Kama alivyoingia ndivyo alivyotoka katika umbile la kibinadamu na kuwaaga wagonjwa wengine waliokuwa kwenye foleni. Baada ya kutoka Mukti alishusha pumzi ndefu asiamini kilichotokea.
ENDELEA...
Alivuta begi kubwa na kuliangalia vizuri na kukuta limejaa fedha mchanganyiko za mataifa makubwa na za Tanzania.
Alifungua begi la pili lililokuwa limejaa madini mchanganyiko na kumfanya mzee Mukti kupiga kelele za kupagawa na kuanza kujimwagia kitu kilichowashtua wasaidizi wake walioingia ndani na kukuta fedha na madini yametawanyika.
“Nini mzee?” wasaidizi walimshangaa.
“Sasa hivi mimi ni tajiri wa maisha.”
“Hizi fedha na madini umetoa wapi?”
“Ni Mungu tu.”
Ghafla alitokea Nargis mbele yake na kumweleza afanye kazi kwanza, aliwaomba watoke na kuyaweka pembeni yale mabegi yenye fedha kisha aliendelea na kazi yake kama kawaida ya kuwahudumia wateja. Alijikuta akili yake ikimuwaza Subira na kutaka afike mapema.
Alijikuta akimshangaa jini Nargis kuonesha huruma ya ajabu, lakini ingekuwa hiyari yake na utajiri kama ule angemfanya kitu kibaya kama si kumpa sumu ili kuwaacha Nargis na mumewe wafurahie ndoa yao. Lakini hakutaka kumfanyia baya lolote zaidi ya kurudi katika ndoa yake.
***
Kibaridi kikali cha alfajiri kilimwamsha Subira ambaye alipojigeuza alishangaa kujiona amebanwa na kitu. Alipofumbua macho alikutana na mwanga mkubwa ukitoka juu kuonesha yumo shimoni. Alipojitahidi kunyanyuka alishindwa kutokana na sehemu aliyowekwa ilikuwa ndogo na kumfanya asiweze kujitikisa.
Ili apate msaada ilibidi apige kelele kuomba msaada kwa wapita njia, baada ya muda watu walikusanyika juu ya kaburi. Walishangaa kumwona mtu amelala kaburini akiwa amelazwa kwenye mwana ndani akiwa amefungwa sanda lakini pembeni ya kaburi hakukuwa na udogo.
Waliingia ndani ya kaburi na kumtoa nje, watu wote walimshangaa na kutaka kujua kipi kilimsibu. Subira alishindwa kusema alikuwa akilia tu, kurudi nyumbani aliogopa aliomba msaada wa nguo. Baada ya kupatiwa pande mbili za kanga, aliomba msaada wa gari mpaka kwa rafiki yake ambaye alimshangaa kumwona yupo vile.
Alimuomba kwanza ampe nguo zake kisha amuazime fedha ili aende Kigamboni kwa mzee Mukti kwani aliamini bwawa liliishaingia ruba lilikuwa haliogeki tena. Shoga yake alimpatia nguo baada ya kuoga. Kutokana na kuchanganyikiwa hata kula hakutaka.
Alikodi gari hadi Kigamboni kwa mzee Mukti, kama kawaida alikuwa hakai foleni alikuwa akipitiliza na kwenda kukaa kwenye chumba maalumu alichotengewa na mganga kisha aliwatuma vijana wa mzee Mukti wakamwite kwani alionekana amechanganyikiwa.
Mzee Mukti alikwenda kwenye chumba maalumu alichotenga kwa ajili ya kukutana na Subira kutokana umuhimu wake katika kuyabadili maisha yake. Lakini siku ile alimuona kama adui, bila Nargis angemfanya kitu kibaya baada ya akili yake kufikiria utajiri aliopewa.
“Karibu,” mzee Mukti alificha chuki yake.
“Asante.”
“Mbona upo hivyo?”mzee Mukti alimshangaa jinsi alivyovaa na mwonekano wake kuonesha ana matatizo makubwa hakuwa Subira aliyemzoea kujiremba lakini siku ile alikuwa vululuvululu.
“Babu mambo ni mabaya kuliko ulivyofikiria.”
“Tatizo nini?”
“Huwezi kuamini kilichonitokea, mimi wa kulala kaburini nimevishwa sanda?” Subira alisema huku akilia.
“Sijakuelewa una maanisha nini?”
Subira alimweleza kilichotokea usiku wakati akiwa kitandani alipotokewa na jini Nargis ambaye alimvisha sanda kama maiti na kupelekwa kulala ndani ya kaburi tena kwenye mwana ndani na jinsi alivyookolewa na watu na kutolewa ndani ya kaburi.
“Duh!” mzee Mukti alishtuka baada kusikia uwezo mkubwa wa Jini Nargis kwa kuvunja nguvu zake zote alizoweka na kufanya anavyotaka.Kwa mara ya kwanza aliamini uchawi unazidiana na kushangaa kama Nargis alikuwa na uwezo wa kuingia kila kona na kufanya aliyoyafanya kulikuwa na umuhimu gani wa kumpa utajiri ili amrudishie mumewe mkononi mwake. Wasiwasi wake alijua lazima alikuwa akimtega kama akikaidi basi naye amtie adabu.
“Mzee wangu naumbuka kwani tumekosea wapi mpaka imekuwa hivi?”
“Mmh! Hebu subiri.”Mzee Mukti alitoka na kumwacha Subira akiwa ameshika tama asijue hatima yake, mzee Mukti aliamini ile ndiyo ilikuwa nafasi yake ya kulirudisha penzi la Nargis kwa mumewe. Alitumia nafasi ile kufungua vifungo vyote alivyomfunga Thabit, baada ya kuandaa dawa ya kuvunja kila alichokifanya ili Thabit ampende Subira.
Baada ya kuandaa dawa alirudi chumbani na kumpa Subira, alipofika alimpa dawa za kuoga, kuweka katika chakula, kinywaji na kuweka katika maji ya kunyunyizia kuzunguka nyumba nzima.
“Hebu kafanye hivi.”
“Mzee wangu mbona kama dawa ulizokuwa ukinipa zamani, zitaweza kweli?”
“Mama, mimi ndiye mganga, hebu kafanye niliyokuelekeza.”
“Mmh! Sawa, naweza kurudi nyumbani kwangu?” Subira aliisha ingia woga.
“Nenda tu wala usiogope.”
“Yaani nakwenda lakini nimeingiwa woga kweli.”
“Ukiingia vitani usiogope kupigwa lazima upambane na si kuogopa.”
“Kwa nini tusiende wote, yaani naogopa.”“Hakuna kitu we nenda tu.”
“Mmh! Sawa,” Subira alisema na kunyanyuka kuelekea nje ili aelekee kwake ambako alipaona panawaka moto.
Inaendelea
Chanzo Globalpublishers
No comments:
Post a Comment