Social Icons

Monday, 6 October 2014

HADITHI: Nilitafuna maiti ya mwanangu niwe tajiri -8


“Unasemaje wewe?” Mukulungu akauliza.
“Nilivyosema ndiyo hivyohivyo!”
“Ongeza moto tafadhali,” akasema Mukulungu.
Muda huohuo, moto ukaongezeka ghafla. Nikahisi mwili mzima ukiungua.
SASA ENDELEA...

NIkweli kabisa, tena ukweli usio na shaka kwamba mara nyingi nimewahi kupata maumivu. Hata hivyo, nakiri sijawahi kupata maumivu makali kama ya moto ule uliokuwa ukiwaka chini yangu, nikiwa nimening’inizwa juu.

Moto ulikuwa mkali sana, nilihisi mwili wangu ukiniteleza. Nikamkumbuka Rita wangu. Mwanamke wa maisha yangu ambaye nilimpenda kwa kila hali. Nakubali vipi kufa nimwache mwenyewe?

Nilimwonea huruma sana. Sikujali mimi kufa, nilikuwa tayari kufa kuliko kuingia kwenye uchawi. Hata siku moja sikupenda uchawi. Sikuwahi kufikiria kuwa naweza kujiingiza kwenye mambo ya uchawi.
“Mamaaaaaa...” nilipiga kelele.

Nilipojaribu kuangalia eneo ambalo Mukulungu alikuwa amekaa na wale wazee, hakuwepo. Hapakuwa na mtu. Kwa mbali sasa nilianza kufikiri kubadilisha mawazo. Hata kama sitakuwa mchawi, nilikuwa tayari kukubaliana nao ili tu niokoke katika ule moto.

“Rahisi sana...nasema nipo tayari, halafu wakinitoa hapa natoroka,” nikawaza.
“Mkuuuuuu...” nikapiga kelele.
Muungurumo mkali ukasikika.

“Mkuuuuu,” nikaita tena.
Muungurumo ukazidi.
“Unataka nini? Kufa hapohapo mtini,” nikasikia sauti ambayo sikuwa na shaka kuwa alikuwa ni Mukulungu.
“Hapana Mkuu, hapana.”

“Hapana nini?” Sasa nikasikia sauti hiyo mbele yangu.
Nikafumbua macho haraka, nikamuona Mukulungu akiwa mbele yangu. Amesimama ananitazama kwa macho makali. Machozi yalikuwa yakinitoka kwa kasi sana machoni mwangu. Machozi ukichanganya na damu, ilikuwa ni balaa juu ya balaa.

“Nisaidie,” nikamwambia.
“Umeshakuwa tayari kuwa nasi?” akauliza.
“Ndiyo.”
“Unasema?”
“Ndiyo Mkuu.”

“Ondoa moto!” akasema Mukulungu.
“Myvuuuuuu!” mlio mkali kama upepo ukasikika, ghafla ule moto ukaondoka.
Nikatetemeka. Mwili ulikuwa umeanza kutoka malengelenge, nikavuta pumzi ndefu sana kisha nikazishusha taratibu kabisa.
“Niokoe Mkuu.”

“Huwezi kuokolewa hapo kabla ya kukubali ninachokuambia,” akasema huku akiketi chini.
“Ndiyo Mkuu.”

“Kwanza lazima ujue kuwa sisi hatuna lengo baya na wewe. Kubwa zaidi ni kukusaidia. Tunahitaji kukusaidia maisha yako, acha ujinga.”
“Sawa, lakini kwa nini mmenichagua mimi?”

“Ngoja ushuke hapo juu kwanza tuzungumze,” akasema.
Nilihisi kizunguzungu cha ghafla, kisha nikahisi kama nimepoteza fahamu hivi. Naam! Ni kweli nilipoteza fahamu. Sikujua kilichoendelea tena baada ya pale.
***
Ni muda mfupi baada ya kutolewa kule kwenye ufukwe nilipokuwa nimening’inizwa. Sasa tupo kwenye chumba kilekile cha awali. Tofauti ni kwamba, wale watu waliokuwepo mwanzoni, safari hii hawakuwepo tena.

Pale kulikuwa na Mango na Ngoma tu. Mukulungu alikuwa amekaa mbele yangu, tukawa tunatizamana. Kitu cha kushangaza ni kwamba, ule uvimbe na malengelenge niliyokuwa nayo kule ufukweni, hayakuwepo tena.

Mwili haukuwa na maumivu tena. Ni kama hapakuwa na jambo lolote lililotokea kabla. Mukulungu alinikazia macho...
“Sasa nisikilize...” akasema.
“Ndiyo!” nikaitikia.

Ngoma na Mango, waliposikia kauli ya Mukulungu ikisema, sasa nisikilize, walisimama kwa wakati mmoja. Wakashikana mikono, halafu wakainamisha vichwa vyao chini, kisha wakaanza kutembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea mlangoni.

Walipomalizikia mlangoni tu, Mukulungu akaendelea: “Galos kijana wangu.”
Sauti ya Mukulungu sasa ilikuwa ya taratibu iliyojaa uungwana. Nilimshangaa kwa kweli. Sikutegemea kumsikia akizungumza nami kwa sauti iliyojaa unyenyekevu kama ile.

“Unajua watu wanafikiria vibaya sana kuhusu uchawi na ushirikina. Nikuambie tu ukweli kuwa, siyo kitu kibaya. Hii ni aina ya sanaa ambayo huwa na makubaliano rahisi. Makubaliano hayo yakifanyika, utajiri unafuata.

“Si kwamba unapewa utajiri kwa manyanyaso au unamdhuru mtu, hapana. Ni waongo wanaosema hivyo. Kwa mfano wewe ni kijana mzuri, una nyota nzuri, ni rahisi kuogelea kwenye utajiri kwa muda mfupi sana.

“Mazungumzo haya yakifikia mwisho na tukakubaliana vizuri, wewe utakuwa tajiri mkubwa sana. Acha woga, achana na mawazo potofu. Tumia uwezo wako kinyota kubadili maisha yako. Hebu nikuulize, unafaidika nini kuishi maisha ya kijinga pale Tandale?

“Kipi unachonufaika nacho kwa kiburi chako huku mkeo akiwa mgonjwa kila siku? Tumia akili. Sisi hatuna lengo baya na wewe. Jambo la msingi kujua ni kwamba, mwisho wa mazungumzo haya, ukiendelea na ule msimamo wako wa kukataa, UTAKUFA.

“Lakini ukiwa mwerevu, ukaingia mkataba na sisi ambao kimsingi ni wa lazima kwa sababu ya marehemu baba yako, basi utaanza maisha mapya. Acha ujinga mwanangu. Acha upuuzi, wewe ni mtu mkubwa sana mwenye utajiri mkubwa kwenye maisha yako. Unanielewa?” akasema.

Maneno yake yaliniingia sana, kiukweli nilijawa hofu sana. Sikuweza kumjibu haraka. Nilibaki namwangalia tu nisijue cha kufanya.
“Galos...” akaniita.
“Mkuu.”
“Umenielewa?”

“Ndiyo, lakini nataka kujua kuhusu baba yangu.”
“Vizuri sana. Hebu sasa nikueleze kwa undani kuhusu baba yako,” akasema.
“Angalia pale...” akasema akisonza kidole kwenye ukuta ambao kulikuwa na ngozi ya mnyama. 
Sikujua ni mnyama gani!
Nikaangalia!

Nilishuhudia mambo ya ajabu ya kushangaza. Hofu kuu ikanijaa, nikazidi kukodoa macho yangu. Mwili mzima ulitetemeka.

Itaendelea 

No comments:

 
 
Blogger Templates