...kuajiri dereva, kufanya manunuzi ya nguo za thamani kwa ajili yake ya mkewe, kutafuta nyumba ya kifahari ya kupanga maeneo ya Mikocheni.
“Mpenziiiii!” Galos aliita, Rita akageuka kuangalia.
“Hee!”
Rita alipayuka kwa mshangao, kumwona Galos katika hali tofauti kabisa na aliyoondoka nayo asubuhi. Alikuwa ameng’ara, uzuri wa sura yake ambayo kwa muda mrefu ulikuwa umefunikwa na umaskini mkubwa sasa ulikuwa umechomoza na kumfanya Galos awe kama ambavyo Rita alimwona siku za mwanzo wa uhusiano wao.
“Galos!” aliita akimkimbilia.
“Yes baby.”
“Nini kimekutokea wewe mwanaume?”
“Mungu ametuona.” Aliitikia Galos akimkumbatia mkewe.
“Si umeondoka hapa asubuhi ukiwa na nguo zako?”
“Ndiyo.”
“Sasa?”
“Wewe acha tu, nitakueleza baadaye, twende zetu!”
“Wapi?”
“Tunahama.”
“Kwenda wapi?”
“Mikocheni.”
“Mh! Mbona ghafla hivi?”
“Punguza maswali mke wangu, ze taimu tu-tesa iz nao!” aliongea Galos akichanganya na Kiingereza kibovu kuthibitisha lile lisemwalo kwamba, ukitaka kumgundua mwanadamu tabia yake, mpe fedha! Tayari Galos alishaanza kuonyesha mikogo ya mafanikio kwa kujaribu kuongea Kiingereza.
“Niache basi hata nikachukue vitu vyangu.”
“Vitu gani? Una vitu humo ndani au takataka? Sitaki uingie humo, kilichomo atachukuwa atakayetaka.”
Rita hakuwa na la kusema, akiwa katika mshangao huo huo aliingia ndani ya gari baada ya Galos kumfungulia mlango, kichwani mwake alikuwa na maswali mengi mno yaliyohitaji kujibiwa na mume wake.
Gari likaanza kuondoka, Rita akibubujikwa na machozi si ya huzuni bali furaha, kila kitu kwake kilionekana ni ndoto na kwamba muda si mrefu angezinduka na kujikuta amelala kwenda kitanda chao cha mbao kisicho na godoro bali jamvi.
“Tunaelekea wapi?”
“Wewe twende”
Dereva akaendesha gari kwa mwendo wa taratibu, Galos na Rita wakiwa wemeketi kiti cha nyuma, kwa mara ya kwanza maishani mwake Rita akimshuhudia mumewe akimfanyia mambo ambayo aliwahi kuyaona kwenye sinema za Kihindi, hakuamini kama ni Galos aliyekuwa akifanya mambo hayo, gari likasimama mbele ya jumba kubwa la kifahari.
“Tumefika.”
“Kwa nani hapa?”
“Kwetu.”
“Kwetuuu? Mbona unazidi kunichanganya mume wangu? Au umejiunga na…”
“Nini?”
“Fre…ma…!”
“Ah wapi, hapa bongo kila mtu akifanikiwa maishani anaambiwa amejiunga na Freemason,” Galos aliongea akifungua mlango wa mbele ya nyumba.
Macho ya Rita yalionyesha mshangao mkubwa alipoitazama sebule, ilikuwa nzuri mno, yenye samani za thamani kubwa ambazo hakika hakuwahi kuziona maishani mwake.
Galos akamsaidia kuketi kwenye moja ya makochi makubwa ya sufi nyeupe, mbele yake kukiwa na runinga ya nchi sabini na mbili.
“Unataka chaneli gani mpenzi?” Galos aliuliza akiwa ameshikilia rimoti mkononi mwake.
“Galos acha utani, hebu nieleze umepata wapi fedha za kufanya mambo yote haya?”
“Madini.”
“Madini? Umeanza lini biashara ya madini mume wangu?”
“Nilikutana na watu wakanifundisha, kwa mara ya kwanza tukapata kipande kikubwa cha Almasi ambacho tumekiuza na kupata kiasi kikubwa cha fedha, ndiyo maana tuko hapa, punguza maswali mke wangu, huu ni wakati wa wewe kula bata badala ya kugeuza nyumba yetu Bunge la Katiba.”
Rita alikuwa akilia kwa furaha, alipopelekwa chumbani ndiyo alichanganyikiwa kabisa, kulikuwa na kitanda pamoja na kabati iliyoundwa kwa miundo ya Kiarabu, kiyoyozi kikiwa kazini, hakika yalikuwa mabadiliko ya haraka mno ambayo hakuyatarajia jana yake wakati anaingia kitandani kulala kwenye kibanda chao cha mbavu za mbwa.
“Hii siyo ndoto kweli?” alimuuliza Galos.
“Subiri kama ni ndoto utaamka!” Galos aliitikia huku akicheka.
Usiku wa siku hiyo hata tendo la ndoa lilikuwa tofauti na siku nyingine zote, waligundua kumbe joto la uswahili liliwasumbua sana.
Kila mtu alikiri mwenzake alikuwa mtaalam wakati walikuwa ni watu walewale, ingawa mioyo yao ilikuwa imejawa furaha na kuridhika, wote kwa pamoja wakakubali penzi bila mawazo kichwani, lilikuwa zuri na la kuvutia.
Hayo ndiyo yakawa maisha yao, mara kwa mara Galos akawa analetewa na majini kipande cha Almasi na kwenda kuuza, fedha zilizopatikana alizitumia kununua nyumba na magari ya kifahari, watu wote wakakiri kwamba “tajiri mpya” alikuwa ameingia mjini, ambaye chanzo chake cha mapato hakikueleweka vizuri lakini ndiye aliyeendesha magari ya kifahari kuliko mtu mwingine yeyote.
Ndani ya miaka miwili ya mafanikio hayo, uani kwa Galos kulikuwa na Ferarri mbili, Buggatti moja, Range rover mbili na Lamborghini moja ambayo alipenda sana kuitumia mwishoni mwa wiki, mke wake akiendesha Buggatti! Kila mtu alimzungumzia Galos, maana kwa watu wengi waishio mjini hasa katika nchi za Kiafrika utajiri wa mtu ni gari analoliendesha, ndiyo vijana wengi huwa radhi wakati mwingine kuendesha gari la mamilioni ya fedha, lakini wakiwa wamepanga chumba kimoja uswahilini.
Pamoja na maisha hayo ya kifahari Rita hakumwacha Mungu wake, bado aliamini kulikuwa na jambo lisilo la kawaida nyuma ya mafanikio ya mume wake, alikuwa mtu wa kanisani mara tatu kwa wiki, mara nyingi akifunga na kuomba ili Mungu amsaidie. Kadiri siku zilivyozidi kusonga ndiyo amani moyoni mwake ilivyozidi kutoweka, hasa pale alipojaribu kumdadisi mume wake juu ya utajiri waliokuwa nao, lakini akaishia kuambiwa “tulia kula bata.”
Kwa miaka mitatu Galos hakuwahi kwenda tena kwenye ulimwengu wa wachawi, kiasi cha kuanza kuhisi kwamba huenda mchezo huo ulikuwa umekwisha, wachawi waliachana naye ili afaidi utajiri. Katikati ya mwaka huo wa tatu, Galos akiwa usingizini, alijikuta tena mbele ya Mukulungu kwenye sherehe ya wachawi chini ya mti mkubwa wa Mbuyu, kila mtu akiwa utupu.
“Enheee Galos!”
“Ndiyo Mukulungu.”
“Umeona raha ya kuwa na utajiri?”
“Ndiyo Mukulu.”
“Sasa nataka kuuchukuwa utajiri wangu, urejee kwenye maisha yako ya zamani.”
“Kwa nini?”
“Imetosha tu,”
“Tafadhali usifanye hivyo, watu watanicheka, heshima yangu itapotea.”
“Nitauacha tu kama utatimiza sharti langu.”
“Lipi tena?”
“Nataka damu ya mkeo!”
“Mke wangu?”
“Ndiyo, umtoe kafara, wazee wanywe damu, nenda kafikirie, kesho utakuja kunipa jibu.”
Galos akainamisha kichwa na kuanza kulia, alikuwa njia panda, ghafla akazinduka usingizini na kumkuta mkewe akimtingisha na kumbembeleza aache kulia.
“Mbona umelia sana? Ndoto gani hiyo?”
itaendelea
No comments:
Post a Comment