Tarehe 9 Oktoba 1989, anasema Alexander Kudascheff, ni siku ya mapinduzi ya amani nchini Ujerumani ambapo maandamano yaliyoanza siku hiyo ndiyo yaliyochochea kuporomoka kwa mfumo wa kikomunisti.
Japokuwa maandamano hayo ya Jumatatu yaliyoanza na malalamiko ya umma mjini Leipzig hayakuwa ya mwanzo, lakini yalikuwa makubwa kupita kiasi na ndiyo yaliyobeba mabadiliko. Hii ni siku ya historia ya uhuru kwa Ujerumani na kwa Ulaya, kwani watu 70, 000 walikusanyika kuandamana dhidi ya chama cha SED kilichokuwa kikitawala Ujerumani ya Mashariki - lililokuwa wakati ule taifa la pili la Ujerumani.
Waandamanaji hao walipaza sauti zao dhidi ya watawala wa kikoministi. "Sisi ndio wananchi". Maandamano ya umati wa watu wa chini dhidi ya "wale walioko juu" - vikaragosi walioko katika kamati ya uongozi wa kisiasa na kamati kuu ya wasiojua wananchi wanataka nini: Uhuru. Uhuru katika maisha, uhuru katika jamii na uhuru wa kusafiri na muhimu zaidi uhuru wa kwenda nchi za nje.
Makundi ya watu yalizidi kuteremka majiani kuandamana kila Jumatatu dhidi ya mtindo wa kufungiwa, na sio tu Leipzig, bali pia Halle na Eisenhüttenstadt, maelfu wengine walikuwa kwa upande wa pili wakiyapa kisogo maovu ya nchi hiyo na mfumo wake, lakini kinyume na sheria. Yalikuwa maandamano ya wasiokuwa na usemi ndani na nje ya GDR.
Tukio muhimu kabisa
Oktoba 9 lilikuwa tukio la mwanzo muhimu katika historia ya mwaka 1989 ya kudai uhuru wa Ujerumani. Ilikuwa siku ambapo wananchi zaidi ya 70, 000 waliopania, walithubutu kutamka "La" kwa serikali ya GDR.
Ilikuwa siku ya kwanza ya maandamano ya amani yaliyoendelea kwa muda wa wiki nne hadi Novemba 9 mwaka 1989, pale Ukuta wa Berlin ulipoporomoka. Zilikuwa wiki nne ambazo Wajerumani na watu wa Ulaya waliandika historia.
Ilikuwa siku ambapo Wajerumani, ambao kwa mujibu wa ujumbe uliowahi kutolewa na Lenin ni watu jasiri wenye kufuta nidhamu na wanaokifanya wanachokidhamiria, walisimama kidete wakifuata yaliyofanywa na wananchi wa nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki dhidi ya mfumo wa kikoministi, dhidi ya uimla, dhidi ya mfumo wa chama kimoja na dhidi ya ushawishi wa Moscow.
Kile kilichoanzishwa Poland na Chama Huru cha Wafanyakazi, Solidarnosch, mapema miaka ya 1980 na kubarikiwa na kiongozi wa Kanisa Katoliki,J ohanna Paulo wa Pili wa kutoka Poland, kiliripuka kwa muda wa wiki nne katika mataifa ya Ujerumani Mashariki, Czechoslovakia na Hungary. Wananchi walinyanyuka na mfumo wa kiimla wa kikoministi ukamomonyoka.
Watawala waliojisahau
Siku mbili kabla ya Oktoba 9, serikali ya Ujerumani Mashariki ilisherehekea miaka 40 ya kuundwa kwake kwa mbwembwe kubwa na gwaride la kijeshi. Lakini chama tawala na viongozi wa serikali hiyo hawakutaka kuuzingatia upepo wa mageuzi na kilio cha wananchi. Matokeo yake wakajikuta wakishinikizwa kwa njia ya amani na baadaye kutimuliwa.
Siku hiyo ndipo Wajerumani wa Mashariki walipoamua kuandika historia. Ndipo zilipofuata wiki nne za maandamano ya amani, mihadhara na kufuatiwa na mwisho wa kutengana Ujerumani na Ulaya.
Oktoba 9 ni mwanzo wa historia ya uhuru ya Ujerumani, ilikuwa hatua muhimu kuelekea Novemba 9. Ni siku ambayo Wajerumani wa Mashariki, wakaazi wa Leipzig, wanaweza kujivunia. Ilikuwa siku ambayo wananchi waliondowa woga wao mbele ya utawala wa kiimla.
chanzo dw.de
No comments:
Post a Comment