Jeshi la polisi mkoani Geita, limefanikiwa kulitia mbaroni jambazi moja na kufanikisha kuzinasa bunduki sita ambazo ziliporwa na kundi la majambazi usiku wa kumkia juzi katika kituo cha polisi wilayani Bukombe.
Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema jambazi hilo lilinaswa porini likiwa na silaha hizo ambazo ziliporwa baada ya kuvamia kituo hicho na kuua polisi wawili papo hapo na kujeruhi wengine wawili.
“Hawa majambazi wameonekana kujichanganya na wafugaji waliopo mipakani, hivyo uhalifu wao wakifanya wanakimbilia kwa wafugaji…natangaza kuanzia sasa wale wafugaji waliopo pembezoni mwa mipaka kuondoka mara moja ili kutowapa nafasi majambazi kujificha,” alisema Mangu.
Hata hivyo, Mangu alisema baadhi ya mapori ya akiba katika mikoa ya Kagera, Geita, Kigoma na Shinyanga yamegeuzwa maficho ya wahalifu na mikakati inafanyika kutafuta ufumbuzi wa kudumu badala ya ukanda wa mapori hayo kutangazwa kanda maalum ya mikoa ya kipolisi.
Akikwepa kulihusisha tukio la juzi la kuvamiwa kwa kituo cha polisi na kuuawa kwa polisi wawili na kujeruhi wengine na kuondoka silaha mbalimbali zikiwamo bunduki aina ya SMG, risasi na mabomu ya kutupa kwa mkono, alisema matokeo ya uchunguzi ndiyo yatabainisha ukweli halisi.
Alisema baadhi ya wahalifu hutoka nchi jirani na kushirikiana na baadhi ya wenyeji kwa kutumia mapori ya akiba na baadhi ya hifadhi kujificha kabla na baada ya kutekeleza uhalifu wao.
Alisema operesheni rasmi ya kuwasaka watuhumiwa waliohusika na tukio la uvamizi wa kituo cha polisi cha Bushirombo imeanza baada ya kikao cha kamati ya ulinzi na usalama cha mkoa wa Geita kufanyika juzi.
Juzi watu wanaoaminika ni majambazi walivamia kituo cha polisi cha Bushirombo ambacho makao makuu ya polisi wilaya ya Bukombe kushambulia na kuwaua polisi WP 7106 Uria Mwandiga na G.2615 Pc Dustani Kimati.
Waliojeruhiwa ni E.5831 CPL David Ngupama Mwalugelwa aliyeumizwa kichwa na usoni pamoja na kung’olewa meno mawili, huku H.627 Mohamed Hassani akijeruhiwa kifuani.
No comments:
Post a Comment