“Mmh! Sawa, naweza kurudi nyumbani kwangu?” Subira aliisha ingia woga.
“Nenda tu wala usiogope.”
“Yaani nakwenda lakini nimeingiwa woga kweli.”
“Ukiingia vitani usiogope kupigwa lazima upambane na si kuogopa.”
“Kwa nini tusiende wote, yaani naogopa.”
“Hakuna kitu we nenda tu.”
“Mmh! Sawa,” Subira alisema na kunyanyuka kuelekea nje ili aelekee kwake ambako alipaona panawaka moto.
SASA ENDELEA...
Subira alirudi nyumbani akiwa hajiamini kwani wasiwasi wake wote ulikuwa kwa Jini Nargis mwanamke halali wa Thabit aliyempindua. Alikodi gari hadi nyumbani kwake, bahati nzuri alimkuta mumewe Thabit bado yupo nyumbani.
Alimshangaa mkewe mavazi aliyovaa na asubuhi ile alikuwa akitoka wapi.
“Mke wangu unatoka wapi asubuhi yote hii na ulikuwa wapi?”
“Mume wangu nitakueleza naomba uniache nipumzike kwanza mengine tutazungumza baadaye.”
“Sawa, vipi kazini huendi?”
“Naenda.”
“Basi fanya haraka tuondoke mengine tutazungumza jioni tukirudi.”
“Sawa mume wangu, naomba nikaoge ili nikuandalie kifungua kinywa.”
“Sawa mke wangu fanya haraka.”
Subira alishangaa Thabit kuendelea kumwita mkewe pamoja na kulala na mkewe jini, alikwenda kuoga maji aliyochanganya dawa aliyopewa na mzee Mukti. Baada kuoga alimwita na Thabit kuoga maji ya dawa. Mumewe aliingia bafuni na kuoga bila kujua maji aliyokuwa akioga yalikuwa na dawa.
Baada ya kuoga alimwandalia kifungua kinywa kama kawaida na kuweka dawa kwenye chakula. Baada ya kuweka dawa alimpelekea chakula ambacho walikula pamoja. Kila alivyokuwa akila na kunywa alihisi kuona kama maluweluwe machoni mwake.
“Subira,” alimwita baada ya kushindwa kujielewa.
“Nini mume wangu?”“Au basi,” alijibu baada ya hali kutulia.
“Niambie mume wangu kuna nini?”
“Walaa, tuwahi kazini.”
“Sawa.”
Kabla ya kuondoka Subira alimuacha ndani Thabit na kuzunguka nyumba kunyunyuzia dawa aliyopewa na mganga. Alifanya kwa haraka kisha alirudi ndani na kumweleza mumewe.
“Mume wangu twende zetu,” Subira alisema huku akimshika mkono wawahi kazini.
Walitoka pamoja na kuingia ndani ya gari kuwahi kazini, walipofika waliendelea na kazi kama kawaida huku Thabit akiwa hajielewi baada ya kuingiwa na kumbukumbu ya ghafla ya Nargis.
“Mmh! Nargis...Nargis...ni...ni...nani? Hapana si...si mke wangu..Mungu wangu na...na Subira ni nani yangu? Hebu,” alinyanyua simu na kubofya namba kisha alizungumza.
“Subira.”
“Abee.”
“Njoo mara moja.”
“Nakuja.”
Baada ya muda Subira aliingia ofisini kwa Thabit na kusimama mbele kusikiliza wito.
“Subira.”
“Abee.”
“Eti wewe hapa ofisini ni nani?”
“Mume wangu, swali gani hilo?”
“Umeniitaje?”
“Mume wangu.”
“Mimi mumeo! Tokea lini?”
“Thabit mume wangu upo sawa?”
“Nipo sawa.”
“Kwa nini unaniuliza swali hilo?”
“Kuna kitu kinanichanganya!”
“Kitu gani hicho?”
“Kwanza kuna pete niliyokuwa navaa ipo wapi?”
“Si...si...jui!”
“Halafu wewe ni msaidizi wangu, mke na mume imeanza lini?” Thabit alishangaa.
“Thabit mume wangu wewe ndiye uliyeniomba niwe mkeo na kufuata taratibu zote nashangaa leo kuniuliza hivyo?”
“Mimi nilikuoa wewe?”
“Ndiyo.”
“Mimi kweli! Thabit nilikuoa wewe na kuwa mke na mume?” Thabit alizidi kushangaa.
“Ndiyo na sasa hivi tuna miaka zaidi ya mitano.”
“Mmh! Siamini...siamini, mimi nina mke.”
“Ndiye mimi.”
“Hapana mke wangu anaitwa Nargis.”
“Mume wangu leo umekuwaje?” Subira alisema huku akitoka ofisini na kurudi na picha iliyokuwa kwenye flemu ya siku yao ya harusi wakiwa wamepozi na kuipeleka mbele ya Thabit.
“Mume wangu hii nini?” Subira alimuonesha Thabit picha yao ya harusi.
“Mmh! Hii harusi ulifunga na mimi?” Thabit alizidi kushangaa huku akitazama picha ya harusi yao kama ndiyo siku ya kwanza kuiona.
“Thabit mume wangu umekuwaje leo, asubuhi tumetoka pamoja na siku zote tupo pamoja kipi cha ajabu kwa leo?” Subira alizidi kushangaa mabadiliko ya ghafla ya mume wake.
“Bado naona mauzauza.”
“Mauzauza gani jamani?’
“Naomba uniache kwa muda nitakupigia baadaye.”
Subira alitoka ofisini kwa Thabit akiwa amechanganyikwa asijue nini kimetokea kwani kila dakika mambo yalizidi kumchanganya. Kwa haraka alichukuwa simu kumpigia mzee Mukti ili amweleze kilichotokea kwani ni muda mfupi toka atoke kwake na kupewa dawa ambayo badala ya kupunguza imeongeza matatizo.
Baada ya kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili:
“Haloo.”
“Haloo babu mbona mambo huku yanazidi kuwa magumu?”
“Kivipi?” Mzee Mukti alijifanya hajui kitu.
Subira alimweleza kilichotokea muda mfupi, mumewe kumshangaa na kumwona si mkewe. Mzee Mukti aliamini kazi aliyotumwa na Nargis ilikuwa imekwisha, alishusha pumzi na kusema:
“Mmh! Mambo mazito, inaonekana uwezo wangu umefikia mwisho.”
“Mungu wangu sasa itakuwaje?”
Itaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment