Damu zilikuwa zimetapakaa chumba kizima! Rita mke wangu kipenzi, alikuwa akigaragara kitandani!
Nikashtuka sana!
SASA ENDELEA...
NILIKODOA macho pale kitandani nikiwa siamini kabisa nilichokuwa nakiona. Ni kweli Rita alikuwa amelala pale kitandani akionekana mchovu sana. Hana nguvu.
Damu ndiyo zilinitisha zaidi, kitanda kizima kilikuwa chapachapa, achana na kitandani, damu nyingine ilikuwa inachuruzika chini. Nilihisi kizunguzungu.
“Rita...” niliita kwa sauti nikisogea kitandani kwa hadhari sana.
Hakuitika.
“Rita...” nikaita tena.
Bado hakuitika.
Moyo wangu ukapigwa na butwaa, nilihisi ganzi ikiushika moyo wangu. Nikasogea taratibu na kumtingisha, hakugeuka. Nikaamua kumgeuza mwenyewe.
Hapo ndipo niliposhuhudia macho yake yakifumbuka kwa mbali, akinitazama kwa huruma. Nilijaribu kumuita lakini hakuitika. Alionekana kutaka kuzungumza lakini ulimi wake ulikuwa mzito sana.
Nilishaanza kuhisi kilichotokea.
“Jikaze mke wangu, hebu niambie unajisikiaje?” nikamwuliza.
“Nakufa Galos, nakufa baba.”
“Hufi mpenzi wangu, hutakufa niamini mimi.”
“Kila mtu atakufa Galos, lakini muda wangu wa kufa umefika.”
“Najua kila mtu atakufa, najua hata wewe utakufa, lakini namaanisha kwa sasa hutakufa mpenzi wangu. Utakufa siku uliyopangiwa na Mungu itakapofika, siyo katika tatizo hili,” nikamwambia.
“Mimba imeharibika tena,” akasema.
“Najua mpenzi, pole sana.”
“Lakini Galos kwa nini inakuwa hivi? Kwa nini nakuwa kama vile nimetoa mimba? Sijawahi kufanya hivyo na wala sitafanya hivyo, kwa nini tumbo liniume sana halafu baadaye damu ziwe kama hivi?
“Hali itaendelea hivi hadi lini? Lazima tutafute ufumbuzi wa hili jambo, hatuwezi kuacha mambo yakawa hivi kila siku,” akasema mke wangu.
“Narudia tena kukuambia mama, niachie mimi. Hebu kwanza tuyaache yote, ngoja tujitayarishe twende hospitali,” nikamwambia.
“Hospitali?” akang’aka.
“Ndiyo, twende hospitali, kwani hujanisikia.”
“Siendi.”
“Kwa nini?”
“Kwani kuna nini cha maana ninachokifuata huko? Mara zote nilizokwenda walinisaidia nini? Hakuna cha maana kabisa. Acha tu nipumzike. Chemsha maji unikande.”
“Hapana, unahitajika kwenda hospitali mke wangu Rita, kwani hujionei huruma?”
“Najionea huruma sana, nataka kwenda hospitali sana lakini kwanza una pesa?” Swali lake likaninyong’onyesha moyo wangu.
Aliuliza swali la msingi sana ambalo kiukweli lilijaa ukweli mtupu. Sikuwa na fedha, hivyo kama nilitaka kweli kumpeleka hospitalini nilitakiwa kuwa na fedha.
“Sina mke wangu lakini nitapata tu,” nikamwambia mke wangu.
“Utapataje?”
“Najua mwenyewe.”
“Galos mume wangu, unanisikiliza lakini?”
“Nakusikiliza mama.”
“Nisaidie tu kubandika maji jikoni kisha unikande, nitapata nguvu,” akasema kwa sauti iliyojaa uchovu, akionekana kutokuwa na matumaini kabisa.
“Jiko lina mafuta?” nikamwuliza.
“Ndiyo...mafuta yapo kidogo, kwa kuchemsha maji tu, yanatosha sana.”
“Sawa.”
Haraka sana nikawasha jiko la mafuta, maarufu kama jiko la Mchina, nikamimina maji kwenye sufuria kisha nikabandika juu yake. Baada ya hapo, nikamgeuza mke wangu upande na kutoa lile shuka lenye damu.
Nikakusanya sehemu moja, kisha nikadeki zile damu pale chini. Baada ya kuwa pasafi kabisa, maji nayo yalikuwa yameshachemka kabisa. Nikayaepua na kumimina kwenye ndoo ya plastiki.
Nikachukua na mengine ya baridi kidogo, nikayachanganya ili kupunguza ule ukali. Nikamsaidia mke wangu kuteremka pale kitandani, nikamfunga kanga mbili, moja kiunoni na nyingine kifuani. Tukaongozana hadi bafuni, nikamkanda vizuri kisha nikamwogesha.
Akajisikia nafuu kidogo. Nikamrudisha chumbani. Ilibidi nitandike kitanda kwanza ndipo apande. Nikampaka mafuta kisha nikamfunika na shuka, akapumzika.
“Unajisikiaje sasa?” nikamwuliza.
“Nguvu kidogo lakini njaa.”
“Usijali mke wangu, nisubiri.”
Nikatoka mbio kwenda kwa rafiki yangu Patrick. Bahati nzuri nilimkuta.
“Vipi Galos,” akaniuliza.
“Poa..”
“Vipi? Mbona sikuelewi? Wale waliokuchukua ni akina nani na kwa nini ilikuwa vile?” akaniuliza akionekana kuwa na hofu.
“Ilikuwaje?”
“Wakati mimi nakuletea pesa uliyosema, nilishangaa kuwaona wale watu wakitaka kukuchukua mkukumkuku, nikajikuta narudi nyuma kiajabuajabu.”
“Kivipi yaani,” nikamwuliza.
“Nilishangaa nakosa nguvu ya kukufuata, kifupi nilijikuta narudi nyuma bila ridhaa yangu, lengo lilikuwa kuja kukusaidia lakini sijui nini kilitokea nini, kifupi nahisi kama ni nguvu za kishirikina.
“Kwani wale ni akina nani na ilikuwaje wakakuchukua? Halafu walikupeleka wapi? Unajua sielewi kabisa,” akasema Patrick mfululizo kiasi cha kunifanya nishindwe kumjibu kwa haraka.
“Kaka hebu tuachane na hayo kwanza, nimejia ile pesa kaka, bado nina matatizo makubwa sana ndugu yangu.”
“Sawa lakini ilikuwaje?”
“Kaka afya ya mke wangu kwa sasa ndiyo muhimu kuliko kitu kingine chochote, tafadhali nisaidie kwanza hiyo pesa niende nikamsaidie halafu mengine yatafuata baadaye,” nikamwambia.
Patrick hakuzungumza kitu tena, alinikazia macho kwa sekunde kadhaa kisha akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti moja ya shilingi 10,000, akanikabidhi.
“Ahsante sana.”
“Usijali kaka.”
Nilitoka mbio hadi dukani, nikanunua unga wa sembe nusu kilo, kisha nikapitia kwa Mama Nishe, nikanunua chakula. Ilikuwa ni wali na samaki, nikawekewa kwenye mfuko mdogo wa Rambo.
Nilipofika nyumbani, kwanza nikampikia mke wangu uji na kumsihi anywe, akajitahidi kunywa. Alipotosheka akarudi tena kulala.
Nikatoa kile chakula kwenye mfuko wa nailoni na kuweka kwenye sahani, nami nikaanza kula. Nikiwa katikati ya mlo wangu, mawazo yakaanza kunisonga tena kuhusu kule Rukwa waliponipeleka wale akina Mango na Ngoma.
Nikaanza kuwaza kuhusu marehemu baba yangu, mzee Matima Mtimandole. Niliumiza sana kichwa, lakini sikupata kiungio mahali popote kuwa baba yangu alikuwa mchawi.
“Yaani baba alikuwa mchawi? Kweli? Haiwezekani...” nikajisemea mwenyewe moyoni mwangu.
“Inawezekana sana na wewe unatakiwa kulipa deni letu. Nimeshakuambia acha kiburi. Labda nikuambie, tayari usajili unaendelea. Ile juisi tuliyokunywa , haikuwa ya matunda kama ulivyodhani.
“Ile ni juisi ya damu, tena damu mbichi kabisa. Damu iliyotoka kwenye mimba ya mkeo tuliyoiharibu. Leo jioni tunakuhitaji makao makuu haraka,” sauti hii iliyojaa muungurumo mkali niliisikia.
Inaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment