Social Icons

Saturday, 13 September 2014

Mangula atumia saa tisa kuweka mambo sawa Mbeya Vijijini


Mbalizi. Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Philip Mangula juzi alitumia saa tisa mfululizo kuzungumza na viongozi wa CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini katika kuweka sawa mambo ambayo hayaendi vizuri kichama.

Katibu Mwenezi wa CCM mkoani hapa, Bashiru Madodi alisema Mangula alifanya kikao na wajumbe wa Kamati ya Siasa wa wilaya na baadaye wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya.

Madodi alisema kikao hicho kilianza saa 2.00 asubuhi ya juzi na kumalizika saa 11.00 jioni, lakini hakutaka kuzungumzia mambo yaliyokuwa yakijadiliwa.

Juzi ilikuwa siku yake ya kwanza kwa Mangula ya kufanya vikao vya aina hiyo tangu alipowasili Jumatano ya wiki hii, ambapo jana alitarajiwa kuwa wilayani Rungwe kuendelea na vikao kama hivyo.

Mangula ambaye ni mlezi wa CCM mkoani hapa, alilazimika kutua Mbeya baada ya kuwapo mitafaruku mingi ndani ya chama hicho ukiwamo ule wa kufukuza uongozi katika Wilaya ya Ileje.

Makada wa CCM mkoani Mbeya wamekuwa mwiba kwa chama hicho pale wanapoonyesha nia ya kutaka ubunge mwakani, huku wakifadhili mashindano ya mpira wa miguu na wengine kuunda vikundi vya Bodaboda kwa lengo la kuwasaidia.

Chanzo Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates