Kila Ijumaa ya wiki kuna kundi la mashabiki wanaelekea maeneo ya Mbezi Beach kumwangalia gwiji wa muziki wa dansi anayezeeka na utamu wake, injini ya bendi ya La Capital, King Kikii ambaye ni maarufu kwa kupeperusha kitambaa cheupe.
Anaitwa Kikumbi Mwanza wa Mpango, ambaye kwa mara ya kwanza alikuja nchini mwanzoni mwa miaka ya 70 akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na bendi iliyojulikana kwa jina la Fouvette Jazz Band, promota aliyewakaribisha alikuwa Fred Ndala Kasheba (Kwa sasa ni marehemu).
Wengi wanaamini kwamba uzuri wa muziki wa bendi hii, ni kwa sababu tu kiongozi wake huyu anatokea eneo ambalo pia lilitoa mastaa wengi wa muziki wa dansi kama kina Franco wa OK Jazz, Tabu Ley wa African Fiesta, Kabasele ya Mpanya (Pepee Kale) wa Empire Bakuba na mpiga gitaa bora aliyewahi kutokea Diblo Dibala na mpinzani wake mkubwa Dali Kimoko.
Katika mahojiano yetu, tumepata fursa ya kumuuliza King Kikii, ni lini aliamini kwamba yeye ni mwanamuziki na kiukweli akasema anajikumbuka alipoanza kuimba na bendi ya Fauvette, alianza kwa nyimbo mbili zilizotamba sana, nazo ni ‘Jacqueline’ na ‘Kamarade ya Nzela’ ambazo ndiyo zilianzisha safari yake ya kuja Tanzania.
Baada ya ziara ya mwanzoni mwa miaka ya 70, watu walimpenda, aliondoka kisha akarudi tena mwaka 1977 kujiunga na bendi ya Maquis du Zaire iliyokuwa ikiongozwa wakati huo na Chinyama Chianza (Marehemu). Mtindo uliokuwa unawika wakati huo ulikuwa ukijulikana kama ‘Kamanyola Bila Jasho” na hapo akaonyesha cheche zake kwenye vibao ‘Nimepigwa Ngwala’ na ‘Kyembe’.
Miaka miwili baadaye, akatafutwa na tajiri mmoja aliyekuwa akiitwa Hugo Kisima, akalipwa ili kuachana na Marquiz, ili aongoze bendi ya mfanyabiashara huyo aliyekuwa akimiliki bendi ya Orchestra Safari Sounds ambako alienda kutambulisha mtindo mpya wa ‘Masantula Ngoma ya Mpwita’ na baadaye mtindo ukabadilika na kuwa ‘Duku Duku’.
Moja kati ya kumbukumbu zisizosahaulika katika enzi za masantula ni wimbo ‘Mimi Msafiri’ na hii ilikuwa ni kama bendi ya mwisho kwa wakati ule kwani aliondoka tena na kuanzisha bendi ya Double O ambayo baadaye nayo ikafa akaishia kuwa msanii mgeni au msanii mwalikwa katika bendi mbalimbali.
Moja kati ya bendi ambazo alikuwa akishiriki maonyesho yake bila kuajiriwa ilikuwa ni Sambulumaa Band, wana `Zuke Muselebende”, iliyokuwa ikiongozwa na mfanyabiashara Emmanuel Mpangala na kuongozwa na Nguza Vicking.
Miaka minne baada ya kutoka kwa Nguza akaja akajiunga na Ndala Kasheba, hii ilikuwa ni 1994 wakaunda Zaita Musica, bendi iliyokuja kutamba na wimbo wa ‘Kesi ya Kanga’ na hapa ndipo mtindo wa kitambaa cheupe ulipozaliwa.
Huu mtindo ndiyo mpaka leo unaoipa bendi ya La Capital wateja wengi wanaopenda muziki wa kistaarabu na mwenyewe anatafsiri kitendo cha kuweka kitambaa cheupe kama ishara ya upendo na amani.
Kiki, ambaye kwa sasa ni raia wa Tanzania(tangu mwaka 1997), anaamini kwamba Wazee Sugu Capital ambayo iliundwa mwaka 2003, ndiyo bendi bora kwa muziki wa dansi kwa sasa, na huenda ikawa ndiyo bendi yake ya kuzeekea, huku akisisitiza kwamba hatakuja kuisahau The Norvella Jazz ambayo ndiyo alianza nayo muziki huko nyumbani kwao Katanga (sasa kunaitwa Shaba) mwaka 1962.
No comments:
Post a Comment