Social Icons

Sunday, 14 September 2014

Uchaguzi CHADEMA waleta sura mpya


KATIKA hali ambayo haikutarajiwa na wengi, Uchaguzi Mkuu wa ndani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeonekana kuwa wenye mchuano mkali huku majina ya wanasiasa wenye ushawishi katika chama hicho waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi yakishindwa kutamba.

Mwenendo huo unaochukua mwelekeo wa kuwepo mapinduzi ya kiuongozi ndani ya jumuiya za chama hicho, ulijitokeza jana wakati wa uchaguzi wa viongozi wapya wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (BAWACHA).

Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, mwanasiasa kijana na mwenye ushawishi mkubwa, Halima James Mdee, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa BAWACHA akishinda kwa kishindo wanasiasa wenzake wanawake wenye majina makubwa ndani ya chama.

Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, aliibuka kidedea kwa kunyakua kura 165 na kuwashinda Chiku Abwao ambaye alipata kura 15, Rebecca Magwisha (4) Lilian Wassira (11), Sophia Mwakagenda (18) na Janeth Rite (35).

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alipokutana na waandishi wa habari kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, alisema Mwenyekiti wa BAWACHA Mkoa wa Shinyanga, Rachel Mashishanga ambaye pia ni Mbunge wa viti maalumu aliyekuwa akigombea nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu naye alishindwa.

Makene alimtaja pia Esther Matiko ambaye ni mbunge kuwa naye alishindwa kutamba katika mchuano wa kuwania nafasi ya kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu.

Kwa mujibu wa Makene, mbunge wa nne kuangukia pua katika uchaguzi huo ni Mariam Msabaha aliyekuwa akiwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa BAWACHA Zanzibar na kupata kura 36 huku mpinzani wake, Hamida Abdallah akiibuka na ushindi mnono wa kura 194.

Katika hali iliyowashangaza wengi, Msabaha akiwa miongoni mwa wagombea walioshindwa alianza kububujikwa machozi baada ya matokeo kutangazwa na kuwalazimu makada wenzake waliokuwa karibu naye kumbembeleza kwa kumfuta machozi huku wakimfariji kuwa katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa na asiyekubali kushindwa si mshindani.

Ukiachilia mbali Msabaha, wagombea wengine wenye majina makubwa ndani ya jumuiya hiyo walioshindwa walionekana kuwa katika hali ya huzuni na walikataa kuzungumza na waandishi wa habari.

Kwa namna hiyo hiyo yenye mwelekeo wa kuwepo mapinduzi makubwa ya kiuongozi ndani ya jumuiya za chama hicho, Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul, aliyekuwa akiwania nafasi ya Katibu Mkuu wa BAWACHA naye aliangushwa vibaya na Grace Tendega aliyewahi kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga.

Dodoso lililofanywa na MTANZANIA Jumamosi kwa wafuatiliaji wa siasa za ndani na nje ya Chadema kuhusu mwenendo huo wa uchaguzi, limeonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa wafuasi wengi wa chama hicho ni vijana na hilo linathibitishwa na wingi wa ushiriki wao katika shughuli za uchaguzi unaoendelea.

Aidha, wafuatiliaji wa uchaguzi huo waliofikiwa na gazeti hili walieleza kufurahishwa na mwenendo wa kampeni na hata matokeo ambayo kwa kiwango kikubwa yamewaacha nje ya nafasi za uongozi baadhi ya wagombea waliokuwa wakitajwa kutumia fedha kusaka ushindi.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti mpya wa BAWACHA, Mdee, baada ya kutangazwa mshindi na kupewa nafasi ya kutoa neno la shukrani kwa wajumbe huku akitokwa na machozi ya furaha alieleza kusikitishwa na majungu, fitina na maneno ya uongo yaliyokuwa yakisambazwa juu yake wakati wa kampeni.

“Siku mbili zilizopita nimepungua uzito kwa sababu ya maneno, fitina, majungu na uongo yaliyokuwa yakisambazwa dhidi yangu lakini sitaki kufika huko, nimewasamehe wote,” alisema Mdee.

Huku akishangiliwa na wanachama waliokuwa kwenye ukumbi huo, Mdee alisema kuwa heshima aliyopewa imetuma ujumbe mzito kwa wote waliokuwa na nia mbaya na yeye.

“Huu ni ujumbe mzito kwao, sasa waelewe kuwa nitapanda jukwaani kwa hoja na si kwa vioja. Kwa sisi ambao tulianza siasa muda mrefu tumezoea maneno ya kashfa, lakini inasikitisha sana ukiona mwanamke mwenzako anakukashifu.

“Bila mwanamke hakuna Ikulu kwa sababu akishakuamini ni vigumu kukusaliti, sasa tukiwa wamoja tutafika mbali na tufufue upeo wa mwanamke uliozibwa kwa muda mrefu,” alisema Mdee.

Alisema mikakati yake ni kuwavuta wanawake ambao wametekwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na vijana wa kike ambao hawaamini kuwa wanaweza kupata wadhifa.

“Vijana wengi wanaogopa kuingia kwenye siasa za upinzani. Pia kwa wiki mbili hizi au tatu mimi na safu yangu tutajipanga vizuri tunajua fedha ni changamoto lakini tukiamua kufanya kazi kwa umoja fedha si tatizo,” alisema Mdee.

Kumalizika kwa uchaguzi wa BAWACHA kunatoa nafasi ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu ambao utamchagua Mwenyekiti wa Taifa na makamu wake hapo kesho.

Chanzo Mtanzania

No comments:

 
 
Blogger Templates