Social Icons

Tuesday, 7 October 2014

Lembeli: CCM ilinihujumu uchaguzi 2010

Dodoma. Mbunge wa Kahama, James Lembeli amemtuhumu Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuph Makamba kwamba alikuwa nyuma ya mpango mahususi wa kumhujumu ili akose ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Lembeli, mmoja wa wabunge walio mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi, alisema mpango huo ulitekelezwa kwa kueneza taarifa za kuanzisha jimbo la Ushetu ambalo alitakiwa agombee badala ya Kahama, lakini baadaye msamaria mwema alimpa taarifa kwamba jimbo hilo ni halipo.

Lembeli katika mahojiano yake maalumu na gazeti hili mjini Dodoma alisema alipewa taarifa hizo saa chache kabla ya muda wa mwisho wa kurudisha fomu za kugombea ubunge na kwamba tukio hilo lilimfanya afute fomu yake ya kugombea mara mbili.

“Ulikuwa ni uhuni na ufisadi wa hali ya juu kisiasa,” alisema mwanahabari huyo wa zamani katika mahojiano hayo maalumu yaliyofanyika mjini Dodoma mapema wiki iliyopita.

Alisema mara ya kwanza alijaza kwamba anagombea Jimbo la Kahama lakini alifuta na kuandika jimbo la Ushetu baada ya kupewa taarifa za kuanzishwa kwa jimbo hilo na baadaye alifuta Ushetu na kuandika tena Kahama baada ya kugundua kuwa ulikuwa mchezo mchafu.

“Baada ya kuruka viunzi, viongozi waandamizi wa CCM wa Shinyanga, akiwamo Mwenyekiti wa Mkoa, Hamisi Mgeja walisusa kunifanyia kampeni,” aliongeza Lembeli ambaye aliibuka na ushindi wa asilimia 54.5 kati ya kura zilizopigwa.

Alisema mpango huo wa kumhujumu ulianza mapema pale baadhi ya viongozi walipokuwa wakieneza kwamba yeye (Lembeli) hatakiwi na kwamba ukweli siyo kwamba alikuwa hatakiwi na wananchi bali baadhi ya viongozi.

Hata hivyo, Makamba alipoulizwa alisema ni uzushi kwa kuwa kazi ya kugawa majimbo ni ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, CCM kazi yake ni kusimamisha tu wagombea.

“Niacheni nipumzike niendelee kula pensheni yangu. Sasa niko Bumbuli natoka kuswali na ninakwenda kula Iddi, niacheni nipumzike jamani, kama kuna maswali zaidi aulizwe katibu mkuu wa sasa,” alisema Makamba.

Hata hivyo, Lembeni katika mahojiano hayo alisisitiza: “Ninachodhani walikaa chini na mambo haya yalifanyika Dar es Salaam na mbaya zaidi katika ofisi ya Makao Makuu ya CCM kwa sababu ndio walioleta taarifa.”

chanzo Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates