Wakashuka garini kwa pamoja, wakaanza kunifuata huku nyuso zao zikionekana dhahiri walinifuata kwa shari!
SASA ENDELEA...
NILIJARIBU kuvuta kumbukumbu zangu vizuri kuona kama ningeweza kuwakumbuka wale vijana, zikagoma. Hakuna mtu niliyemfahamu kati yao. Kilichonishangaza ni namna walivyokuwa wakinifuata.
Walionekana wazi kuwa wanamfuata mtu wanayemjua kwa uhakika kabisa. Walikuwa wananifuata mimi. Kilichonitisha ni ile hali ya kuja wakiwa wanaonekana wana uhakika kuwa mimi mtu wanayemfuata.
Nilitaka kukimbia lakini sikujua ni kwa nini miguu ilishiiwa nguvu. Nikiwa bado nawashangaa, Patrick alitokea akiwa ameshika shilingi elfu kumi mkononi. Ni ile niliyomuomba.
Kabla hajanifikia, tayari wale vijana wawili walishafika, wakasimama mbele yangu. Nyuso zao zilitangaza vita. Zilikuwa zimekunjamana wakionekana dhahiri kama wamekuja kulipiza kisasi.
Sijui nini kilitokea, lakini ghafla nikashangaa Patrick akirudi nyuma kwa hofu, tayari wale jamaa walikuwa wameshanifikia kabisa. Walikuwa wamesimama mbele yangu.
“Galos!” mmoja wa vijana wale akaita.
“Ndiyo, vipi?”
“Achana na mambo ya vipi.”
“Mnasemaje?” niliuliza nikiwa nimejawa hofu.
“Tunasemaje?” mwingine akadakia.
“Mbona siwaelewi, ninyi ni akina nani na mnataka nini kwangu?” nikawauliza tena.
“Dar es Salaam ni ndogo sana. Huwezi kujificha milele, sasa tumekukamata. Songa kule...” akasema mmoja wao.
Sikujua ilivyokuwa, ni kama niliduwazwa hivi, nikajikuta natembea mwenyewe kuelekea kwenye gari. Mmoja wao alinifungulia mlango, ulikuwa wa kiti cha nyuma.
Nilipokaa tu, nikagundua kuwa kwenye gari kulikuwa na mtu mwingine amekaa mwishoni, mimi nikakaa katikati kisha yule mmoja wa wale niliokuwa nao nje, akaketi dirishani, mwingine akaenda kwenye kiti cha dereva.
Gari likaondolewa.
***
Niseme ule ukweli kutoka moyoni mwangu, akili hazikuwa zangu kwa muda. Nilihisi kupumbazwa, baadaye nikaona kiza kidogo, kisha nikahisi usingizi mzito sana.
Nikalala.
Sina hakika kama nililala au nilipoteza fahamu, lakini fahamu kuwa, sikuwa na mawasiliano tena na watu wale kwa muda.
Sikujua chochote kilichoendelea!
***
Nilihisi baridi kali sana, kwa mbali nikasikia muungurumo wa maji yalipiga kwa kasi. Ni kama vile nilikuwa nimesimama ufukweni mwa ziwa au bahari. Sikuwa na hakika ni wapi hasa kati ya sehemu hizo.
Macho yangu yalikuwa mazito kufumbuka. Nilijitahidi sana kuyafumbua lakini ilishindikana. Ghafla maji ya baridi yakamwagwa mwilini mwangu. Nilishtuka kwa kasi na kufumbua macho.
Nikasimama.
Nilikutana na kitu cha ajabu sana. Mtu mmoja, mrefu, mweusi, mwenye ndevu nyingi alikuwa amekaa kwenye kiti cha mbao mbele yangu. Nyuma yake kulikuwa na wasichana waliokuwa wameshika vifaa maalum vilivyotengenezwa kwa ngozi, wakimpepea!
Pembeni yangu kulikuwa na wale vijana wawili walionichukua mtaani kwangu Tandale. Wakaniangalia mara moja, kisha wakarudisha macho yao kwa yule mzee.
Kwa mara moja, wote wakaainamisha vichwa vyao na kuvirudisha juu!
“Mkuu, tumekamilisha kazi uliyotuagiza!” wakasema wote kwa wakati mmoja.
Yule mzee akatingisha kichwa.
“Mango!” yule mzee akaita.
Kijana mmoja wao, akaitikia kwa sauti: “Naam! Mkuu.”
“Kushoto...” akasema, mara moja huyo jamaa ambaye sasa niligundua kuwa anaitwa Mango, akasogea mkono wangu wa kushoto, akanishika bega.
“Ngoma!” akasema tena, yule kijana mwingine akaitikia:
“Mkuu.”
“Kulia.”
Naye akasogea kulia kwangu na kusimama kisha akaniwekea mkono begani. Kusema ule ukweli, sijawahi kuhisi woga kama niliopata siku hiyo. Niliogopa kuliko kawaida. Mpaka muda ule, sikuwa ninajua nilikuwa wapi na nilifanya kosa gani. Nilibaki nimesimama nikiwa sijui la kufanya.
“Galos,” yule mzee akaita.
“Ndiyo mzee.”
“Najua hujui hapa ni wapi.”
“Ni kweli sijui.”
“Hapa ni pembeni mwa Kata ya Sandulula, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Mkoa wa Rukwa.”
“Nimefikaje? Kwa nini nipo hapa na mmenileta kufanya nini?”
“Unamfahamu Matima Mtimandole?”
“Ni baba yangu mzazi, kwa sasa ni marehemu.”
“Yeye ndiye sababu ya wewe kuwa hapa. Unafahamu alichotufanyia?”
“Sijui, lakini ninyi ni akina nani?”
“Hayo utayajua baadaye, lakini unatakiwa kufahamu kitu kimoja, mkeo hawezi kuzaa mtoto akabaki salama katika maisha yake yote. Tutaendelea kuharibu mimba zake kila siku.
“Najua sasa hivi ana mimba nyingine. Kwa taarifa yako, pia imeshaharibika. Mkakati wa mwisho uliokuwa umebaki ulikuwa ni kumuua kabisa mkeo, kukuua na wewe ili kizazi chenu kipotelee mbali.
“Tulikuwa na uwezo wa kufanya hivyo muda mrefu kabla, hata sasa tunaweza kufanya hivyo, ndiyo maana umeona umetoka Dar es Salaam hadi Rukwa kwa nusu saa tu. Hujui umefika wala usafiri uliotumia.
“Makosa ya baba yako, ndiyo unayotakiwa kuyatumikia wewe. Adhabu tumeshaipitisha – ni kifo. Tutaanza na mkeo, halafu wewe. Hakuna mtu yeyote atayejua tukio hilo,” alisema mfululizo kwa sauti huku sauti yake ikiunguruma.
“Mango...” akaita.
“Ndiyo mkuu.”
“Peleka eneo la tukio!”
Nihisi mwili ukiniisha nguvu! Mango na Ngoma wakanishika juujuu, kisha wakaanza kutembea kunipeleka nisipopajua!
Inaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment