Sikupata shida kugundua kuwa alikuwa ni mzee Mukulungu ambaye kule huitwa Mkuu. Nilibaki natetemeka, nisijue cha kufanya. Kwa kweli niliogopa sana!
SASA ENDELEA...
MAPIGO ya moyo wangu yalibadilika kabisa, yalikwenda kwa kasi kuliko kawaida. Niliangalia huku na huko, sikuona kitu. Nilibaki kama niliyepumbaa kwa muda ambao sikuujua.
Nilitetemeka sana!
“Nakuuliza, umenielewa?”
“Sijaelewa. Kifupi sikuelewi? Kwa nini msiniache na maisha yangu?”
“Hatuwezi kukuacha wakati kuna deni la baba yako. Hilo ndilo linalokutesa, vinginevyo tungekuacha huru.”
Nikazidi kuchanganyikiwa, kila aliponiambia kuhusu baba yangu, akili yangu ilizubaa. Baba yangu anaingiliana vipi na mimi? Labda ni kweli alikuwa mchawi, maana sikuwahi kuona kiashiria chochote kutoka kwa mzee wangu, ambacho kilimkaribisha na mazingira ya uchawi.
Hata kama ikiwa kweli, kwa nini mimi niingizwe kwenye mambo yao? Kwenye mikataba ambayo siifahamu na sijui makubaliano yao? Kwa nini?
Kwa hakika nilichanganyikiwa sana!
Nilitamani kuepukana na mkasa ule, lakini sikuwa na uwezo. Sikujua nilitakiwa kutoa jibu gani kwa yule mzee. Nilibaki kimya tu natetemeka, lakini cha ajabu, mke wangu Rita akiwa haonekani kugundua chochote.
“Mimi na baba tunahusiana vipi?”
“Swali la kipumbavu kabisa...hujui uhusiano wako na baba yako? Mnahusiana damu. Halafu hicho kiburi chako wewe, tulipaswa tuwe tumeshakuua, bahati yako ni mtoto wa mwisho.”
“Niacheni jamani. Niacheni niendelee na haya maisha yangu kama yalivyo.”
“Hatuwezi kuendelea kubishana, jioni utakuwa makao makuu, kwa heri.”
Muungurumo mkali ukasikika, sauti kama radi ikafuatia kisha nikahisi kama upepo mkali sana ukivuma kwa kasi, kisha kukawa shwari!!!
“Kwa nini mimi?” nikasema kwa sauti.
Hapo ndipo Rita alipojitahidi kujigeuza na kuniangalia. Sauti ile aliisikia vyema, inamaana kuwa, muda wote ule hakusikia kitu chochote nilichozungumza...
“Kuna nini mpenzi wangu?” akaniuliza akionekana kunionea huruma ya wazi kabisa.”
“Acha tu mama.”
“Usijali nitapona mke wangu, najua ni kwa kiasi gani unaumia. Najua ni kwa kiwango gani huna furaha kutokana na hali hii niliyonayo, lakini jipe moyo, nitakuwa sawa!”
Hapo nikawa na uhakika zaidi kuwa, Rita hakuna alichokuwa akikijua. Sikutaka kumwambia chochote, isingekuwa sawa kumwambia kuwa mimba zake zilikuwa zinatoka kwa sababu ya kafara ya majini ambayo yalikuwa yanafanya kisasi.
Sikutaka kabisa ajue jambo hilo, hiyo niliendelea kuifanya siri iliyokuwa katikati ya moyo wangu. Nilimsihi atulie, nikamwambia sikuwa na tatizo kubwa bali nilichanganywa na namna mimba zake zilivyokuwa zikiharibika kila mara.
“Nataka sana watoto mpenzi, natamani kuona vurugu za watoto wetu humu ndani, ndiyo maana unaniona sina raha,” nikamwambia.
“Hata mimi pia, ndani ya moyo wangu natamani sana jambo hilo, ndiyo haja ya moyo wangu mpenzi. Tutulie, muda ukifika mambo yatakuwa mazuri,” akasema Rita akiwa hajui kabisa kilicho kichwani mwangu.
Nikajituliza kisha nikaendelea kula chakula changu. Sikuwa na raha kabisa. Nilipomaliza nilipanda kitandani, kisha nikajilaza, kichwa changu kikiangalia juu ya dari, mawazo tele yakiwa yamenisonga!
***
“Galos! Galos! Galos...” kwa mbali nilisikia nikiitwa jina.
Sikugeuka, nilihisi nilikuwa ndotoni. Ilikuwa usiku wa saa sita, nikiwa nimelala na mke wangu Rita ambaye wakati huo alikuwa akisema kuwa hali yake iliendelea vizuri.
Nikapuuza!
“Galos! Galos! We Galos...” sauti ile ikaendelea kuita.
Nikatulia, nikatingisha mwili wangu kidogo ili kujihakikishia kuwa sikuwa ndotoni. Ni kweli sikuwa kwenye ndoto kama nilivyokuwa nikifikiria awali.
“Galos!” sasa ikaita kwa sauti ya juu kidogo.
“Nani?” nikauliza.
Mtu huyo alikuwa akiniita kupitia dirishani. Pamoja na kumwuliza alikuwa ni nani, hakujibu kitu. Dakika ya kwanza ikakatika, ikafuata ya pili! Nikashindwa kuvumilia.
“Wewe ni nani?”
“Naitwa Ngoma.”
“Ngoma?” nikauliza kwa mshtuko dhahiri.
“Ndiyo ni Ngoma, nipo na rafiki yangu Mango.”
“Naomba muondoke kwangu,” nikasema kwa hasira.
“Wewe huna ubavu wa kutufukuza, nadhani ni vema kama ukitoka mwenyewe ndani tukaondoka.”
“Kwenda wapi?”
“Makao makuu.”
“Haiwezekani.”
“Itawezekana,” alijibu huku tayari akiwa ameshaingia ndani kwangu.
Sikujua ni nani kati yao aliyeingia ndani, lakini niliona mtu mmoja tu. Alisimama mbele ya kitanda chetu, akaniangalia kwa macho yaliyoonekana kung’aa sana kwa mwanga mkali, kisha akapuliza dawa fulani ya unga iliyokuwa kwenye kiganja chake...
Nikapoteza fahamu!
***
Kwa harakaharaka niliwaona watu kama kumi wakiwa wamekaa kwenye zulia kwa mzunguko. Ulikuwa mduara mkubwa, halafu mimi nilikuwa nimekaa katikati. Mbele yangu kulikuwa na nyama mbichi, tena inayochuruzisha damu!
Wale watu wote walikuwa wameinamisha vichwa vyao chini. Nikawaangalia, lakini hakuna aliyeniangalia hata mmoja. Cha kushangaza, sikuwaona Ngoma, Mango wala Mkuu.
Muda kidogo, nikasikia vishindo, nikawaona watu wawili wakiingia. Nilipowaangalia nikagundua walikuwa ni Mango na Ngoma.
Wale watu wakainua vichwa vyao juu mara moja na kuviinamisha tena. Kidogo, akaingia Mkuu akiwa amevaa joho linaloburuzika chini!
“Mkuuu!” Mango na Ngoma walisema kwa wakati mmoja.
Watu wote wakasimama wakati mkuu akiingia. Akaonyesha ishara kuwa wote waketi – wakafanya hivyo. Akabaki yeye mwenyewe akiwa amesimama. Tofauti pekee niliyoiona ni kwamba, wale watu waliokuwa wameinamisha vichwa vyao, sasa walikuwa wameviinua!
Mkuu akaanza kuzungumza...
“Nina furaha sana jioni ya leo. Tunakwenda kufanya tukio moja kubwa sana...kuna mgeni hapa kama mnavyoona na kama nilivyowapa taarifa zake. Anaitwa Galos. Jambo la kufurahisha ni kwamba ameshakunywa damu ya mwanaye. Zoezi lililobaki ni kula maiti ya mwanaye.
“Zoezi hilo halitafanyika leo, kwa leo anatakiwa kusaini mkataba na kuanza kazi mara moja. Kuna mambo mawili tu, asaini maisha yake yabadilike yawe mazuri au asisaini, tumuue, mimi ninywe ubongo wake,” akasema Mkuu.
“Sawa Mkuu,” wote wakaitikia wakiinamisha vichwa chini.
“Galos...” Mkuu akaniita.
Sikuitikia!
Siyo kwamba nilionyesha kiburi, sikuweza kufanya hivyo!
Inaendelea
No comments:
Post a Comment