Hapo ndipo Rita analazimika kumbana Galos aeleze ukweli kama kulikuwa na jambo la siri alilokuwa akilifahamu kwani kilio chake kilimshangaza.
Je, nini kitaendelea?
“Naomba unieleze kama kuna chochote unachokifahamu juu ya haya yote yanayotutokea.” Rita alimuuliza Galos ambaye bado aliendelea kulia pamoja na kutulizwa kwa muda mrefu.
“Hakuna ninachokifahamu.”
“Sasa ni kwa nini unalia kiasi chote hicho?”
“Inaniuma tu, kila ninapotarajia kupata mtoto, anayeyuka!”
“Usijali mume wangu, tutapata tu mtoto mwingine, cha muhimu tuendelee kupendana.”
Saa mbili baadaye Rita alikuwa usingizini, lakini Galos alikuwa macho, akili yake yote ikimuwaza Mukulungu na mambo aliyokuwa akimfanyia.
Hakuwa tayari kusaini mkataka wa kichawi lakini pia alihitaji sana watoto maishani mwake akiwa na mke wake, kwa hali ilivyokuwa hofu ilikuwa imeanza kuugubika moyo wake kwamba Rita angeweza kumwacha, kama mimba zingeendelea kuharibika.
Hilo ndilo jambo kabisa hakutaka litokee, maisha yasingekuwa na maana bila mwanamke aliyempenda. Macho yakaendelea kubaki wazi, akimsubiri kwa hamu Mukulungu, atokee na waondoke wote kwenda kwenye ulimwengu mwingine ambako alitaka kukutana na kuongea na Mukulungu ili amwache aendelee na maisha yake.
Kulipokucha asubuhi alikuwa bado yu kitandani na mke wake, muujiza wa kwenda kwenye ulimwengu usioonekana haukutokea. Siku hiyo alishinda nyumbani na mke wake lakini siku iliyofuata aliingia mitaani kutafuta riziki, safari hii akiwa ameamua kufanya biashara ya kuuza maji kwa mkokoteni.
Alifanya kazi hiyo asubuhi mpaka jioni na kurejea nyumbani akiwa taaban, hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, ya umaskini wa hali ya juu, akiishi eneo la watu maskini, ambalo lilitoa harufu mbaya saa ishirini na nne sababu watu waliachilia maji machafu ya chooni kutiririka mitaroni.
Maisha yaliendelea kwa miezi sita, bila Rita kuugua, wala Galos kuchukuliwa tena na Mukulungu kwenda kwenye ulimwengu wa kichawi, lakini mwanzoni mwa mwezi wa saba, katikati ya usiku alishtukia anapigwa pigwa begani, alipofumbua macho alikutana moja kwa moja na uso wa Mukulungu ukiwa umejawa na tabasamu.
“Twende!”
Hakuwa na swali la kuuliza, akatupa jicho kumwangalia mkewe kando yake, usingizi aliokuwa nao ulikuwa mzito mno. Taratibu Galos alinyanyuka na kuanza kumfuata Mukulungu, kufumba na kufumbua wakajikuta wako chini ya mti mkubwa, mamia ya wachawi wakiwa wamekusanyika hapo, wakila nyama za binadamu zilizochomwa kwenye majiko makubwa.
“Nimekupa muda mrefu sana wa kufikiria, umefikia uamuzi gani?”
“Katika lipi?”
“La uchifu.”
“Wa wachawi?”
“Ndiyo.”
“Hilo nimekwishaligomea.”
“Bado hutaki pamoja na kukufanyia mambo yote tuliyoyafanya?”
“Ndiyo.”
“Wewe maskini jeuri, lakini sikiliza, mkeo ni mjamzito tena, ukifanya mchezo hata huyo mtoto hutamwona.”
“Ni mjamzito?”
“Wewe hujui lakini mimi najua.”
“Siyo kweli, angeshaniambia.”
“Subiri utaona.”
“Mukulungu tukamtese?” mtu mwingine aliyekuwa jirani aliuliza na Mukulungu aliuza akatikisa kichwa kuonyesha ishara ya kukataa, mwisho akamruhusu Galos aondoke zake, akanyanyuka na kuanza kutembea kuelekea gizani.
***
“Mbona ulikuwa unaongea peke yako?”
“Mimi?”
“Ndiyo.”
“Wapi?”
“Usingizini.”
“Nilikuwa naongea nini?”
“Mambo mengi yasiyoeleweka, mara ujauzito, mara hutaki kusaini mkataba, ni mkataba gani huo?”
“Ndoto tu darling.”
Asubuhi kulipopambazuka, Rita aliondoka kitandani anakimbia kwenda nje kutapika, aliporejea alimpa Galos taarifa kwamba alikuwa na miezi miwili tangu apate hedhi mara ya mwisho, hapakuwa na sababu tena ya kutilia mashaka ambacho Galos aliambiwa na Mukulungu, roho ikamuuma kufahamu ya kwamba hata mtoto ambaye mke wake alikuwa naye tumboni pia asingemwona.
“Sijui nitafanyaje?” aliwaza.
Maisha yaliendelea vizuri baada ya hapo, ujauzito ukaendelea kukua na Galos akiendelea kufanya kazi zake ngumu za kimaskini, kila alichokipata alikitumia kumtunza mke wake. Wala hakujiwekea akiba yoyote ya kulea mtoto, sababu alifahamu lazima angekufa, mimba ilipotimiza miezi sita, Rita alianza kumsisitizia Galos aanze kununua vitu mbalimbali vya mtoto lakini kijana huyo aliishia kububujikwa na machozi.
Mwezi wa saba, Galos akijua labda Mukulungu alishaahirisha adhabu yake, usingizi ulimpitia akajikuta katika ulimwengu wa wachawi ambako alianza kulazimishwa tena kusaini mkataba, akakataa. Vitisho vya kuua mtoto vikaendelea lakini bado hakubadilika, mwisho Mukulungu akabadilisha maelezo na kuanza kuzungumzia utajiri, hapo ndipo akaugusa moyo wa Galos.
“Utakufa maskini, mimi naweza kukufanya uwe tajiri kuliko unavyofikiria, unachotakiwa ni kutimiza masharti.”“Kuwa tajiri nataka, ambacho sitaki ni kuwa mchawi.”
“Basi kubali uwe tajiri kwanza!”
“Bila kuwa mchawi?”
“Inawezekana, suala la uchawi tutalifikiria baadaye.”
“Sharti ni lipi?”
“Kesho utarudi tutakuambia.”
***
Ghafla Galos akazinduka akiwa kando ya mke wake aliyekuwa akiteseka kwa maumivu makali ya tumbo na kudai damu zilikuwa zikimtoka, mara moja akaelewa adhabu ilikuwa imefika. Hakuna la kufanya zaidi ya kutoka ndani ya nyumba kwenda kutafuta usafiri, jirani yuleyule wa awali alimsaidia kumpeleka Rita mpaka hospitali ambako ilithibitika mtoto alikuwa amefia tumboni.
“Itabidi achomwe sindano za uchungu ili amsukume atoke, baada ya hapo atasafishwa.”
Hicho ndicho kilichofanyika, Rita akapewa dawa hizo na kusukuma, mtoto mkubwa kabisa akatoka, baada ya hapo akasafishwa.
Hali yake ilipotengemaa walikabidhiwa kichanga chao na kwenda kukizika makaburini, jirani kabisa na hospitali, wakarejea nyumbani wakiwa na huzuni, wote wakilia kwa uchungu, lakini Galos alilia zaidi.
Usiku huohuo alipitiwa na usingizi mzito na kujikuta tena kwenye ulimwengu wa wachawi, Mukulungu alikuwa na maiti ya mtoto mchanga mikononi mwake,
akamwambia Galos kwamba maiti ile ndiyo iliyotoka tumboni mwa mke wake, ilifukuliwa makaburini mara tu baada ya kuzikwa.
“Hili ndilo sharti unalotakiwa kulitimiza, ule maiti hii ya mtoto wako, ndipo utakuwa tajiri! Uko tayari?”
Itaendelea
No comments:
Post a Comment