“Sawa lakini tukimtia umaskini lazima yule mwanamke atamkimbia na wewe kupata nafasi ya kumpata mume wako.”
“Una uhakika gani kama huyo mwanamke atamkimbia, sitaki kuharibu chochote kwenye mali ya Thabit. Sitaki apate tatizo lolote ila nitahakikisha anarudi mikononi mwangu kwa jasho na damu.”
SASA ENDELEA...
“Sawa, kwa vile umeamua mwenyewe hatutaingilia uamuzi wako,” mama naye aliunga mkono.
Walikubaliana kuliacha lile jambo mpaka muda wa Nargis kurudi duniani na kujua watafanya nini. Baada ya Nargis kwenda chumbani kwake mama na dada yake walikuwa na kikao cha faragha kuhusiana na jambo lile ambalo Malkia Zabeda lilimuumiza sana akili kutokana na kumpenda sana mtoto wake wa mwisho Nargis.
“Mwanangu sasa tutafanyaje suala la mdogo wako?”
“Mama mimi msimamo wangu ni uleule, kama upo tayari nikamuulie mbali baba Zumza ili tumalize kero zote.”
“Hapana tutafute njia nyingine kwa vile unamjua vizuri mdogo wako kifo chochote na mumewe tutazua ugomvi mkubwa hata kupoteza uhai wa mmoja wenu.”
“Ndiyo maana mimi nimejitoa kwenye jambo hili najua lina lawama baadaye.”
“Kwa nini usitekeleze mpango nilioupanga?”
“Mpango gani?”
“Wa kumtia umaskini Thabit ili mwanamke aliyenaye amkimbie kwa vile najua amempenda kwa ajili ya mali kisha mdogo wako ampate mumewe.”
“Mamaaa! Bado tatizo litakuwa palepale.”
“Kwa nini?”
“Hata tukimrudisha, kwa vile wataendelea kuishi duniani tatizo lazima litajirudia huenda hilo likawa kubwa kuliko yaliyotangulia.”
“Wee fanya kwanza nilivyokutuma kilichobaki niachie mimi.”
“Sawa basi kazi hiyo nitaifanya usiku wa kesho ili akiamka siku ya pili akute amerudi katika umaskini.”
“Tena itatusaidia kwa vile miaka minne atamkuta amechoka kama mpira wa makaratasi.”
“Sawa mimi nitatekeza ulichonituma.”
“Ukifanya hivyo utanifurahisha sana, kazi itakayobaki niachie mimi,” Malkia Zabeda alifurahi mwanaye mkubwa kukubali kumsaidia mdogo wake.
Baada ya kikao kile cha faragha waliendelea na mambo mengine huku mpango ukiwa wa siri ambao Nargis hakuujua.
***
Baada ya Subira mipango yake kwenda kama alivyotaka na kufanikiwa kumteka kimapenzi Thabit bila kujua, aliianza siku kwa Thabit.
Alimuandalia kifungua kinywa kitamu kilichochanganywa na dawa ili asione tofauti ya mapishi ya kijini na kibinaadamu.
Baada ya kufungua kinywa waliondoka pamoja hadi kazini kama mke na mume. Thabit aliingia katika ofisi yake na kumuacha Subira akifanya majukumu yake kama msaidizi. Akiwa anaendelea na kazi alikumbuka kumueleza mzee Mukti kuhusu mipango ilivyokwenda.
Baada ya kumueleza hatua waliyofikia mganga naye alimueleza kuwa ameota ndoto iliyomtisha sana kuwa mali zote za Thabit zinateketea na moto na Thabit kawa maskini anayetembea mjini akiomba.
“Mungu wangu! Hilo si tatizo?” Subira alishtuka.
“Ni kweli tatizo, lazima usiku wa manane tuzunguke sehemu zote kwenye mali za mpenzi wako kuzizindika kwa vile inaonesha hali ya hatari ipo mbele juu ya mali hizo.”
“Sawa mzee wangu.”
Walikubaliana usiku wafanye zindiko kwenye maduka yote ya Thabit kabla kitu kibaya hakijatokea. Subira alifanya kazi moyo wake ukiwa umejaa hofu, alifikiria kumweleza Thabit ndoto ya mganga lakini alihofia kuulizwa ilikuwaje akajuana na mganga. Alitamani usiku uingie upesi ili wakaifanye kazi ile kabla tatizo halijatokea.
Majira ya saa saba usiku mganga Mukti Buguju aliongozana na Subira katika maduka ya Thabit kuyafanyia zindiko kabla tatizo aliloota halijatokea. Alianza na maduka mawili ya Kariakoo yaliyokuwa karibukaribu. Mzee Mukti na wasaizidi wake wakiwa katika vazi la shuka nyekundu waliyojifunga chini mgongo wazi na vilemba vyekundu. Mkononi alishika usinga huku msaizidi wake akiwa ameshika beseni lenye dawa.
Mganga alichovya usinga kwenye maji ya dawa na kumwagia kuzunguka ofisi kisha aliingia ndani na kufanya dawa zake kila kona na kutoka. Baada ya kumaliza duka moja alikwenda la pili na kufanya aliyofanya duka la kwanza. Baada ya kumaliza zoezi lile walipanda gari kuelekea Posta kwenye duka lililobakia.
Mzee Mukti hakuvua nguo za kazi na vijana wake mpaka maeneo ya Posta, walipokaribia jengo lenye duka la Thabit walishtuka kuona moto ukiwaka.
“Ha! Jengo linaungua,” Subira alipiga kelele.
“Kwani tunakwenda jengo gani?” mganga aliuliza.
“Hilo linaloungua.”
“Mmh!” mganga aliguna na kufanya Subira kushtuka.
“Vipi mbona unaguna?”
“Tunachelewa,” alisema mganga kwa sauti ya kukata tamaa.
“Tumechelewa nini?” Subira aliuliza.
“Ule moto si wa kawaida, kwani duka lake lipo wapi?”
“Pale moto unapowaka.”
“Tungejua tungeanza zoezi letu mapema, inaonesha ile ndoto leo ndiyo siku yake ya kuteketeza mali za Thabit ili arudi katika hali ya umaskini,” alisema mzee Mukti.
“Mungu wangu!” Subira alishika mikono kichwani.
“Majini wana hasira baada ya kushindwa kumrudisha Thabit kwao wameamua kuharibu mali zake ili arudi katika umaskini.”
“Kwa hiyo na yale maduka nayo yatateketea?”
“Yale yatakuwa salama hawataweza kufanya chochote kwa vile tumewahi tungechelewa ingekuwa kilio cha kusaga meno.”
Itaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment