Majira ya saa tatu na nusu asubuhi Mustafa aliingia ofisini, kama kawaida aliachia tabasamu lililokuwa likimtesa Subira. Baada ya kusalimiana aliingia ofisini kwake kuendelea na kazi. Haikuchukua muda kishindo kizito kilitokea ndani ya ofisi kilichomshtua Subira na kujiuliza kuna kitu gani ndani.
ENDELEA...
Alinyanyuka taratibu huku mapigo ya moyo yakiwa juu na kugonga ofisini kwa bosi wake taratibu. Hakukuwa na majibu yoyote, ile hali ilizidi kumtisha aligonga tena kwa nguvu kidogo huku akimwita kwa jina lake.
“Bosi…bosi.”
Vilevile hakukuwa na jibu, aliufungua mlango taratibu na kuchungulia ndani, alishtuka kumuona bosi wake akiwa amejilaza kwenye meza huku kidoleni pete yake ikionesha kama moto unawaka. Alijiuliza kile ni nini kwa vile hakuelezwa na mganga kutokea na kitu kile.
Alimsogelea huku akitetemeka alimtikisa akimwita, lakini hakukuwa na jibu, alipomuangalia vizuri aligundua amepoteza fahamu. Haraka alirudi ofisini kwake na kumpigia simu mzee Mukti ili kumpa kinachoendelea pale ofisini.
“Vipi binti?” aliuliza baada ya kupokea.
“Mzee wangu kila dakika kunatokea kitu cha ajabu.”
“Kitu gani?”
“Baada ya bosi kuingia, ilichukua muda mfupi kusikia kishindo kizito, nilipoingia ndani nimemkuta amelalia meza akiwa amepoteza fahamu. Kilichonishtua zaidi pete aliyovaa inawaka moto.”
“Hiyo kawaida wala usihofu zoezi limekwenda vizuri sana, umenifurahisha kufanya kama nilivyokuelekeza.”
“Mzee zoezi limeenda vizuri wakati hali ya bosi ni mbaya?” Subira alimshangaa mzee Mukti kusema vile.
“Kazi imeisha, sasa fanya hivi mvue pete hiyo iweke kwenye maji yaliyochanganywa na dawa iliyopakaza kwenye meza kwa dakika tano. Kisha utaitoa na kumvisha kidoleni na kumuacha bila kumfanya chochote.
Ukitoka hapo kamuandalie chai, akishtuka mpe chai kisha endelea na kazi. Mchana mpe juisi kitakachofuata utanijulisha. Nilitaka kusahau na lingekuwa kosa kubwa, kabla hujaishika pete jipake dawa hiyo mkononi.”
“Sawa mzee.”
Subira alifanya kama alivyoelekezwa kwa kuweka maji kidogo kwenye kikombe na kuchanganya na dawa, alijipaka dawa mikononi kisha alimvua pete iliyokuwa ikiwaka moto huku akitetemeka na kuiweka kwenye kikombe.
Ilipogusa maji moto ilizimika kama kaa la moto huku ikitoa moshi na kutulia. Baada ya zoezi lile aliifuta pete kumvisha tena na kutoka ofisini kwa bosi wake kwenda kumtengeneza chai ili amalize zoezi la asubuhi.
Baada ya kuchemsha chai aliweka kwenye chupa na kurudi kuendelea na kazi, lakini kazi ilimshinda kwani hakujua hatima ya bosi wake.
Kompyuta aliiwasha na kutulia akiiangalia huku akisubiri kitakachoendelea. Baada ya dakika kumi alishtushwa na sauti ya Thabit.
“Subira.”
“E..eeeh! Abee bosi,” Subira alishtuka toka katika dimbwi la mawazo.
“
Chai tayari maana nashangaa nasikia mwili kuchoka ghafla,” Thabit alisema huku akijinyoosha.
“Tayari.”
“Ndiyo maana nakupenda.”
“Nioe basi,” Subira alijikuta akiropoka.
“Kila kitu mipango.”
Subira alijikuta alijishtukia kwenda mbali zaidi wakati zoezi aliloambiwa na mzee Mukti lilikuwa halijakamilika.
Alikwenda jikoni kuchukua chai kabla ya kuibeba aliweka dawa na kuikoroga vizuri kisha alibeba kikombe kumpelelea bosi wake. Aliitenga juu ya meza na kusema kwa unyenyekevu:
“Karibu chai bosi.”
“Asante,” Thabit alisema huku akichukua kikombe cha chai ili akipeleke mdomoni.
Subira alishindwa kuondoka alisimama akiangalia nini kitatokea wakati huo mapigo ya moyo yalikuwa juu. Wakati akikipeleka kikombe mdomoni hali ilikuwa mbaya kwake jasho la hofu lilimtoka na kubana pumzi.
Thabit alipiga funda mbili za haraka kutokana na moto wa chai na kumumunya midomo kisha alisema:
“Dah! Subira unajua kupika chai, umeolewa?”
“Sijaolewa.”
“Mmh! Sawa, chai tamu sana.”
“Kwani vipi?”
“Kaendelee na kazi.”
Subira hakuongeza neno alitoka na kwenda ofisini kwake huku akizidi kuyaona maajabu ya mzee Mukti pale bosi wake alipokunywa chai bila kikombe kupasuka. Alitaka kumpigia simu mzee Mukti Buguju kumweleza alipofikia lakini aliona mapema alisubiri aone kinachoendelea.
***
Thabit akiwa ofisini kwake alijiona mtu tofauti na alivyojizoea kwa kipindi kirefu, aliushangaa uzuri wa sekretari wake. Kwake alikuwa kama kiumbe kipya ambacho hakuwahi kukiona siku za nyuma. Alinyanyua simu na kumwita ofisini kwake ili amuulize kitu.
Baada ya muda Subira alisimama mbele yake huku akiachia tabasamu pana lililozidi kuuteketeza moyo wa bosi wake.
“Abee bosi.”
“Kaa.”
Subira alikaa na kumtazama bosi wake aliyeonekana kumshangaa kitu kilichomfanya amuhoji.
“Bosi mbona unanishangaa?”
“Una muda gani hapa kazini?”
“Miaka mitano sasa.”
“Miaka hiyo mitano! Ulikuwa ukifanya sehemu gani?”
“Kama msaidizi wako.”
“Muongo, mbona nilikuwa sikuoni?”
“Kweli bosi, basi tu labda sina mvuto moyoni mwako.”
“Hapana, umeolewa?”
“Bado.”
“Una mchumba?”
“Sina.”
“Jiandae mchana tukapate chakula cha pamoja kwa mazungumzo zaidi.”
“Bosi wewe si unakula kwako?”
“Ndiyo.”
“Kwa hiyo nikale na wewe kwako?”
Itaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment