Dodoma. Ushindi wa kura mbili za wajumbe wa Zanzibar ambao uliwezesha kupita kwa Katiba inayopendekezwa, umeelezwa kuwa ulitokana na ushawishi mkubwa wa mjumbe Hamad Rashid Mohamed.
Siri hiyo imefichuka ikiwa ni siku tatu baada ya kupitishwa kwa Katiba inayopendekezwa na kuvunjwa kwa Bunge la Katiba baada ya kumaliza kazi yake.
Mmoja wa mawaziri waandamizi wa Serikali ya Muungano alilidokeza gazeti hiliJumapili kuwa ushindi wao ulipatikana kwa kusaidiwa na mkongwe huyo wa siasa kutoka Zanzibar. Waziri huyo alisema kitendo cha CUF kumweka pembeni kiongozi huyo, kiliwapa nafasi kubwa kumtumia katika kufanikisha azma hiyo na kuwa asingekuwa huyo, mambo yalikuwa ni magumu kwa namna yoyote.
Katiba inayopendekezwa ilipitishwa Alhamisi na sasa inatarajiwa kukabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete Oktoba 8, mwaka huu sherehe ambazo zitafanyika katika eneo litakalopangwa mjini Dodoma.
“Watu wanasema kuwa tumechakachua kura, hivi katika hali ya kawaida hawajui kuwa bila ya Mzee wa Wawi (Hamad Rashid) tungetupwa vibaya na tusingekuwa na chetu, ama labda tungetumia mbinu zingine,” alisema kiongozi huyo. “…Hivi mdogo wangu, kama mnavyowajua watu wa Zanzibar misimamo yao ni mikali sana na mara nyingi hawayumbishwi hata kwa jambo lolote, hapa siyo hizo kura mbili tulikuwa tunakosa kura nyingi sana.”
Alisema kuwa Serikali na Chama cha Mapinduzi wanamshukuru Hamad na kwamba wanaimani kupitia kwake ikiwa watamtumia vizuri itakuwa ni safari ya kifo cha CUF. Alipotafutwa kuzungumzia jambo hilo Hamad, kama kweli alitumia mbinu hizo alisema “Nimefanya kazi kubwa na nimefanikiwa hivyo ninamshukuru Mungu.”
Mjumbe huyo ambaye ana mgogoro na chama chake cha CUF, alisema kuwa mpango wa kushinda ulikuwa ni mgumu, lakini ilimlazimu kutumia mbinu zote anazojua hadi akajihakikishia ushindi.
Alijigamba kuwa, hata kama wangekuwapo wabunge wa CUF, bado angeibuka na ushindi kwa kuwa wako wengi wanaomsikiliza na kikubwa alikuwa akicheza kwa namba tu.
“Hata hawa Serikali mimi niliwaambia kuwa wasiwe na wasiwasi tutashinda na nilijua tunapitia wapi ili tuweze kushinda, maana kwanza wafanyakazi kutoka Zanzibar walikuwa kwangu na hata wale wajumbe ulioona wanapiga kura za siri niliwaambia wafanye hivyo lakini zikawa za ndiyo,” alisema.
Alisema kuwa kila mmoja aliyekwenda mbele kupiga kura ya siri, alikuwa akimuonyesha kwani alikaa mahali ambapo kulikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na wapigakura hao.
Alijisifia kuwa amefanikiwa kupigia na kupitisha Katiba ambayo anaamini itakuwa na demokrasia pana kuliko ilivyokuwa mwanzo.
Akizungumza zaidi alisema, kilichomkera ni kitendo cha kusumbuliwa na kudhalilishwa na watu wa CUF na wakisahau fadhira zake kwa mambo aliyoyafanya ndani ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment