Social Icons

Saturday, 13 September 2014

Sitta ageuka mbogo, awashambulia wasomi

Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, amejibu mapigo akiwashambulia wasomi wanaohoji uhalali wa wajumbe wa Bunge hilo kupiga kura wakiwa nje ya nchi, akisema wasomi hao wanachanganya sheria za nchi.

Sitta aliwafananisha viongozi wa Ukawa na wasanii waigizaji, akitabiri kuwa watashindwa vibaya katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Halikadhalika, mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo ‘kuwapoza’ wajumbe ambao ni waumini wa Dini ya Kiislamu wanaopaza sauti wakitaka Mahakama ya Kadhi itambuliwe, akisema kuna ‘namna’ itaingizwa kwenye Katiba.

Sitta alitoa matamko hayo mawili jana, wakati akiendesha vikao vya Bunge hilo mjini Dodoma, katika kipindi ambacho suala la Mahakama ya Kadhi likiwa limewagawa wajumbe wa Bunge hilo katika makundi mawili kwa misingi ya imani za dini zao.

Alianza kwa suala la wasomi mbalimbali wanaohoji uhalali wa Bunge hilo kutaka kuruhusu wajumbe wake watakaokuwa nje ya nchi, kupiga kura ya uamuzi kupitisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa akisema:

“Kuna watu wanaojiita wasomi, nadhani wanaohusiana na hao wanaoitwa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) ambao jitihada yao kubwa sana ni kuzuia kabisa isipatikane katiba.” Sitta akaongeza kusema, “Leo (jana) nimemsikia mmoja anasema kwamba kupiga kura (nje) itakuwa sivyo tutakuwa tanavunja katiba ya nchi. Huyu mtu kasoma sheria ya uchaguzi,” alisema.

“Sisi hatupigi kura ya uchaguzi tunapiga kura ya uamuzi. Ni kura ya uamuzi kuhusu suala ambalo wajumbe hao wana haki ya kupiga kura na kushiriki katika kuamua juu ya katiba,” alisisitiza Sitta.

Akijenga msingi wa uamuzi huo, Sitta alitolea mfano kuwa wakati wa upigaji wa kura katika hatua ya kamati, wapo wajumbe waliopiga kura zao wakiwa hospitalini.

“Ndio maana hata wakati wa kamati tulipigisha kura hata hospitali kwa hiyo hili ni jambo la kawaida kabisa wala msifadhaike watu wameamua tu kujisema wanayotaka,”alisisitiza.

Baada ya dakika 70 hivi kupita, Sitta akasimama tena na kusema wapo wajumbe wamesoma kwenye vyombo vya habari kwamba Ukawa wanapanga kumpeleka yeye (Sitta) katika mahakama ya Kimataifa ya The Hague, nchini Uholanzi.

“Ni waigizaji wazuri sana. Hebu fikirieni vituko vyao. Tulipokuwa hapa mwanzoni tumevutana siku 18 kuhusu kura ya wazi ama ya siri. siku ya kuzikubali kanuni watu hawa waliopigania kura za siri kufa na kupona wakapiga kura za wazi”.

Sitta akaendelea kusema” Haya wakaleta tishio na sio tishio tu wakamtuma mwenzao akaleta hoja binafsi kwamba Bunge hili lisiendelee hadi hati ya muungano ipatikane”.

Chanzo Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates