Social Icons

Saturday, 13 September 2014

Mabasi ya Super Feo wafungiwa kusafirisha abiria


 
Na Emanuel Madafa,Mbeya

Kufuatia kuwepo kwa ongezeko la ajali za barabarani nchini hususani kwa Mkoa wa Mbeya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini, SUMATRA Mkoani Mbeya imesitisha leseni za mabasi ya kampuni tano za usafirishaji wa abiria mkoani hapa yakiwemo mabasi ya Super Feo kutokana na kukiuka sheria za barabarani.
 
Kaimu Afisa Mfawidhi wa SUMATRA, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Denis Daud, alisema Super Feo imesitishiwa leseni za mabasi yake kuanzia Septemba 11 mwaka huu.
 
Amesema hali hiyo ni  kutokana na basi lake lenye namba za usajili T 273 CDD lililokuwa likitokea Songea kwenda Mbeya kupata ajali katika eneo la Sanangura Songea na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi 24 kutokana na mwendo kasi.
 
Amesema, kwa mujibu wa taarifa za awali za uchunguzi, kutoka Jeshi la Polisi, chanzo cha ajali hiyo ilisababishwa na mwendokasi uliosababisha kugonga mti na kupinduka.
 
Amebainisha kuwa kwa kuzingatia kifungu namba 15 cha sheria ya SUMATRA na pia kanuni namba 22 ya kanuni za ufundi, Usalama na Ubora wa Huduma za Mwaka 2008, Mamlaka inasitisha lesseni ya usafirishaji kwa mabasi ya Kampuni ya Super Feo kutoa huduma katika njia zote Tanzania tarehe 11/9/2014.
 
Amesema,  mabasi hayo ambayo yanamilikiwa na mmiliki Moses Amlani, hayataruhusiwa kujishughuisha na shughuli zozote zile za usafirishaji  mpaka hapo, muhusika atakapotekeleza baadhi ya masharti yaliyopendekezwa na mamlaka hiyo.
 
Aidha, Daudi, amesema kuwa moja ya masharti ambayo mmiliki atatakiwa kuyatekeleza ni pamoja na kuwasilisha vyeti vya mafunzo ya kuendesha abiria(PSV) vya madereva wake pamoja na kujaribiwa na jeshi la polisi kwa lengo la kujiridhisha kama wana sifa za kuendesha mabasi.
 
Amesema, lingine ni mmiliki kuwasilisha na kukaguliwa na SUMATRA mikataba ya ajira ya madereva wote wa kampuni yake pamoja na kadi za uanachama wa mifuko ya pensheni.
 
Pia, SUMATRA imesitisha leseni za mabasi manne yanayosafirisha abiria kati ya Mbeya Mjini na Ubaruku wilayani Mbarali kutokana na kushiriki katika mgomo kwa kufunga barabara ili kuzuia shughuli za usafirishaji kwa lengo la kushinikiza madai yao kwa Serikali.
 
Amesema, kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni Na. 18(i) (b) na 32 (1) (h) ya kanuni za leseni za usafirishaji(Magari ya abiria) 2007 na kupitia kifungu Na. 15 cha sheria ya SUMATRA, mamlaka imeamua kusitisha leseni zao na kwamba wahusika hao hawatajihusisha kutoa huduma ya usafirishaji.
 
Aliyataja magari hayo kuwa ni Coaster yenye namba T423 BSA ambayo inafanya shughuli zake za kusafirisha abiria Mbeya- Rujewa, Coaster T339 safari za Mbeya- Rujewa, Coaster namba T640 BAN pamoja na Fuso namba T968.
 
Hata hivyo, Afisa huyo, aliwataka madereva na wamiliki wa magari kuzingatia sheria na kanuni za utoaji wa huduma kwa jamii kwani mamlaka haitasita kuwachukulia hatua watu watakao kuka taratibu hizo ili iwe fundisho pamoja na kupunguza idadi ya vifo vya watu vinavyotokana na uzembe.

No comments:

 
 
Blogger Templates