipotezea zaidi ya milioni mia nane.”
Kusikia vile Subira aliangua kilio na kumfanya Thabit aingie kazi ya kumbembeleza.
“Mpenzi nyamaza japo zimepotea hizo bado hatutatetereka.”
“Naomba jioni twende kwa mtaalamu ili alinde mali zetu.”
“Lazima tufanye hivyo ni wapi?”
“Kigamboni.”
“Itabidi tuwahi kwenda.”
“Tuondoke saa kumi na mbili.”
Walikubaliana saa kumi na mbili kwenda Kigamboni kwa mganga, kukubali kwenda kwa mganga kulimfanya Subira kufurahia kuweza kumpeleka Thabit bila kujua na yeye kumaliza mambo yake ya kumdhibiti ikiwemo ndoa ya haraka.
Baada ya kukubaliana Subira alimpigia simu mzee Mukti kumjulisha mpango wa kumpeleka kwake umefanikiwa.
“Niambie binti,” alisema mzee Mukti baada ya kupokea simu.
“Babu kila kitu kimekwenda vizuri, jamaa kakubali kuja hivyo maliza kila kitu.”
“Hilo si la kuniambia bali ndiyo nilichokuwa nikikiomba usiku na mchana, mkitoka hapa utaniambia ndoa itavuma kwa kasi kama vumbi kwenye upepo mkali.”
“Yaani nitashukuru mzee wangu.”
“Kama amekubali mwenyewe jua amekwisha.”
“Basi jioni wageni wako.”
“Karibuni sana.”
Baada ya kukubaliana na mganga Subira alijipanga jioni kumpeleka Thabit ili akammalize kabisa.
CHINI YA BAHARI
hini ya bahari jini Hailat dada wa Nargis alirudi akiwa amechoka sana mwili ukiwa na mabaka ya moto. Mama yake alipomuona alishtuka na kutaka kujua mwanaye safari aliyokwenda amekutana na nini kilichomfanya aumie vile.
“He! Vipi tena mwanangu?”
“Mama hatari, wametuwahi!” alisema huku akijiangalia makovu ya moto.
“Kivipi?”
“Wamewahi kuzikinga mali zao japo tumefanikiwa kuharibu duka moja ambalo ndilo kubwa. Lakini mengine wameyakinga yanaonekana kama bahari nilipojaribu kuingia niliungua, bila uwezo wa kijini ningekufa kifo kibaya.
Mama sikubali nami naingia katika vita hii kuhakikisha namuondoa duniani Thabit na mganga wake sijali atakachokifanya Nargis, nipo tayari kwa lolote,” Hailat alisema huku akimwaga machozi ya hasira.
“Hebu tulia basi kazi hii nimekutuma mimi, nataka unisikilize mimi si mtu mwingine.
Kama umefanikiwa kuharibu mali moja tutajipanga kuharibu zote. Kuna kitu kimeingia kwenye akili yangu muda si mrefu. Kuna mali ya mabilioni ya Thabit ipo baharini inapita usiku huu utakwenda kuimaliza yote, hakikisha linabaki jivu.
Kwa pigo hilo tutakuwa tumemmaliza na mali zake zote zitakazopitia majini tutaziharibu, lazima atafilisika tu,” Malkia Zabeda alipanga kuyateketeza makontena yote kumi ya mali za Thabit na mali zote zitakazopita baharini.
“Sawa mama, kwa kazi hii sina haja ya kupumzika wala kusikilizia maumivu ya moto, tena nitaifanya mwenyewe bila kumshirikisha mtu,” Hailat alikubaliana na mama yake.
Hailat pamoja na maumivu ya moto lakini alifurahia kuziteketeza mali zote za Thabit zilizokuwa zikipita baharini usiku ule.
Alipanga kutopumzika na kuifanya usiku uleule ili asubuhi kila kitu kiwe kimekwisha. Alijipanga kuifuata meli yenye makontena ya bidhaa za watu na kuharibu za Thabit tu.
Hakutaka kuwashirikisha majini wengine kwa kuogopa taarifa kumfikia Nargis na kuharibu mpango mzima.
Aliamini hasara ya kuteketeza mali zile lazima zingemtia umaskini kwa kujua kwa mtindo ule lazima atayumba kifedha kwa vile wangeendelea kuharibu vitu vyote vitakavyopita njia ya bahari. Alihakikisha kila kona atakayoitumia kuingiza mali zake wanaziharibu.
***
Majira ya saa kumi na mbili jioni Thabit na Subira walivuka kivuko cha Feri mpaka Kigamboni. Baada ya kuvuka waliendelea na safari yao kuelekea Mji Mwema kwa mganga Mukti Buguju. Baada ya muda mfupi walifika nyumbani kwa mganga. Kwa vile Subira aliishamtaarifu kuwa wanakwenda walipokewa kwa heshima zote.
Hakukuwa na haja ya kukaa foleni, waliingizwa moja kwa moja chumba cha matibabu.
“Karibuni sana.”
“Asante,” waliitikia pamoja.
“Karibu mzee,” mzee Mukti alimkaribisha Thabit aliyeoneka kapendeza kwa fedha.
“Asante mzee wangu.”
“Jamani mna tatizo gani?” mzee Mukti alijifanya kama ndiyo siku ya kwanza kuonana na watu wale.
“Mzee wangu tuna tatizo, kuna vitu vimetutokea leo asubuhi ambavyo vinaonekana si vya kawaida,” Subira alianza kutoa maelezo.
Itaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment