Wanamgambo wa Dola la Kiislamu wenye itikadi kali wametoa mkanda wa video ukionesha mfanyakazi wa shirika la kutoa misaada raia wa Uingereza David Haines akikatwa shingo.
Haines alitekwa nyara nchini Syria mwaka jana, na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ameshutumu kuuwawa kwake jana Jumamosi, na kusema kuwa ni "kitendo cha uovu mkubwa."
Cameron amethibitisha kifo cha haines katika taarifa baada ya wizara ya mambo ya kigeni ya Uingereza kusema hapo kabla kuwa "inafanya kazi haraka kuthibitisha mkanda huo wa video." Haines ni raia wa tatu wa mataifa ya magharibi kuchinjwa katika wiki za hivi karibuni na kundi la Dola la Kiislamu, ambalo limekamata maeneo makubwa ya ardhi ya Syria na Iraq.
"Haya ni mauaji ya kuchukiza na yasiyoweza kuelezeka, ya mtu asiyekuwa na hatia na mfanyakazi wa kutoa misaada. Ni kitendo cha uovu mkubwa," amesema Cameron , na kuongeza kuwa "moyo wangu uko pamoja na familia ya David Haines ambaye ameonesha ujasiri mkubwa na uadilifu wakati wote wa masaibu haya."
"Tutafanya kila kitu katika uwezo wetu kuwatafuta wauaji hawa na kuhakikisha kwamba wanakabiliana na sheria, hata kama itachukua muda mrefu kiasi gani," Cameron amesema.
Cameron kuongoza kikao maalum
Cameron amerejea katika makaazi yake ya mtaa wa Downing muda mfupi baada ya usiku wa manane na anatarajiwa kuongoza kikao cha kamati ya dharura ya kuchukua maamuzi katika serikali yake mapema leo Jumapili.
Mkanda huo wa video umetokeza siku moja baada ya familia ya Haines kutoa rai ya wazi siku ya Ijumaa ikiwataka watu waliomteka kuwasiliana nayo.
Wizara ya mambo ya kigeni imesema inatoa kwa familia ya Haines kila msaada unaostahili. Wameomba kuachwa katika faragha kwa muda.
Wanamgambo wa Dola la Kiislamu hivi karibuni waliwakata shingo waandishi habari wawili raia wa Marekani , James Foley na Steven Sotloff, na kuweka mkanda wa video katika mtandao wa internet baada ya Marekani kuanza mashambulizi ya anga na misaada ya kiutu mwezi Agosti kuyasaidia majeshi ya Iraq na ya Wakurdi kaskazini mwa Iraq.
Kundi la Dola la Kiislamu pia limeweka mtandaoni video inayoonesha kuuwawa kwa kukatwa shingo kwa wanajeshi wa Kikurdi na Lebanon na kuuwawa kwa kupigwa risasi wanajeshi kadhaa wa Syria waliokamatwa na kundi hilo.
Mwishoni mwa video hiyo ikionesha kukatwa shingo kwa Sotloff, kundi la Dola la Kiislamu limetishia kumuua Haines na kumuonesha kidogo katika mkanda huo.
Ni mauaji ya kinyama
Rais Barack Obama amesema katika taarifa kuwa anashutumu vikali "mauaji hayo ya kinyama " ya Haines yaliyofanywa na kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu.
''Marekani inasimama bega kwa bega leo hii na rafiki wetu wa karibu na mshirika katika majonzi''. Amesema Obama, na kuongeza kuwa Marekani itashirikiana na Uingereza pamoja na muungano mkubwa wa mataifa kutoka katika eneo hilo na duniani kwa jumla kuwafikisha watu waliofanya kitendo hiki mbele ya sheria, ''na kubomoa na kuharibu kabisa kitisho hiki kwa watu katika nchi zetu , eneo la mashariki ya kati na dunia kwa jumla," Obama amesema.
Chanzo Dw.de
No comments:
Post a Comment