Social Icons

Saturday, 11 October 2014

Waliokufa kwa Ebola ni zaidi ya watu 4,000

Idadi ya vifo vya Ebola imeripotiwa kupindukia 4,000, huku muunguzi wa Kihispania akipigania maisha yake Jumamosi, na serikali za mataifa zikijaribu kutuliza wasiwasi kuhusiana na ugonjwa huo hatari.

Ebola Patient Brasilien 10.10.2014

WHO imesema watu 4,033 wamefariki kutokana na Ebola kufikia Oktoba 8, katika ya jumla ya watu 8,399 waliosajiliwa kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo katika mataifa saba. Ongezeko kubwa la vifo limekuja wakati Umoja wa Mataifa ukisema ahadi zilizotolewa kupambana na mripuko huo ziko chini ya kiasi cha dola za Marekani bilioni moja zinazohitajika.

Mbali ya Afrika Magharibi ambako karibu vifo vyote vimetokea, hofu imeongezeka kuhusiana na mripuko huo mbaya zaidi wa Ebola. Serikali ya Cananda ilishauri raia wake siku ya Ijumaa kuondoka katika mataifa ya Afrika Magharibi yalioathiriwa zaidi na ugonjwa huo, huku ikichukuwa hatua katika mipaka ya ke kuwachunguza wasafiri walio na uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa huo.

Marekani na Uingereza pia zimeimarisha uchunguzi katika viwanja vikubwa vya ndege. Kituo cha udhibiti na uzuwiaji magonjwa cha Marekani CDC, kimetabiri kuwa idadi ya watu walioambukizwa Ebola inaweza kufikia milioni 1.4 kufikia mwezi Januari ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa kudhibiti mripuko huo.

Mchoro wa visa vya Ebola Afrika Magharibi.

Mchoro wa visa vya Ebola Afrika Magharibi.

Kuanzia Australia hadi Zimbabwe, na Brazil hadi Uhispania, watu wanaoonyesha dalili za homa, au waliokuwa na mawasiliano na waathirika wa Ebola hivi karibuni, waliowekwa katika vituo vilivyotengwa au kuamriwa kubakia majumbani mwao. Serikali zimeonya kuwa vitisho vinaweza kuibua hofu baada ya mwanaume kuondolewa katika ndege ya Marekani na timu ya kukabiliana na ugonjwa huo, baada ya kupiga chafya na kuripotiwa kusema kuwa: "Nina Ebola. Wote mmeukwaa."

Wasiwasi mkubwa umeendelea nchini Uhispania juu ya namna kirusi hicho kiliweza kusambaa katika hospitali kuu ya taifa kutengea wagonjwa. Wafanyakazi wa afya waliliambia shirika la habari la AFP kuwa ghorofa la karantini la hospitali ya Carlos III mjini Madrid, ambako muuguzi mwenye umri wa miaka 44 Teresa Romero aliathirika, ilifungwa mwaka uliyopita kutokana na kupunguza matumizi, na ilifunguliwa tu kwa ajili ya wamishonari wawili waliorudishwa kutoka Afrika wakiwa na ugonjwa huo mwezi Agosti.

Waziri mkuu Mariano Rajoy aliitembelea hospitali ambako Romero aliepata ugonjwa huo wakati akiwahudumia wamishonari, alisemekana kuwa katika "hali mbaya lakini isiyobadilika" siku ya Ijumaa. Madaktari waliwapeleka wagonjwa wengine watatu kwa ajili ya uangalizi siku ya Ijumaa, na kufanya idadi ya watu walioko katika uchunguzi, akiwemo Romero, mume wake na wafanyakazi wengine wa afya.

Mshukiwa wa Ebola akiweka karantini nchini Marcedonia.

Mshukiwa wa Ebola akiweka karantini nchini Marcedonia.

Wafanyakazi wa Ebola wamezidiwa

Katika ishara ya msongo hospitalini hapo, wafanyakazi hawakujitokeza siku ya Ijumaa. Muunguzi mmoja alisema ni wafanyakazi wachache wanaoripoti kazini. "Tumechoka sana, tunafanyakazi chini ya shinikizo kubwa."

Umoja wa Mataifa na viongozi w amataifa yalioathirika zaidi na Ebola - Guinea, Liberia na Sierra Leon waliomba msaada zaidi kukabiliana na mripuko huo barani Afrika. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson alisema ni robo tu ya kiasi cha dola bilioni moja kilichoombwa kukabiliana na ugonjwa huo zilizoahidiwa. Aliwatolea mwito madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wa afya kujitokeza.

Matamshi yake yalirejea wito uliyotolewa siku ya Alhamisi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, ambaye rasilimali kuunga mkono mapambano laazima ziongezwe mara 20. "Visa vinaongezeka kwa kiwango kikubwa," alisema Ban. "Msisubiri mashauriano, chukuweni tu hatua."

"Tunapaswa kufanyakazi sasa ili ugonjwa huu usiwe ukimwi unaofuata wa dunia," Mkurugenzi wa CDC Tom Frieden aliwaonya viongozi wa Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia na shirika la fedha duniani waliokutana mjini Washington.

Mwanamke Mmarekani Nancy Writebol aliepona Ebola baada ya kutibiwa.

Mwanamke Mmarekani Nancy Writebol aliepona Ebola baada ya kutibiwa.

Lakini Liberia, ambako idadi rasmi ya vifo ilitajwa na WHO kuwa 2,316 siku ya Ijumaa, serikali ilisema iliwapiga marufuku waandishi wa habari kuingia katika kliniki za Ebola, ikihoji kuwa ni katika kulinda faragha za wagonjwa. Hatua hiyo ilikuja wakati wauguzi katika kliniki kubwa zaidi ya Ebola ya serikali wakianza mgomo baridi mjini Monrovia, wakidai malipo ya hatari, na kupuuza maombi ya maafisa wa Umoja wa Mataifa kuepusha mgomo wakati wa mgogoro huu.

Nchini Ufaransa, watu waliondolewa kutoka jengo la umma kwa muda katika kiunga cha mji wa Paris siku ya Alhamisi, baada ya mwanaume wa kiafrika kuugua. Mapema, kuwasili kwa kundi la wanafunzi kutoka Guinea kulisababisha hofu katika shule ya Ufaransa. Lakini katika matukio yote, uwezekano wa Ebola uliondolewa.

Mercedonia iliwaweka karantini watu waliokaribiana na Muingereza aliefariki siku ya Alhamisi baada ya kuonyesha dalili za Ebola. Maafisa wa afya wa Brazil walimuweka karantini raia wa Guinea aliehofiwa kuwa na Ebola, lakini walisisitiza kuwa ilikuwa ni hatua tu ya tahadhari, na mwanaume huyo hakuwa tena na homa na dalili nyingine za Ebola.

Serikali ya Morocco ilitoa wito wa kuahirishwa mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika ya mwaka 2015 kutokana na kitisho cha Ebola.

chanzo Dw.de

No comments:

 
 
Blogger Templates