WAFUATILIAJI wengi wa masuala ya siasa wameandika uchambuzi wao kuhusu matokeo ya Kura ya Maoni ya Scotland, nchini Uingereza. Wengi wamelinganisha hali ya kisiasa ya Muungano wa Uingereza na Muungano wa Tanzania na wengine kutaka fursa waliyopewa Waskochi pia itolewe nchini.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wamechanganya wakidhani Uskochi ndio Tanganyika na hivyo wakitaka Tanganyika ipewe nafasi ya kuamua kama wanautaka Muungano. Baadhi wamepatia kwa kuona Uskochi kama Zanzibar na hivyo kutaka Wazanzibari waulizwe kama wanataka kuendelea na Muungano wake wa sasa na Tanzania Bara.
Majadiliano makali kuhusu Muungano nchini Tanzania kiukweli yapo mbali sana kwa viwango vyote tofauti na majadiliano yaliyopo nchini Uingereza. Mjadala mkubwa hapa Tanzania ni Muundo wa Muungano, ama Serikali Moja, Mbili au Tatu.
Nchini Uingereza, kabla ya kura ya maoni, mjadala ulikuwa ni kama Taifa la Uskochi liendelee kuwa ndani ya Muungano au hapana. Uingereza inaundwa na Mataifa matatu ya Uskochi, England na Wales. Ukijumuisha na Ireland ya Kaskazini ndio unapata kinachoitwa Falme ya Uingereza (United Kingdom). Hivyo, Kura ya Maoni ilihusu Taifa moja tu na wamepiga kura kukataa kutoka nje ya Muungano wao.
Matokeo ya kura ya maoni sasa yamefikisha mjadala wa Uingereza kwa viwango vya Tanzania. Suala la Uingereza limeanza kuchukua mjadala mkali sana kiasi cha kuibua hisia za uzalendo wa Kiingereza. Tofauti na Tanzania ambapo viongozi wakuu wengi wa Serikali wanataka muundo wa Muungano wenye Bunge moja la Muungano, Waziri Mkuu wa UK ndiye aliyefungua mjadala wa nafasi ya England katika kutoa madaraka ya ndani kwa Uskochi na baadaye Wales na Ireland.
Akihutubia nchi yake saa chache baada ya matokeo ya kura ya maoni, Waziri Mkuu huyo alisema kuwa suala la mamlaka zaidi wa Uskochi ni lazima liende sambamba na nafasi ya England katika Muungano. Kwamba miswada ya sheria inayopitishwa katika Bunge la Uingereza na inayohusu masuala ya England ipigiwe kura na wabunge kutoka England tu. Hivi sasa wabunge kutoka Uskochi wanapiga kura kwa masuala yanayohusu Uingereza pia.
Nilipomsikia Waziri Mkuu Cameron anaongea hivyo, nikajisema mbona kama namsikia Job Ndugai ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndugai ni muumini wa kwamba hata kama tunabakia na Bunge moja la Muungano, basi wabunge kutoka Zanzibar wasiruhusiwe kupiga kura kwenye mambo yanayohusu Tanganyika tu. Suala hili limeleta mzozo mkubwa kwenye kamati za Bunge Maalumu la Katiba (BMK) linaloendelea mjini Dodoma hivi sasa.
Sasa England leo inajadili kama kama Tanganyika. Kwamba iweje wao wawe hawana Bunge? Siku si nyingi wataanza kuhoji iweje wao hawana Serikali? Kama ilivyo Tanzania, masuala yote yanayohusu England yanashughulikiwa na Serikali ya Muungano wakati Uskochi wana uhuru na masuala yao kama Elimu, Afya na Hifadhi ya Jamii kwa kiwango fulani.
England) inaunda asilimia 84 ya watu wote wa Uingereza na ndio yenye eneo kubwa kuliko mataifa mengine yanayounda Muungano huo. Wasiwasi mkubwa wa wachambuzi wa mambo ni kwamba iwapo England itakuwa na Bunge lake, basi Bunge la Muungano halitakuwa na kazi. Jarida la The Economist linaandika “ kukiwa na asasi za England kama Bunge na hatimaye Serikali, Muungano hautakuwa endelevu. Sehemu kubwa ya Muungano itafunika maeneo mengine na hatimaye Muungano kufa”.
Haya ndio maoni ya wasiotaka Serikali tatu hapa Tanzania pia. Kwamba liTanganyika likubwa, litaumeza Muungano na hatimaye kuuvunja. Waingereza wamepata woga. Kura ya maoni haijamaliza tatizo bali imelikuza.
Cameron itabidi afanye ziara Tanzania azungumze na mwenzake Rais Jakaya Kikwete labda atakuwa na la kujifunza. Kikwete naye atajifunza kwa Cameron kwa kuita kura ya maoni ya pande zote mbili za Muungano na si Zanzibar peke yake maana utaifa wa Utanganyika umeanza kuota mizizi.
Uingereza ina changamoto kubwa ya kisiasa hivyo vyama vya siasa vinatoa majawabu yenye kulinda maslahi yao ya kisiasa. Hii pia inatokea sana Tanzania. Wakati Tume ya Katiba inaundwa na hata baada ya kufanya kazi, baadhi ya wabunge wanaounda kundi la UKAWA hivi sasa waliishambulia sana Tume na wajumbe wake kiasi hata cha kuhoji ‘kwanini Bajeti ya Tume ina fungu la kuzuia Ukimwi’.
Hii ilitokana na sababu kuwa wabunge hawa walikuwa na mashaka kwamba taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba itaungana na msimamo wa CCM. Baada ya Rasimu kutoka, waliokuwa wanaitukana Tume ndio mashabiki wakubwa wa Tume na waliokuwa wanaitetea Tume ndio wanaitukana Tume kwa sababu maslahi yameguswa.
Cameron anataka suala la wabunge wa England tu kupitisha sheria za England kwa sababu chama chake cha Conservatives kina mbunge mmoja tu Uskochi. Kiongozi wa chama cha Labour Ed Miliband anapinga mapendekezo ya Cameron kwa sababu iwapo yakipita chama chake kitasahau kuongoza UK maana kinategemea wabunge kutoka Uskochi ili kupata wingi wa Wabunge katika Bunge la Makabwela (House of Commons).
Hata hivyo baadhi ya Wanachama wa chama cha Conservatives na chama kidogo cha English Democrats wanapendekeza Shirikisho kwa kuanzisha Bunge la England na House of Commons ibakie na masuala kama Mambo ya Nje, Usalama na Miundombinu.
Mwanazuoni Robert Hazell wa Chuo Kikuu kishiriki cha London anajenga hoja kwamba “Shirikisho lenye mshirika mmoja mwenye nguvu zaidi ya wengine haliwezi kudumu”. Anasema duniani kote imekuwa hivyo. Mifano ni kama West Indies (Jamaica), Yugoslavia na USSR (Russia).
Katika kujibu changamoto hiyo ya Shirikisho lenye mshirika mkubwa zaidi, Chama cha Labour kinapendekeza kuwa England igawanywe kwenye mikoa na kutoa mamlaka kwa mikoa kujiendesha kama ilivyo kwa Uskochi. Wazo hili kwa hapa Tanzania lilikataliwa na Tume ya Warioba. Ninaamini ni moja ya wazo mwafaka sana kama litafanyiwa kazi vizuri.
Kwamba Tanzania iwe ni Shirikisho lenye Serikali za Mikoa zenye mamlaka fulani fulani kama Elimu, Afya na baadhi ya kodi. Ujerumani iliamua kuchukua njia hii baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia na baada ya kuporomoka kwa Prussia.
Labda wao waliweza kwa sababu Katiba ya Ujerumani iliandikwa na wataalamu na si wanasiasa. Katiba ya Tanzania inaandikwa na wanasiasa. Uingereza wanapaswa wafuate njia ya Wajerumani inaweza kuwasaidia kujibu ‘The English Question”.
No comments:
Post a Comment