Social Icons

Thursday, 9 October 2014

HADITHI: Nilitafuna maiti ya mwanangu niwe tajiri -10


Safari kwenda hospitali ikaanza, kichwa changu kikiwa kimejawa na mawazo mengi ya vitisho vya mzee Mukulungu na  serikali yake ya kichawi, sikujua jinsi ya kujinasua kutoka kwenye mtego huo lakini jambo nililoelewa ni kwamba sikuwa tayari kusaini mkataba wa kichawi na kuanza kuua watu. SASA ENDELEA...

Dakika ishirini baadaye gari likiendeshwa kwa kasi, lilikata kona kuingia hospitali tukanyoosha moja kwa moja hadi mapokezi ambako muuguzi alikuwepo, akatupeleka moja kwa moja chumba cha daktari mke wangu akiwa amekalishwa kwenye kiti cha magurudumu.
“Vipi?” Daktari aliuliza, alikuwa kijana mdogo tu, kwa miaka ya nyuma usingeweza kukubali  daktari wa umri ule akuhudumie, alilingana kabisa na watoto wa kidato cha sita.
“Mke wangu anaumwa.”
“Nini?”

“Tumbo.”
“Mjamzito?”
“Alikuwa mjamzito.”
“Unamaanisha nini kaka yangu?”
“Damu nyingi zinamtoka.”

“Ooh! Dada unaweza kupanda hapo kitandani?”
“Ndiyo.” Rita aliitikia na kwa msaada wa mimi na jirani yangu, tulimbeba na kumpandisha juu ya kitanda, daktari akachukua pazia  lililounganishwa na vyuma na kukizungushia kitanda,  kisha akatutaka mimi na jirani yangu tusimame nje ya pazia ili ampime mgonjwa, ampime bila mimi kuwepo? Nilijiuliza kichwani mwangu lakini sikuwa na jinsi, ikabidi nitii.

Dakika kumi baadaye daktari alitokeza akivua mipira mikononi mwake, jambo lililoashiria kuwa alikuwa amempima mke wangu sehemu za siri, sikukipenda kabisa kitendo hicho lakini sikuwa na namna. Akaniangalia usoni, nami nikagundua masikitiko aliyokuwa nayo.
“Pole sana ndugu yangu.”
“Kwa nini daktari?”

“Mimba imeharibika.”
“Sijui kama tutakuja kupata mtoto?” niliuliza swali hilo nikimsikia Rita akigugumia kwa maumivu nyuma ya pazia.

Nilikuwa na siri nzito ndani ya moyo wangu ambayo nisingeweza kumweleza mtu,  wachawi walikuwa wamedhamiria kuhakikisha sipati mtoto maisha yangu yote, mwisho wangeniua mimi mwenyewe kama adhabu sababu tu  baba yangu alikiuka masharti ya uanachama wake wa uchawi. Jambo hili liliniumiza moyo sana, nikajiuliza jinsi ya kujinasua lakini sikupata jibu, nikainamisha kichwa chini huku machozi yakinibubujika.

“Kwani ni mimba ya ngapi kuharibika?”
“Ya tatu.”
“Mna mtoto?”
“Hatuna.”
“Hii inaitwa kwa kitaalam Habitual Abortion, inabidi ufanyike uchunguzi wa kina kufahamu ni kwanini mimba zinaharibika.”

“Hata ukifanya uchunguzi daktari sijui kama…”
“Hapana usiseme hivyo, inawezekana kabisa tukaligundua tatizo.”
“Siyo rahisi.”

“Kwanini unasema hivyo? Kuna jambo unalijua?”
“Hapana daktari!”
“Acha tumpeleke chumba cha upasuaji tukamfanyie Evacuation, kesho utafanyika uchunguzi wa kina kufahamu ni kwa nini mimba zinatoka mfululizo.”
“Hilo neno la Kiingereza ulilolisema sielewi maana yake.”
“Evacuation?”
“Ndiyo.”

“Ni kitendo cha kusafisha mfuko wa uzazi baada ya mimba kuharibika.”
“Ahsante daktari.”
“Mna bima?”
“Hapana.”
“Kwa hiyo mtalipia taslimu?”
“Sina fedha.”
“Mh!”

“Ni kiasi gani daktari?” jirani aliuliza.
“Inaweza kufika shilingi elfu arobaini.”
“Nitazilipa.”
“Ahsante jirani.”
Tukaelekea dirishani kufanya malipo, baada ya hapo Rita akachukuliwa kwenye chumba cha upasuaji ambako mfuko wake wa uzazi ulisafishwa na kutolewa saa nzima baadaye, akiwa katika hali ya usingizi na kulazwa kwenye wodi ya wazazi.

Jirani yangu  baada ya hatua hiyo aliondoka na kuniacha nje ya wodi, nikabaki hapo mpaka asubuhi ya siku iliyofuata kichwa changu kikiwa kimejawa na mawazo mengi juu ya mambo yote niliyoyaona usingizini na vitisho nilivyokuwa nimepewa na mzee Mukulungu, ambaye tayari alishaitoa mimba ya mke wangu, hii ilionyesha kwamba alikuwa hatanii, kama nisingeusaini mkataba wao mwisho wa siku nisingekuwa na mtoto na wangeniua.

“Siwezi kusaini, siwezi kuwa mchawi, bora nife!” niliendelea kukataa akilini mwangu.
Mchana wa siku hiyo yote vipimo vingi vilifanyika ili kufahamu ni kwa sababu gani mimba za mke wangu zilikuwa zikitoka ilichukuliwa damu kwenda kupima homoni za uzazi na kitu kingine kiitwacho Rhesus Factor,  ambacho niliambiwa huhusika sana na mimba kuharibika pale ambapo mtoto anakuwa na Positive wakati mama yake ana Negative, mama mjamzito hutengeneza askari mwilini mwake waitwao Anti D ambao huenda kumshambulia mtoto  kwenye mfuko wa uzazi, kusababisha kifo chake na hatimaye mimba kuharibika.

Pia akapigwa picha iitwayo Ultra-Sound kwenye mfuko wake wa uzazi, kuona kama kulikuwa na kasoro yoyote  lakini vipimo vyote vilionyesha hapakuwa na tatizo la namna yoyote ile, madaktari wakashangaa, mwisho wakafikia uamuzi wa kuturuhusu mimi na mke wangu turejee nyumbani.
Nililia mno tukiwa nyumbani kiasi cha kumfanya Rita awe na wasiwasi, kilichokuwa kikinisumbua moyoni mwangu ni siri nzito niliyokuwa nimeibeba ambayo nisingeweza kabisa kumshirikisha mke wangu. Niliumia kuona watoto ambao wangeniletea furaha maishani wakifa kikatili kwa sababu tu sikuwa tayari kuwa mchawi.

“Darling mbona unalia sana?”
“Basi tu.”
“Au kuna jambo unajua?”
“Mh! Mh!Mh!” niliishia kuguna tu.
“Tafadhali nieleze.”

inaendelea

No comments:

 
 
Blogger Templates