“Sasa nataka kuuchukuwa utajiri wangu, urejee kwenye maisha yako ya zamani.”
“Kwa nini?”
“Imetosha tu,”
“Tafadhali usifanye hivyo, watu watanicheka, heshima yangu itapotea.”
“Nitauacha tu kama utatimiza sharti langu.”
“Lipi tena?”
“Nataka damu ya mkeo!”
“Mke wangu?”
“Ndiyo, umtoe kafara, wazee wanywe damu, nenda kafikirie, kesho utakuja kunipa jibu.”
Galos akainamisha kichwa na kuanza kulia, alikuwa njia panda, ghafla akazinduka usingizini na kumkuta mkewe akimtingisha na kumbembeleza aache kulia.
“Mbona umelia sana? Ndoto gani hiyo?”
ENDELEA...
Galos alibaki kimya, machozi yakiendelea kumbubujika. Moyo wake ulitamani kufunguka na kumweleza mke wake ukweli wa yaliyokuwa yakimtokea na hasa juu ya siri ya utajiri wao usio wa kawaida. Alishindwa kufanya hivyo pamoja na Rita kumshawishi aeleze kilichomfanya alie akiwa usingizini.
“Mh! Galos, hebu nieleze ni nini kilikuwa kinakuliza usingizini tena ukisema maneno sitaki kumuua mke wangu?” Rita aliuliza akimwangalia Galos usoni.
Akainamisha kichwa chake chini, alipokinyanyua dakika kama kumi hivi baadaye, alifuta machozi, akamwangalia mke wake machoni, kisha kushusha pumzi ndefu.
“Rita!” Galos akaita.
“Bee!”
“Nikikuambia ukweli hutaniacha?”
“Siwezi.”
“Wanataka nikutoe kafara!”
“Mh!” Rita aliguna kwa mshangao, maneno hayo yalithibitisha kabisa alichokisikia wakati Galos akilia usingizini.
“Ni kweli.”
“Akina nani?”
“Baba yangu alikuwa mchawi kabla ya kifo chake…” Galos alijaribu kuzungumza lakini alishindwa, kwikwi ya kulia ikamkaba.Alichokifanya Rita pamoja na hofu iliyokuwa imemwingia, ni kuwa mvumilivu, akimbembeleza mume wake mpaka aseme ili ajue ni kitu gani kilikuwa kikimsumbua.
Alipotulia, Galos aliamua kufunguka na kuweka kila kitu bayana, kuanzia historia ya baba yake na uchawi, kulazimishwa arithi mikoba jambo ambalo alilikataa, adhabu ya kutopata mtoto aliyekuwa amepewa, hatimaye kula maiti ya mwanaye ili apate utajiri.
“Kwa hiyo mimba zinazotoka ni adhabu Galos?”
“Ndiyo mke wangu.”
“Na hiyo maiti uliyokula ni ipi?”
“Ya mimba ya mwisho.”
“Mungu wangu!” Rita alisema kwa mshtuko akiwa ameshikilia midomo yake.
“Ndiyo hivyo, leo wamenichukua tena nikiwa usingizini na kunipeleka kwenye ulimwengu wao ambako wameniambia wanataka nikutoe wewe kama kafara, ufe mke wangu, nimekataa kwa sababu ninakupenda, wameniachia mpaka kesho ndiyo nitarejea tena kuwapa jibu, kama nitakataa, watachukua kila kilicho chao na tutarejea tena kwenye umaskini.”
“Hawawezi, Mungu wetu ana nguvu kuliko wao na kila kitu tulichonacho ni halali yetu, hawana uwezo wa kutunyang’anya.”
“Ni wachawi mke wangu.”
“Mimi namwamini sana Mungu!”
“Sasa tutafanyaje?”
“Nitafunga, kumwomba Mungu apambane nao badala ya sisi, kisha tuone hiyo kesho!”
“Kweli Mungu atawaweza?”
“Galos! Huu ni wakati wa wewe kuamini kwamba Mungu wetu ana nguvu kuliko miungu mingine yote.”
“Naogopa!”
“Huhitaji kuogopa, acha tusubirie hiyo kesho tuone.”
Hawakulala tena mpaka asubuhi, Rita akisali, huku Galos akiwa kando yake. baadaye alimwongoza sala ya toba, kama aliyoongozwa yeye kanisani, Galos akawa amempokea Kristo kama Mwokozi wa maisha yake. saa kumi na mbili alfajiri, walianza rasmi mfungo wakimwomba Mungu awalinde na kuwaepusha na nguvu za giza.
Hawakutoka ndani siku hiyo mpaka jioni ya saa kumi na mbili, Rita akatoka chumbani kwenda jikoni kuandaa chakula, kilipokuwa tayari wote walijumuika mezani kula, Galos akionekana mwenye nguvu na matumaini, hofu yote ya mkono wa Mukulungu ikiwa imemtoka, alijisikia yu tayari kwa lolote kwani imani yake ilikuwa imepanda juu.
Baada ya chakula wote walijitupa kitandani, wakaendelea na mazungumzo mbalimbali kuhusu maisha, saa tano na dakika arobaini na tano, Galos akapitiwa na usingizi, muda huo huo akajikuta yuko kwenye ulimwengu wa kichawi. Rita akanyanyuka kitandani na kuanza kusali akimwomba Mungu ajibu kwa mapigo dhidi ya Mukulungu na jeshi lake.
Kwenye ulimwengu wa giza Galos hakuwa wa kawaida, alikuwa na nguvu mno, Mukulungu na jeshi lake walishindwa kumtuliza na kujikuta wakipokea vipigo na wengi kuchomwa moto, mwisho wakasalimu amri na kulala chini kifudifudi kutii amri ya Galos.
“Ufalme wako Mukulungu umefika mwisho, nguvu ya Mungu iko mahali hapa kusambaratisha kila kitu.”
“Ndiyo Galos.”“Ni wakati wa wewe na watu wako kutubu, mkamrejee Bwana, kwani mmetenda maovu kwa muda mrefu, mmeharibu maisha ya watu na kuwaua wengi, tubuni sasa mkapate kusamehewa.”
“Tuko tayari!” watu wote wakaitikia.
“Basi simameni kwa miguu yenu.”
Wote wakanyanyuka na kusimama wima, Galos akawaongoza sala ya toba, wakaapa wasingeshiriki uchawi tena maisha yao yote yaliyobaki, alipowaeleza juu ya ubatizo wote walitamani kubatizwa lakini Galos aligundua hakuwa na uwezo wa kufanya jambo hilo, akawataka wafike kanisani Word Alive, Sinza Mori ambako wangefundishwa Neno la Mungu na baadaye kubatizwa.
Galos akafumbua macho na kumkuta Rita bado akisali na kunena kwa lugha mpya, akakiacha kitanda na kumkumbatia mke wake, wakalia kwa furaha sababu ya ushindi waliokuwa wameupata.
Siku ya Jumapili Kanisa la Word Alive lilijaa idadi kubwa sana ya watu kuliko kawaida, wengi wakiwa ni watu maarufu lakini kumbe walikuwa wakishiriki mambo ya ushirikina, wote wakakabidhi maisha yao kwa Mungu, na Galos hakudiriki kufungua mdomo wake kutoboa siri ya yaliyotokea usiku, kila kitu alikiacha mikononi mwa Mungu.
Yeye na watu hao wasiopungua mia mbili na ishirini walibatizwa wiki mbili baadaye mafundisho yalipokamilika, ukawa mwanzo mpya wa maisha kwa Galos na mke wake Rita, ambaye mwaka mmoja baadaye wakiwa na utajiri wao alijifungua mtoto wa kike, wakampa jina Genesis.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment