Social Icons

Friday, 10 October 2014

HADITHI: Nilitafuna maiti ya mwanangu niwe tajiri -12


“Hili ndilo sharti unalotakiwa kulitimiza, ule maiti hii ya mtoto wako, ndipo utakuwa tajiri! Uko tayari?

Mwili wa Galos ulikuwa ukitetemeka kama mtu mwenye homa kali, yote hiyo ilikuwa ni kwa sababu ya hofu. Moyo ulimuuma mno, kumwona Mukulungu ameshikilia maiti ya mtoto wake mkononi, tena kichwa chini miguu juu, akining’iniza.

Machozi yakambubujika. Hakuna kitu alichokipenda maishani kama watoto, yeye na mke wake kwa muda mrefu walikuwa wametamani kuwa na mtoto pamoja na umasikini wao, waliamini huyo ndiye angewapa faraja lakini Mukulungu bila huruma aliua kila mtoto waliyempata.
“Kwa nini mnanitendea hivi?” aliuliza kwa uchungu.
“Unataka kuwa tajiri hutaki?”

“Nataka!”
“Basi timiza masharti.”
“Huu ni unyama.”
“Umasikini unatenda unyama zaidi kuliko mimi, umeteseka kwa miaka mingi, hivyo basi kama umechoka na aina hiyo ya maisha, kula maiti ya mwanao!”

Galos akainamisha kichwa, fikra zake zote zikarejea kitandani alikomwacha mkewe Rita akiwa mwenye huzuni. Mwanamke huyo asiye na hatia hakujua kabisa kilichokuwa kikiendelea maishani mwake, mwenye siri moyoni alikuwa ni mumewe, Galos akamwonea huruma, lakini hakuwa na jinsi, umasikini ulikuwa umemchosha, akapiga hatua na kusimama mbele ya Mukulungu.
“Niko tayari, ili mradi tu mke wangu asije kufahamu siri hii.”

“Hawezi kufahamu, mambo ya huku huwa hayasemwi, isitoshe yeye pia kama hatasaini mkataba wa kurithi kazi ya baba yako, atakufa!”
“Tafadhali msimuue mke wangu.”

“Achana  na hiyo, chukua haka kamaiti ka mwanao ukakachome pale kwenye moto unaowaka, kisha ule, baada ya hapo utarejea nyumbani na kila kitu kitakachotokea kitakushangaza, utatajirika bila juhudi yoyote.”

Galos akanyoosha mkono wake wa kuume, huku mkono wa kushoto akiutumia kufuta machozi na  makamasi, akaishika maiti ya mwanaye miguuni, hivyohivyo akiining’iniza alitembea mpaka kwenye moto na kuiweka juu ya wavu, wachawi wote wakashangilia, wakimwita Shujaa.

Maiti ilichomwa kama mshkaki au kuku juu ya jiko la mkaa, ikaendelea  kudondosha maji na mafuta hatimaye ikakuka kabisa, ndipo Mukulungu akamwamuru Galos aiondoe kwenye moto na kwenda nayo kando ambako majani ya mgomba yalikatwa na kuwekwa juu yake, wachawi wengi wakamzunguka.
“Kula! Kula  uwe tajiri.” Mukulungu alisema.

Huku akilia Galos akakata mguu wa maiti ya mtoto wake, macho yake yakiwa yamefumbwa, akaanza kuila bila  huruma, kichwani mwake akiwaza utajiri, magari atakayokuwa akiendesha, majumba ambayo angemiliki, heshima ambayo angepewa katika jamii.

Alipomaliza tu kula ghafla alizinduka usingizini na kumkuta mke wake ameketi kitako akilia, akaanza kumbembeleza na kumtuliza. Rita alitaka kufahamu ni kwa nini Galos alilia sana akiwa usingizini, lakini hakuambiwa ukweli. Wote wawili hawakulala usingizi, saa kumi na mbili kasorobo za asubuhi, Galos aliamka na kutoka nje ya nyumba yao kwenda msalani kujisaidia haja ndogo.

Alipofungua tu gunia lililotumika kama pazia kwenye choo, alishangaa kuona kitu kiking’ara ardhini, taratibu akainama na kukiokota, kilimshangaza, alishasikia sana juu ya Almasi, Ruby na Dhahabu, hisia zake zilimtuma kudhani hiyo ilikuwa ni Ruby.

Haja kubwa na ndogo zote zikakata, akasahau hata chooni alikwenda kufanya nini, haraka akarudi hadi ndani akiwa amekishika kipande cha jiwe alichokiokota mkononi mwake.
Ndani hakuongea kitu, akaifuata suruali yake ya khaki iliyokuwa imetundikwa kwenye msumari na kukiweka ndani yake, uso wake ulikuwa umekunjuka na kujawa na furaha iliyomshangaza Rita.
“Vipi tena?”

“Ahaa!Ahaaa!”
“Mbona umechangamka?”
“Basi tu.”

Jua lilipochomoza hakutaka hata kusubiri kifungua kinywa, aliondoka moja kwa moja akitembea kwa miguu hadi katikati ya jiji eneo la Kariakoo ambako alianza kutafuta mahali ambako watu walinunua madini, baada ya kuuliza alijikuta yuko mtaa wa Mafia, kulikokuwa na mnada wa wauza madini, akaingia kwenye moja ya ofisi.
“Mnanunua madini?”
“Ndiyo.”

“Mnaweza kununua la kwangu?”
“Lipi?”
Galos hakuwa na jibu, alichokifanya ni kuingiza mkono mfukoni mwa suruali na kutoa kipande cha jiwe alichokuwa nacho na kukiweka juu ya meza, watu wote ndani ya chumba hicho walisimama na kuonyesha mshangao, hapo ndipo akaelewa alikuwa na kitu cha thamani alichokipata kimazingara.
“Umeipata wapi Almasi kubwa kiasi hiki?”
“Niliachiwa na baba.”

“Mungu wangu! Hebu subiri.” Aliongea mtu huyo na kuiweka juu ya chombo kilichoonekana kuwa mzani.
“Gramu ngapi?” mtu mwingine aliyekuwa chumbani aliuliza.
“Mia moja na hamsini.”
“Mungu wangu! Haijawahi kutokea hapa ofisini, nimefanya kazi hapa kwa miaka karibu thelathini, kijana umetajirika, una akaunti?”
“Sina.”

“Utatuuzia?”
“Ndiyo, kama tutaelewana bei.”
“Unauzaje?”
“Kwani ninyi mna bei gani?”
“Subiri.” Alisema mtu huyo akivuta mashine ya kupigia hesabu na kuanza kubonyeza namba fulanifulani, kisha akamwonyesha Galos, kulikuwa na sifuri nyingi zilizotanguliwa na mbili, kisha tano!
“Kiasi gani hicho?”

“Utapata milioni mia mbili na hamsini.”
“Sawa.”

Biashara ikawa imefanyika, bila Galos kuelewa thamani hasa ya Almasi yake, wanunuzi wakamsaidia kufungua akaunti kwenye benki ya kizalendo ya Wezesha Mzawa, kiasi cha milioni ishirini  na tano akazichukua na kwa msaada wa watu haohao, akanunua gari aina ya Mark II, kuajiri dereva, kufanya manunuzi ya nguo za thamani kwa ajili yake ya mkewe, kutafuta nyumba ya kifahari ya kupanga maeneo ya Mikocheni.

Mfukoni akabaki na milioni tatu baada ya kununua samani za ndani ya nyumba yake, ndipo akamwamuru dereva amwendesha kuelekea nyumbani. Alipofika, kitu cha kwanza alichofanya ni kupiga honi mbele ya kibanda chao, Rita akatoka akiwa ameshika sufuria la ugali na kumwaga ukoko kando ya barabara, kichwani mwake akiwa hajui kabisa ndani ya gari hilo alikuwemo mumewe.
“Mpenziiiii!” Galos aliita, Rita  akageuka kuangalia.
“Hee!”

itaendelea

No comments:

 
 
Blogger Templates