Social Icons

Sunday, 5 October 2014

HADITHI: Nilitafuna maiti ya mwanangu niwe tajiri -7


“Sawa Mkuu,” wote wakaitikia wakiinamisha vichwa chini.
“Galos...” Mkuu akaniita.
Sikuitikia!
Siyo kwamba nilionyesha kiburi, sikuweza kufanya hivyo!
SASA ENDELEA...

KAMA moyo ungekuwa unaweza kuonekana, naamini bila shaka yoyote moyo wangu ungeonekana ukiwa unatetemeka kwa hofu. Sikuwa na hili wala lile. Nilihisi kuchanganyikiwa.

Niliinua uso wangu na kuwatazama wale watu waliokuwa wamenizunguka, nikawaona kama wananikodolea macho mimi wakinishangaa.

Nikazidi kuchanganyikiwa. Kuna mambo matatu yalikuwa yakiuchanganya sana ubongo wangu. Kwanza kuhusu mkataba! Naweza kusaini mkataba wa kishetani?

Naweza kuingia kwenye makubaliano nisiyoyaelewa? Inamaana mimi niwe mchawi? Niliwaza. Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu lazima jambo hilo lingemchanganya kama ilivyokuwa kwangu.

Pili ni kuhusu kunywa damu! Mimi nilikunywa damu ya mwanangu? Inawezekana vipi? Ni kweli nilipewa kitu kama juisi ambayo ladha yake sikuijua mara moja, lakini kwa nini niambiwe ilikuwa ni damu ya mwanangu?

Damu ya mwanangu kivipi? Lingine kubwa kabisa lililoniumiza ni kuhusu kula maiti ya mwanangu. Nitaweza kumtafuna mwanangu? Kwa muda mrefu kiasi gani mimi na mke wangu tumehangaika kupata mtoto na mimba zinatoka!

Leo iweje nije kula maiti ya mwanangu? Ni mambo ambayo yalizidi kunikoroga! Kwa namna fulani niliona ni bora kufa kuliko kula maiti ya mwanangu. Potelea mbali hata kama Rita atabaki katika mateso lakini hatanyanyasika tena maana atapata mwanaume mwingine ambaye atamzalia watoto.

Mimi nisingeweza kumpa watoto kwa sababu tayari nilikuwa kama kafara la majini! Moyo wangu ulijaa huzuni sana, nikapata nguvu mpya na jeuri ya hali ya juu kunijaa moyoni. Nilimwangalia Mukulungu kwa hasira, sura yangu ikatangaza dharau ya wazi.

Nilionekana waziwazi nilikuwa tayari kwa lolote!
Ni kama nilikuwa nimejipanga sawasawa. Nikazidi kumkazia macho bila kuyapepesa kabisa. Naye akaniangalia kwa ukali. Muda uleule, nikaona kitu kama machozi yakidondoka machoni mwa Mukulungu. Nilipotazama vizuri, niligundua jambo jingine la kushangaza sana.

Macho ya Mukulungu yalikuwa yakidondosha damu! Tena ilikuwa damu mbichi kabisa!
“Galos! Galos! Galos!” akaita kwa ukali.

“Ukali wako haunitishi,” nikajikuta nimetamka kwa haraka nikiwa najiamini kuliko kawaida.
Pamoja na woga niliokuwa nao tangu mtiririko wa tukio lile ulivyoanza, nilijishangaa sana kupata nguvu ya ajabu na ya ghafla sana mbele ya Mukulungu ambaye aliogopwa na kila mtu!
“Unasemaje?”

“Nipo tayari kwa lolote!”
“Umeuuzunisha moyo wangu. Kwa hakika moyo wangu sasa unavuja damu....damu inachuruzika. Sasa nitakuuliza kwa mara ya mwisho kabla sijachukua hatua inayokustahili. Uko tayari kusaini mkataba au haupo tayari?” akauliza Mukulungu akinikazia macho.

“Sipo tayari!”
“Unasema?”
“Sipo tayari.”
“Galos, una hakika na kinachotoka kinywani mwako.”

“Nasema sipo tayari kusaini ujinga!”
“Paaaaa! Paaaaa! Paaaa!” ilikuwa ni mlio wa mikanda ikishuka mwilini mwangu.

Sikuelewa ni nani aliyenipiga na alikuwa wapi. Nilihisi maumivu makali sana, mwili wangu ukaishiwa nguvu ghafla na nikahisi kutapika. Nilijilazimisha kutoa matapishi lakini haikuwezekana. Nikajitahidi tena na tena lakini haikuwezekana.

“Mpelekeni kwenye hatua ya pili haraka! Huyu nitamalizana naye mwenyewe, hana ujanja huyu. Mpumbavu kabisa. Wa kumlaumu ni baba yako aliyeingia mkataba na sisi!” akasema Mukulungu.

Wale watu haraka wakanivaa. Kila mmoja alikuwa akinisukuma huku akinipiga sehemu anayoona inamfaa. Ndani ya dakika kumi tu, tayari kila kiungo katika mwili wangu kilikuwa kimeshapigwa. Nililainika na nilipatwa na maumivu makali kuliko kawaida.

Waliniburuza hadi kwenye chumba ambacho sikukielewa kilivyokuwa, lakini muda mfupi sana baadaye, nilipoteza fahamu kabisa! Sikujua chochote kilichoendelea.
***
Nilihisi maumivu makali sana miguuni, mwili wangu ulikuwa una joto kali kuliko kawaida, baadaye nikagundua kuwa siyo joto tu, ni moto mkali ulikuwa unatembea mwilini mwangu. Nilipofumbua macho, nilishangaa kujiona nimening’inizwa, kichwa chini, miguu juu.

Miguu yangu ilikuwa imefungwa kwa mnyororo juu ya kamba, mikono yangu ilikuwa chini lakini nayo ilikuwa imefungwa kwa mnyororo, chini kukiwa na moto ambao ulikuwa ukinielekea pale juu nilipokuwa nimefungwa!

Nilikuwa nachomwa kama nyama!
Ni eneo ambalo sikulijua ilikuwa ni wapi, lakini ilikuwa pembeni ya kitu kama ziwa au bahari, maana niliona nipo ufukweni. Nilipoangalia kando nikamuona Mukulungu akiwa na wenzake wawili wananitazama.

Wote walikuwa wamekenua meno yao wakinicheka. Mukulungu ndiye aliyekuwa amebeba kitu kama faili lenye makaratasi. Akaacha kucheka na kusogea karibu yangu. Akanitazama kwa macho ya hasira sana. Alionekana kuwa na neno alilotaka kuzungumza...

“Utakufa hapo mtini taratibu kama ng’ombe anavyobanikwa baada ya kuchomwa. Hili ni zoezi la mwisho kwako. Ni adhabu ya mwisho. Narudia tena hakuna adhabu nyingine, maana adhabu hii itakufikisha moja kwa moja kwenye kifo.

“Sasa ni hiyari yako kusema, upo tayari kusaini mkataba uendelee na maisha yako na tukupe utajiri au ufe hapo mtini ukibanikwa kama nyama ya ng’ombe?” akasema Mukulungu akiniangalia kwa macho yanayosubiri majibu.

“SITASAINI UCHAFU WENU, KAMA KUFA NIPO TAYARI KUFA!” nikamjibu kwa kujiamini.
Nilihisi maumivu makali sana lakini sikuwa tayari kabisa kujiunga na mambo nisiyoyajua wala sikuwahi kuyaota. Nilikuwa tayari kwa lolote! Mukulungu na wenzake wakaonekana kunishangaa sana!
“Unasemaje wewe?” Mukulungu akauliza.

“Nilivyosema ndiyo hivyohivyo!”
“Ongeza moto tafadhali,” akasema Mukulungu.
Muda huohuo, moto ukaongezeka ghafla. Nikahisi mwili mzima ukiungua.

Itaendelea 

No comments:

 
 
Blogger Templates