“Aliwasha udi na kuufusha kisha aliuweka chini ya kitambaa na kuvuta moshi wake baada ya muda alisikika akiguna peke yake na kusema kwa sauti nyembamba.
“Ewe mwanadamu una shida gani?”
“Nataka kuchukuliwa mume wangu.”
“Mbona unasema uongo?”
“Kweli huu ni mwaka wa tano nipo ndani ya ndoa yangu.”
SASA ENDELEA...
“Mbona kuna aliyeanza kuwa katika ndoa kabla yako?”
“Ni kweli, lakini naomba msaada wako.”
“Sasa nimsaidie nani mwenye mali au wewe?” Mganga aliuliza.
“Kivipi?” Subira hakumwelewa mganga.
“Mwenye mume ametoka hapa kuomba nisiiguse ndoa yake la sivyo atanifanya kitu kibaya.”
“Lakini wewe si mganga, hawezi kukutisha.”
“Ni kweli lakini si wakuharibu mambo ya watu.”
“Kwa hiyo huwezi kunisaidia.”
“Sina msaada zaidi ya wewe kumwachia mume wake, zaidi ya hapo utatafuta matatizo.”
“Kwa hiyo umeshindwa?” Subira aliuliza.
“Sijashindwa bali huo ndiyo ukweli, hebu angalia pembeni yako,” mganga alisema akiwa bado amejifunika kichwani.
“Nini?” Subira aliuliza huku akigeuka kuangalia pembeni yake lakini hakuona kitu.
“Mbona hakuna kitu, kuna nini?”
“Umeangalia vizuri?”
“Ndiyo.”
“Mbona mimi naona.”
Kauli ya mganga ilimfanya Subira ageuke tena kuangalia pembeni japokuwa mwanzo hakuona kitu chochote. Alipoangalia pembeni kwa mara ya pili hakuona kitu aligeuka ili amuulize mganga aliyemuona alimchezea akili baada ya kazi kumshinda. Macho yake yalishtuka baada ya kumuona mtu tofauti na mganga aliyekuwa amekaa mbele yake.
“He!” Alishtuka na kushika mkono kifuani kwa mshtuko.
“Unashtuka nini?” aliyekuwa mbele yake alimuuliza.
“Ha...ha...pana, ni...ni...sa...mehe.”
“Nikusamehe nini?”
“Ni...ni...me...me...ku...wa si...si...sikii,” Subira alipata kigugumizi cha ghafla.
“Sikiliza Subira nina imani kote ulipopita umeelezwa vizuri mimi ni nani na nina nguvu gani. Najua una tamaa ya mali, sikiliza sasa hivi sitaki shari na wanadamu ndiyo maana sitaki kukufanyia lolote baya. Sasa nieleze unataka nini ili uachane na mume wangu?” Subira aliulizwa kwa sauti ya upole tofauti na alivyotegemea.
“Si...si...taki chochote,” alijibu huku akitetemeka.
“Sema ukweli ulio ndani ya moyo unataka nikupe nini uachane na mume wangu, kwa ulichonifanyia nilikuwa ninawezo wa kuua au kukugeuza kiumbe cha ajabu. Lakini namshukuru Mungu amenipa subira na akili ya kuushinda mtihani huu. Mpaka unahangaika kwa waganga ulijua kabisa Thabit ni mume wangu na utajiri aliona ni mimi nimempa lakini ulijitoa akili .
“Ni kweli mimi ni jini na mwanaume niliyemchagua katika viumbe wanadamu ni Thabit baba wa watoto wangu Zumza na Zamzu. Hivi kweli hata akili ya kawaida tu, mfano wewe usafiri kwenda kwenu kujifungua nyuma aje mwanamke amchukue mumeo kwa nguvu za kichawi utajisikiaje?”
“Nitajisikia vibaya.”
“Utakubali kumwachia mumeo mpenzi?”
“Hapana.”
“Utafanyaje?”
“Nitapambana ili kumrudisha.”
“Nina imani jibu unalo, nafahamu ungekuwa wewe mtu huyo ungemuua hata kwa risasi, hali hii Thabit mume wangu wa halali umetaka kuniua vipi angekuwa mumeo mimi ni mwizi?”
“Ni...ni...sa...samehe dada yangu,” Subira alipiga magoti.
“Nataka kukueleza jambo moja dogo, ili ninalokupa ni onyo la mwisho. Naomba uachane kabisa na mume wangu. Nakuahidi ukiachana na mume wangu nitakupa zawadi nzuuuri.”
“Nimekuelewa dada yangu, sasa nikitoka hapa niende wapi?”
“Ooh! Swali zuri, kuna nyumba nimekutafutia utakaa hapo maisha yako yote masharti yake usiiuze tu. Kwa sasa utakwenda kumueleza ukweli Thabit kuwa wewe si mkewe kisha utaondoka, ukiondoka usirudi tena kazini, nimetafuta wafanyakazi wengine.”
“Sawa, hapo uliponitafutia nitapajuaje?”
“Ukitoka ofisini kwa Thabit kabla ya kuvuka mlango fumba macho ukitoka nje tu utajikuta kwako.”
“Sawa.”
Ghafla Subira alishangaa kujikuta mbele ya mganga ambaye muda huo alikuwa akinyanyua kitambaa alichojifunika kupiga ramli na kunyoosha mkono kuchukua maji. Alijinyoosha kuonyesha alichoka sana kisha alisema:
“Dada ondoka, kazi yako nzito, nilikuwa nakufa najiona angeendelea dakika tano ningekufa.”
“Angeendelea nani?”
“Binti hebu ondoka ukizidi kukaa hapa utanitafutia matatizo,” mganga alizungumza kwa wasiwasi huku akimeza funda la maji na kujishika shingoni kama mtu aliyekabwa.
“Kwani umepatwa na nini?” Subira alijikuta akimshangaa mganga.
“We’ mwana umetumwa? Hebu ondoka, kumbe ulipotoka ulimshindwa umekuja kunitafutia matatizo bure nikifa familia yangu utaitunza wewe?”
“Mmh! Makubwa.”
Subira alijikuta akichanganyikiwa asijue nini kimetokea, kwani muda mfupi alikuwa akizungumza na Nargis na ghafla tena akawa anazungumza na mganga, alijiuliza kile ni nini. Kwani baada ya kuzungumza na mganga ghafla akaja Nargis mara tena akarudi mganga.
Japokuwa alijiona kama yupo ndotoni lakini maneno ya Nargis yalikuwa na ukweli hivyo alitakiwa kuyafuata kwa usalama wa maisha yake. Hakutaka kuendelea kuwa pale kwani kila dakika mganga alipandisha hasira. Alinyanyuka na kutoka nje na kwenda kwenye gari lake na kurudi moja kwa moja ofisini kufanya aliyoelezwa na Nargis.
Aliendesha gari mpaka ofisini na kwenda moja kwa moja ofisini kwa Thabit na kuingia. Thabit alipomuona alishtuka na kumuuliza:
“Subira ulikuwa wapi?”
“Thabit naomba unisamehe.”
“Nimekusamehe, kaendelee na kazi.”
“Hapana kuna kitu nataka kuzungumza na wewe.”
Inaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment