Social Icons

Saturday, 13 September 2014

HADITHI: Nilioa jini nikamsaliti -17


Kutokana na uchungu moyoni alijikuta akilia na machozi kumtoka, kwa vile alikuwa ameinama machozi yake yalitua kwenye paji la uso wa mumewe. Alishangaa kumwona akibadilika rangi mchanganyiko huku mwili ukitikisika kisha ilirudi yake ya kawaida na mwili ulitulia.

Alimuona Thabit  akifumbua macho na kupepesa kisha alijinyoosha kuonesha yupo sawa. Nargis alitaka kumsemesha lakini hakutakiwa kufanya vile kwa vile sicho kilichompeleka muda ule.

Aliamini kila alichokipanga kilikwenda kama alivyotaka aligeuka na kuondoka na kumuacha mumewe akiwa hajambo na kuamini taarifa atakayoisikia juu ya mali zake kurudi atamuongezea furaha. Kwa vile alikuwa ametoka usiku sana aliwahi kurudi chini ya bahari kabla familia yake haijagundua kutoka kwake.

Thabit baada ya kujiona yupo vizuri alinyanyuka kitandani na kutoka nje ya wodi, muuguzi alishtuka sana kumuona mtu aliyekuwa yupo hoi hajiwezi ameweza kunyanyuka kitandani na kutembea kama kawaida.
“Kaka vipi?”
“Safi.”

‘Si...si ni wewe uliyekuwa u...u..kiumwa?” muuguzi alishtuka.
“Ndiyo.”
“Mmh! Haya ni maajabu, muda mfupi ulikuwa hoi na mimi nimetoka kukuhudumia. Nashangaa kukuona ukiwa mzima…halafu kuna dada alikuja kukuona yupo wapi?”

Wakati Nargis akija katika umbile la kibinadamu alikutananaye akitoka kumpa dawa mgonjwa akiwa hajiwezi. Lakini dakika chache alishtuka kumuona akitoka akiwa mzima wa afya njema kama hakuwahi kuugua ugonjwa wowote, lakini yule dada mrembo hakumuona.
“Dada gani?” Thabit alishtuka.

“Kuna dada mmoja mrembo sana, aliniomba akuone, nilipomkatalia alianza kulia kwa kusema wewe ni mtu wake muhimu sana na asipokuona leo itachukua muda wa miaka minne kuonana. Nilimruhusu lakini ajabu alivyotoka sikumuona na wewe kukuona hujambo.”

“Kwa kweli sijamuona mtu, ila namshukuru Mungu sasa sijambo.”
Thabit akiwa bado anazungumza na muuguzi aliyemshangaa simu yake iliita.
“Haloo.”

“Asalam aleykum mpenzi?”
“Waleykum salam, mpenzi wangu nani?”
“Huwezi kunitambua kwa kujieleza mpaka unione, nilitaka kukujulisha nimefurahi kukuona umepona pia mali zako zote zipo kama kawaida.”
“Mali zangu zipi?”

“Kwani kipi kilichokufanya uugue ghafla?”
“Mmh! Za dukani.”

“Basi kila kitu kipo vizuri, ila kumbuka ahadi.”
“Ahadi gani?”
“Utaijua baada ya miaka minne.”
“Sawa.”

“Kwaheri ya kuonana,” baada ya ujumbe wa utata Nargis alikata simu na kurudi zake chini ya bahari.
Baada simu ya Nargis kukatika bila kumshtua Thabit juu ya ahadi aliyowekeana na mkewe siku aliporudi chini ya bahari kujifungua baada ya kuvurugwa akili na Subira na kumfanya asimkumbuke tena mkewe Nargis.

“Kaka naomba niwasiliane na mganga mkuu ili nimueleze maajabu haya ili nijue atafanya nini,” muuguzi alishindwa kumruhusu.
“Hakuna tatizo niache niondoke .”
“Subiri.”

Muuguzi alimjulisha mganga mkuu aliyefika pale na kumshangaa Thabit ambaye walikuwa wakipanga kumpeleka nje ya nchi kimatibabu. 
“Haya ni maajabu, mtu uliyekuwa hujiwezi lakini ghafla umepona!”
“Kwani nilikuwa naumwa sana?”

“Kila aliyekuona alikuwa akilia, mpaka sasa hivi naona kama ndoto.”
“Yote ni maajabu ya Mungu.”
“Basi tunaomba tukufanyie vipimo kabla ya kukuruhusu kwa vile bado akili yangu haiamini.”
“Hakuna tatizo.”

Walikwenda chumba cha uchunguzi ili kumfanyia uchunguzi wa kina Thabit, muda wote muuguzi na mganga mkuu walikuwa wakijiona kama wapo ndotoni. Wakiwa chumba cha uchunguzi simu ya Thabit iliita, alipoangalia ilikuwa ikitoka kwa msaidizi wake.
“Haloo.”
“Bosi?”
“Ndiyo.”

“Haya ni maajabu ya karne.”
“Kwa nini?”

“Kuna simu nimepigiwa na mwanamke mmoja yenye lafudhi ya mwambao na kunieleza kuwa vitu vyote vya bosi wako vimerudi kama zamani, vyote tulivyoviona ilikuwa kiini macho. Niliondoka hadi kwenye makontena na kukuta kweli vitu vyote tulivyoagiza vipo.

“Kingine alichoniambie eti hata ugonjwa wako ni kiini macho na kama siamini baaada ya kuona vitu vyote nikupigie simu. Baada ya kukuta vitu vyote vipo nimekupigia simu na wewe kupokea na kukuta hujambo haya ni maajabu ya karne.”

“Hata mimi mtu huyo kanipigia simu na kunieleza kuwa vitu vyangu vimerudi.”
“Ni nani?”

“Hata simjui amesema nitamjua baada ya miaka minne.”
“Sasa atakuwa nani?”
“Akija tutamuona.”

“Basi bosi lazima tufanye sherehe kubwa.”
“Lazima tufanye.”

Baada ya kuzungumza na msaidizi wake, alifanyiwa vipimo vilivyoonesha hakuwa na tatizo lolote mwilini. Kabla ya kuondoka alimpigia simu Subira aliyekuwa amefuata dawa Kigamboni kwa mzee Mukti. Baada ya kupokea alishtuka na kusikia anayezungumza ni mpenzi wake Thabit alikataa.
“Wewe unayezungumza ni nani?” Subira hakuamini kusikia sauti ya mpenzi wake.
“Nini mpenzi wako.”

“Hebu acha utani, niambie wewe ni nani?”
“Subira mpenzi wangu ni mimi Thabit mpenzi wako.”
“Siwezi kuamini wewe si Thabit,” Subira alikataa katakata.

“Nifanye nini ili ujue mimi ni mpenzi wako?”
“Hata ufanyeje siwezi kukukubalia,” Subira alibisha kutokana na hali aliyomuachanayo jioni ile.

Itaendelea 

Chanzo globalpublishers 


No comments:

 
 
Blogger Templates