Social Icons

Sunday, 14 September 2014

HADITHI: Niloa jini nikamsaliti -18


“Subira mpenzi wangu ni mimi Thabit mpenzi wako.”
“Siwezi kuamini wewe si Thabit,” Subira alikataa katakata.
“Nifanye nini ili ujue mimi ni mpenzi wako?”
“Hata ufanyeje siwezi kukukubalia,” Subira alibisha kutokana na hali aliyomuachanayo jioni ile.
SASA ENDELEA...

Mpaka kukimbilia kwa mzee Mukti ambaye aliangalia na kumweleza mpenzi wake atapona lakini ugonjwa lazima ungemsumbua na kuchukua muda mrefu.
“Fanya hivi nifuate hospitali, kwani upo wapi?” 
“Nipo Kigamboni.”

“Basi fanya haraka nimeruhusiwa muda si mrefu.”
“Nakuja, lakini wewe si Thabit,” bado alikataa. 
Subira pamoja na kuelekea hospitali alipokuwa amelazwa Thabit akiwa na dawa za kumchua na kunywa alizopewa na mzee Mukti.

Aliendesha gari hadi hospitali na kulipaki pembeni na kukimbilia ndani ya wodi. Kutokana na papala alimpita mpenzi wake aliyekuwa amekaa mapokezi.

Aliingia mpaka wodini na kushtuka kukuta kitanda kitupu mawazo yake yalimpelekea labda Thabit amefariki. Alijikuta akiangua kilio cha sauti na kufanya muuguzi kumfuata na kumuuliza analia nini.
“Yupo wapi mpenzi wangu?”
“Umemuacha mapokezi.”

Bila kusema neno aligeuka hadi mapokezi na kumkuta Thabit amejaa tele akiwa mzima wa afya kwa mshtuko alianguka chini na kupoteza fahamu asiamini alichokiona na kuona kama yupo ndotoni. 
Alipewa huduma ya haraka iliyomrudisha katika hali yake ya kawaida.
Baada ya kupata nafuu alimuangalia mpenzi wake asiamini kilichotokea bado alijiona kama yupo ndotoni.

“Ni wewe mpenzi wangu?”
“Ni mimi.”
“Hapana,” Subira alisema huku akimpapasa mpenzi wake ili kuhakikisha kama ni yeye kweli au anaota mtu aliyemuacha muda mfupi akiwa hajitambui viungo vyote havifanyi.
“Ni mimi.”

Subira alimkumbatia Thabit kwa furaha baada ya kuamini kweli aliyembele yake ni mpenzi wake akiwa mzima wa afya njema.
“Yaani siamini.”
“Basi amini, hata vile mali zilizopotea zimerudi.”
“Unasema!”

“Mali zilizoungua dukani na kwenye makontena zimerudi kama kawaida.”
“Jamani huu si utani au unanitania mpenzi wangu?”
“Sikutanii kama umenikuta mzima kabisa basi na kila kitu changu kipo salama.”
“Haya ni maajabu ya dunia.”

“Walaa si maajabu lile ni jasho langu la halali haliwezi kutoweka kiajabu.”
  Kabla ya kuondoka Subira alimpigia simu mzee Mukti kumjulisha juu ya tukio lile la ajabu ya karne. Taarifa ile ilimshtua sana na kuuliza:
“Ha! Unasema kweli?”

“Kweli kabisa ninavyokuambia nipo naye sasa hivi mzima wa afya kabisa.”
“Subira unanigeuza mtani wako wa kunitania?”
“Walaa kweli kabisa.”

“Mmh! Unajua siamini.”
“Kama huamini ngoja nikupe uzungumze naye.”
“Hebu nipe.”

Subira alimpa simu Thabit aliyezungumza:
“Haloo mzee.”
“Wewe ni Thabit?”
“Ndiyo.”

“Mpenzi wa Subira?”
“Ndiyo.”
“Mmh! Kimetokea nini?”

“Kwa kweli mpaka sasa sijui, namshukuru Mungu kama nilikuwa mgonjwa lakini sasa  mzima wa afya.” 
“Sawa, umeishafika nyumbani?”
“Ndiyo nataka kutoka hospitali.”
“Basi kapumzike.”

“Sawa mzee naomba basi utengeneze mambo naona wabaya wangu bado wananiandama.”
“Hakuna tatizo.”
Kabla ya kukata simu Subira alichukua simu na kumwambia kitu mzee Mukti kilichozidi kumshangaza.
“Babu yaani haya ni maajabu ya mwaka hata vitu vyote vilivyoungua dukani na kwenye makontena vimerudi.”

“Wewee!” mzee Mukti aliona sasa ule ni utani.
“Hata mimi nilikuwa kama wewe, kwangu bado naona kama ndoto lakini huo ndiyo ukweli wenyewe.”
“Hebu subiri niangalie kipi kimetokea.”

“Sawa, sisi tunakwenda nyumbani, vipi zile dawa nimpe?”
“Usimpe mpaka nitakapokupa maelekezo.”
“Sawa.”

Baada ya Subira kukata simu na kumshika mkono mpenzi wake ili waondoke, mzee Mukti alichanganyikiwa na kuingia kwenye rada zake kuangalia nini kimetokea tofauti na kitu alichokiona juu ya matukio yale. Kwanza kwenye rada yake kuonesha moto mkubwa.

Hakukubali alitumia uwezo wake wote kutaka kujua nini kimetokea tofauti na kitu alichokiona. Baada ya moto kutulia aliona jinsi jini Nargis alivyo mponya Thabit na kurudisha mali zote zilizoteketezwa kijini. Matukio yale yalimshangaza na kujiuliza kufanya vile alikuwa na maana gani.

Lakini aliamini mali yote iliyorudi haitateketea tena  kwa vile sehemu ile alikuwa imeizindika. Ila kwenye makontena kulionesha pepesi  hivyo palitakiwa kudhibitiwa usiku ule kabla upande wa pili haujarudi tena.
Aliwapigia simu na kuwajulisha baada ya mali kurudi walitakiwa kuzizindika ili zisiharibike tena. Walikubaliana na mzee Mukti alikwenda kuzizindika na kazi ilifanyika usiku wa manane.

Siku ya pili ilikuwa sherehe kwa wafanyakazi wote waliokata tamaa baada ya kuchanganyikiwa kutokana na mali kuteketea kila kukicha.  Hali ilirudi kama kawaida na biashara iliendelea kwa Thabit kufungua maduka mengine makubwa kila kona ya jiji na kuanza kujipanga kufungua matawi mikoani.

Subira naye alitumia nafasi hiyo kuomba ndoa, Thabit hakuwa na pingamizi  aliwatuma washenga walikwenda nyumbani kwao na Subira ndoa ilipangwa mara moja na siku ilipofika Subira aliolewa na Thabit kuwa mke wake halali wa ndoa.

Ilikuwa furaha isiyo na kifani baada ya Subira kutimiza ndoto yake ya kuwa mke wa Thabit.

Inaendelea 

Chanzo globalpublishers 


No comments:

 
 
Blogger Templates