Majira ya saa tano usiku alifuatwa na kijana wa mzee Mukti na kumwambia ajiandae kuna safari ya kwenda baharini.
Alipewa shuka nyekundu na kilemba chekundu na kuambiwa avue nguo zote ajifunge zile kisha asuburi. Baadaye aliitwa na nje alipofika alikuta watu wanne na mzee Mukti na kuelezwa.
“Sasa mama kazi ndiyo inakwenda kuanza kwa vile hali ya hewa inaruhusu.”
“Sawa.”
SASA ENDELEA…
Waliongozana kuelekea baharini wakiwa wamebeba kikapu chenye vitendea kazi na mbuzi mwekundu aliyekuwa amefungwa vitambaa vyekundu kwenye pembe. Subira kwa vile alikuwa mgeni alikaa katikati, msafara ulichukua dakika ishirini kufika baharini.
Walikuta maji yamejaa pomoni, alisimama pembeni ya maji, mzee Mukti alitoa vitendea kazi na kutengeneza mavazi yake mekundu. Baada ya mganga kupanga vitu vyake, Subira alielezwa ampande mgongoni na yule mbuzi alishikwa kwa mbele na kuingia naye ndani ya bahari.
Subira alikuwa akitetemeka kwa vile hali ya bahari ilikuwa tulivu lakini kulikuwa na milio ya kutisha. Hawakuijali waliendelea na kazi yao, alitembea na mbuzi yule mpaka maji ya kifuani wakiwa bado yupo chini. Wasiwasi wa Subira mbuzi yule kufa kwa kukosa hewa.
Baada ya kufika usawa ule mzee Mukti alishika usinga na kibuyu kidogo na kuingia nacho ndani ya maji. Baada ya kumsogelea Subira alizungumza kwa lugha anayoijua huku akimshika sikio la kulia kisha kumuwekea mkono katikati ya kichwa. Aliambiwa autazame mwezi na asipumue mpaka amalize kumshika kichwani. Baadaye alimuachia na kufanyika maombi mengine kazi iliendelea kwa zaidi ya saa mbili bila mbuzi aliyemkalia kutolewa ndani ya maji.
Baada ya zoezi kwenda vizuri alielezwa atoke, ajabu mbuzi aliyemkalia hakuwepo kwenye miguu yake. Alielezwa atoke ndani ya maji naye alifanya kama alivyoekekezwa. Alitoka mwenyewe bila mbuzi na kusikia wakisema:
“Kazi imekwenda vizuri tofauti na tulivyofikiria.”
Baadaye aliambiwa asogee pembeni ili aoge kisha warudi nyumbani, Subira alisogea pembeni na kuoga baada ya kuoga alipewa shuka nyeupe kujifunga kisha walirudi nyumbani. Walipofika mzee Mukti alimweleza:
“Kazi yako imekuwa rahisi tofauti na tulivyofikiria, mpeni chakula kisha apumzike ili asubuhi awahi kazini.”
“Sawa mzee,” waliitikia wasaidizi wake.
Baada ya kupata chakula na kuoga tena, alijifunga shuka nyeupe na kulala nayo hadi alfajiri alipoamshwa kuoga tena ili kujiandaa awahi kazini. Kabla ya kuondoka alipewa dawa nyingine.
“Hii utaiweka ndani ya maji kisha haya majani utatumia kunyunyiza kila kona ya ofisi kisha yatupe. Dawa hii inaua nguvu za kijini ambazo zipo pale ofisini.
Hii nyingine utainyunyizia kwenye meza ya bosi wako akigusana na pete mawasiliano yatakuwa yamekatika kati yake na mkewe jini, hivyo utatumia ile dawa ya chai na juisi kwa vile tayari tutakuwa tumekata mawasiliano.
Mtakapoanza uhusiano usikubali kukutana naye mpaka uje huku kuna dawa nitakupa kuhakikisha unakuwa salama katika penzi lako na kuifanya ndoa yako iwe ya haraka. Nina imani ikifanya kwa kuzingatia maelezo yangu utashangaa mwenyewe.”
“Nashukuru mzee wangu, nakuahidi zawadi kubwa.”
“Wewe tu kazi yangu nimemaliza.”
Baada ya kupewa dawa na maelekezo Subira aliondoka kuwahi kazini, alikodi Bajaj ambayo ilimpeleka moja kwa moja mpaka ofisini. Siku ile aliwahi kazini tofauti na siku zote mpaka mlinzi alishangaa.
Baada ya kuingia ofisi kwa bosi wake, alianza usafi mara moja kisha alichukua kikombe cha chai na kuweka maji kidogo na kuweka dawa ya unga na kuikoroga kisha alichukua majani aliyopewa na kuanza kunyunyiza ndani ya ofisi. Ghafla mle ndani ulitokea mtikisiko mkubwa , Subira alitoka mbio kuhofia uhai wake na kwenda kusimama pembeni ya ofisi huku akitweta.
Bahati nzuri alitoka na mkoba wake na kumpigia simu mzee Mukti ili kumweleza yaliyotokea huku yakizidi kumkatisha tamaa. Baada ya kuita kwa muda mfupi ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo.”
“Haloo mzee.”
“Vipi mbona hivyo?”
“Huku kuna tatizo lingine limetokea.”
“Tatizo gani?”
Subira alimwelezea kilichotokea muda mfupi baada ya kuanza kunyunyiza dawa aliyompa.
“Kumbe ni hilo endelea tu.”
“Mzee yaani mtikisiko mpaka mwenyewe nikashtuka, hapa nilipo natetemeka mwili hauna nguvu kabisa halafu unaniambia niendelee?”
“Zile ndizo nguvu za kijini zilizomo ofisini, unaponyunyiza maji huo mtikisiko uliousikia ni kuvunjika kwa nguvu hizo. Kwa hiyo kaendelee wala usihofu, jitahidi umalize zoezi kabla bosi wako hajafika.”
“Sawa.”
Subira alirudi ofisini akiwa hajiamini, alichukua kikombe chenye maji na kuanza kunyunyiza ile dawa. Mtikisiko wa mwanzo ulijirudia tena lakini hakuacha aliendelea kufanya hivyo kila kona ya ofisi na hali ya mtikisiko ilitulia. Baada ya zoezi lile kwenda vizuri alichukua dawa nyingine na kuipaka kwenye meza na kurudi sehemu yake ya kazi.
Majira ya saa tatu na nusu asubuhi Mustafa aliingia ofisini, kama kawaida aliachia tabasamu lililokuwa likimtesa Subira. Baada ya kusalimiana aliingia ofisini kwake kuendelea na kazi. Haikuchukua muda kishindo kizito kilitokea ndani ya ofisi kilichomshtua Subira na kujiuliza kulikuwa na kitu gani ndani.
Inaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment