Social Icons

Friday, 3 October 2014

HADITHI: Nilitafuna maiti ya mwanangu niwe tajiri -1


NILIRUDI nyumbani na kumkuta mke wangu akiwa vilevile. Alikuwa amejilaza kitandani akiugulia maumivu ya tumbo. Nikaketi kitandani na kumsogeza karibu yangu. Nikamlaza miguuni mwangu.
“Vipi Rita, unaendeleaje sasa?” nikamwuliza.
Hakujibu!

Alijipapasa tumbo huku akikunja uso. Nilijua alichomaanisha. Rita bado alikuwa anaumwa tumbo. Sikuwa na fedha za kumpeleka hospitalini. Nilibaki nimejiinamia kwa mawazo. Huku nimemshika Rita wangu, huku nimeshika tama!

Kwa tabu Rita alifumbua macho na kuniangalia. Aliniona nikiwa nimeshika tama kuonesha kwamba nilikuwa kwenye lindi la mawazo.
“Vipi na wewe huko umefanikiwa?” aliniuliza Rita kwa sauti chovu, kavu iliyotoka kwa kukatakata.
“Hakuna kitu Rita. Pamoja na kuwahi kote huko, sijafanikiwa kupata kibarua.”
“Kwa nini?”

“Watu walikuwa wengi sana, tena waliwahi zaidi yangu. Lakini ujenzi bado unaendelea, kesho nitajaribu tena naweza kubahatisha.”

Nilizungumza kwa uchungu mwingi. Nikijikaza kiume, machozi nikayabana ndani ya kuta za macho yangu, sikutaka yatoke Rita ayaone!
Mwanaume mzima!

Aibu!Haifai mwanaume kulia hovyo!
Ndivyo nilivyoamini, hata baba yangu aliniambia hivyo, kwamba wanaume wanatakiwa kujikaza. Mara chache sana nilipojisikia hasira ya kulia, nilifanya hivyo nikiwa na mbali na uso wa mke wangu.
Sikuwa tayari mke wangu ayaone machozi yangu, najua ningemuumiza zaidi, jambo ambalo sikuwa tayari kabisa kuliruhusu litokee.

“Lakini Galos, maisha haya ni mpaka lini? Tutakuwa wenye shida hivi hadi lini? Natamani hata kufa kuliko kuendelea na maisha haya ya dhiki na tabu kiasi hiki,” akasema Rita akimwaga machozi.
“Acha kumkufuru Mungu mke wangu. Mapambano bado yanaendelea. Tutafanikiwa siku moja,” nilimwambia maneno ya kumpa matumaini.

Taswira ya maisha yetu ilikuwa ngumu kufanikiwa. Tufanikiwe kwa lipi hasa? Nimezaliwa familia ya kimaskini, mbaya zaidi sina ujuzi wala elimu yoyote. Kikubwa ninachojua ni kubeba zege kwenye ujenzi wa majengo makubwa.

Ndiyo kazi iliyoniweka mjini na mke wangu Rita. Leo kazi inapatikana, kesho hakuna. Ni tabu mtindo mmoja. Pamoja na yote hayo, niliendelea kumwambia Rita avumilie, siku moja tutafanikiwa.
Kichwani nilijua ni ndoto!

Rita aliniangalia kwa jicho la kuhoji, kwa kiasi kikubwa alionekana wazi kutokubaliana na maneno yangu kabisa. Alijua ni kwa namna gani nilikuwa naongea maneno ya kumfariji tu.
Ni kweli!
Nilimfariji tu!

Nilimtazama Rita machoni, nikaachana naye. Nikaanza kukagua vizuri chumba chetu. Kilikuwa kimoja tu...tena hakina umeme! Tuna kitanda tu ndani, zaidi ni jiko la mafuta na ndoo za maji.
Nikahema kwa kasi, halafu nikaliendelea lile jiko pale chini, nikalifungua na kuangalia kama lilikuwa na mafuta ya taa! 
Hakuna kitu.

Sufuria zote zilikuwa kama nilivyoziacha. Jiko lilikuwa limenuna! Hapakuwa na matumaini ya kupika siku hiyo.

“Rita,” nikamuita mke wangu.
“Abee Galos.”
“Unajiasikiaje sasa?”

“Bado naumwa...hasa hapa,” akasema akinionesha tumboni, chini ya kitovu.
“Pole sana mke wangu,” nikamwambia halafu nikatulia kidogo.
Kisha nikamwuliza tena: “Hivi umefanikiwa kula?”
“Hapana!”

“Mungu wangu....” nikatamka kwa sauti kubwa.
Nilichanganyikiwa kwa sababu kubwa mbili; Rita wangu alikuwa anaumwa, lakini mbaya zaidi hata chakula alikuwa hajapata! Atapona vipi?
Bila dawa!

Bila chakula! “Kwa nini mimi?” nikasema kwa sauti kubwa bila kugundua kwamba nilizidi kumuumiza Rita.

Akaanza kulia.
Nilikuwa nimefanya kosa kubwa sana, haraka nikaanza kumbembeleza Rita asizidi kulia.
“Tafadhali nyamaza mke wangu, haya mambo yataisha tu. Mungu mkubwa,” nikamwambia.
“Yataisha lini? Kila siku matatizo tu, sidhani kama kuna mwisho hapa, zaidi ya mateso kila kukicha!” alisema kwa uchungu, akanizidishia maumivu moyoni mwangu.

Nilitulia kwa muda nikiendelea kutafakari, lakini sikupata jibu la maana. Tatizo ilikuwa ni pesa. Nikamkumbuka rafiki yangu ambaye huwa ananisaidia ninapokuwa na shida. Nikainuka pale kitandani.
“Narudi baada ya muda kidogo.”
“Unakwenda wapi?”

“Ngoja nikatafute maarifa.”
“Sawa.”

Nikatoka nyumbani na kwenda kwa rafiki yangu Patrick ambaye alikuwa fundi baiskeli. Niliamini yeye angeweza kunisaidia. Kwa bahati nzuri nilimkuta kijiweni kwake. Nikamvuta pembeni.
“Kaka nina matatizo sana, mke wangu anaumwa sana, sina pesa hata ya kula. Nimekwenda kibaruani wiki sasa nakosa nafasi.”

“Pole sana ndugu yangu.”
“Kilinichonileta kwako, naomba unisaidie shilingi elfu kumi ili niweze kumpeleka mke wangu hospitali, ndani ya wiki hii nitajitahidi nikurudishie!”
Patrick alitulia kwa muda akifikiria, hakujibu kitu. Aliondoka na kuniacha nimesimama palepale.
Niliduwaa nisijue la kufanya. Dakika ya kwanza iliondoka bila Patrick kurejea, hatimaye ya pili na sasa ilikatika robo saa nzima!

“Si yule pale,” nikasikia sauti ya kijana wa kiume akitamka, nikageuka kumwangalia...
“Ndiyo ni yeye,” mwingine akadakia.
Walikuwa wanaume wawili wa shoka, waliojazia sawasawa. Wakashuka garini kwa pamoja, wakaanza kunifuata huku nyuso zao zikionekana dhahiri walinifuata kwa shari!

Inaendelea

Chanzo globalpublishers 


No comments:

 
 
Blogger Templates