“Mango...” akaita.
“Ndiyo Mkuu.”
“Peleka eneo la tukio!”
Nihisi mwili ukiniisha nguvu! Mango na Ngoma wakanishika juujuu, kisha wakaanza kutembea kunipeleka nisipopajua!
SASA ENDELEA...
HAIKUWA safari ndefu sana. Tuliishia kwenye chumba kimoja kidogo chenye giza kali sana. Nikabwagwa chini kama mzigo. Moyoni nilikuwa na maumivu makali, sikujua sababu ya kupewa mateso yale.
Walivyonitupa pale chini, kama walioambiana waliondoka kwa pamoja na kuniacha peke yangu nikiugulia maumivu makali. Ghafla nilihisi wadudu wakianza kunitembelea mwilini mwangu.
Walikuwa wadudu ambao niligundua haraka kuwa walikuwa siafu.
Waliniuma kwa kasi mwilini mwangu, siafu wale hawakuwa na huruma hata kidogo. Nilihisi mwili ukivimba. Nilipiga kelele lakini hakuna aliyetokea kunipa msaada wowote.
Baada ya muda kama robo saa hivi, mlango ulifunguliwa, mwanga hafifu ukaonekana. Mara baada ya mlango kufunguliwa, wale siafu wote waliondoka mwilini mwangu.
Kuna mtu mmoja aliingia peke yake, sikumjua ni nani.
“Galos,” mtu huyo aliita.
Sauti yake ilinifanya nimjue kuwa ni yule mzee aliyewaagiza akina Ngoma na Mango walipeleke kwenye kile chumba.
“Naam!”
“Unajisikiaje?”
“Naumia sana mzee. Kwa nini mnanitesa kiasi hiki?”
“Hujui?”
“Sijui kitu.”
“Nilikuuliza swali mara ya kwanza, kuwa unamfahamu Matima Mtimandole ukasema ndiyo, si ni sawa?”
“Ni kweli.”
“Hebu ngoja tupate mwanga kidogo, fumba macho yako haraka.”
Nikafumba.
“Haya fumbua.”
Nikafumbua.
Nilishangaa sana kukuta nipo kwenye chumba kingine kizuri tofauti na kile cha awali, hapakuwa na siafu tena wala chochote kibaya. Kifupi kilikuwa chumba kizuri kama cha kawaida cha kuishi watu.
“Hiki ni chumba changu cha mazungumzo na wageni. Huwa nawaingiza watu ninaowaheshimu tu, hivyo nawe nimekupa hii heshima, lakini ukinitibua utajuta,” akasema akinikazia macho.
Kilikuwa chumba kilichotandazwa zulia zuri jekundu la manyoya ya kuteleza. Chini kulikuwa na mito mbalimbali. Nikajiegemeza kwenye mto mmoja, nikiangalia uvimbe niliokuwa nao mwilini kutokana na kuumwa na wale siafu.
Ghafla nikiwa nimezubaa, aliingia msichana mmoja akiwa amebeba chano kilichokuwa na glasi mbili za juisi, akaweka moja mbele yangu kisha akapeleka nyingine kwa yule mzee.
“Karibuni kinywaji!” akasema yule msichana mrembo akitabasamu.
“Ahsante,” yule mzee akaitika.
Mimi nilibaki kimya, moyoni nilikuwa na woga wa hali ya juu. Yule mzee akachukua glasi yake na kuipeleka kinywani mwake. Akapiga funda moja kubwa kisha akairudisha glasi chini, akaniangalia.
“Kunywa!” alisema kwa kuamrisha.
Nikainua glasi na kuipeleka kinywani, nikanywa. Dah! Ilikuwa juisi yenye ladha tamu kuliko kawaida. Sikukumbuka ni lini au wapi nilipata kunywa juisi yenye ladha tamu kama ile.
Nikarudisha glasi chini huku nikijitahidi kuachia tabasamu la kulazimisha.
“Naitwa Mukulungu – Mkuu wa Wachawi. Walio chini yangu wamezoea kuniita Mkuu, nawe pia unatakiwa kuniita hivyo,” akasema.
Nikatingisha kichwa kukubaliana naye.
“Nataka kukusaidia.”
“Nitashukuru.”
“Kwanza nataka kukujulisha sababu ya wewe kuwa hapa. Marehemu baba yako Matima Mtimandole, alikuwa mwanachama wetu. Tulifanya naye kazi vizuri lakini mwisho alianza kuharibu masharti yetu.
“Nadhani unakumbuka kuwa mmefiwa mfululizo na ndugu zenu. Utakumbuka kuwa, baba yako ndiyo amekuwa wa mwisho kufariki na mara baada ya kufariki, utajiri wote ukapukutika.
“Ni sisi ndiyo tulifanya hivyo kwa sababu ya ubishi na ujuaji wa baba yako. Wewe umepata nafuu kwa sababu ni mtoto wa mwisho, ndiyo maana tukaamua kuchukua watoto wako.
“Mkeo anaweza kupata mimba na akajifungua kama haitakuwa ya kwako. Tunachotaka sisi ni kizazi chako chote. Tunataka ubaki peke yako kwenye mateso makali, ndiyo lengo letu,” alisema mfululizo akiniangalia.
Nilipigwa na butwaa.
Nilimkumbuka baba yangu, mama yangu na ndugu zangu waliofariki. Moyo wangu uliumia sana, maana nilibaki peke yangu kama jicho.
“Sitaki kukuambia maneno mengi, ila unatakiwa kujua kuwa, tunataka kukusaidia – tupo tayari kurudisha utajiri wa baba yako mikononi mwako,” akasema.
Sikujibu kitu.
“Unanielewa?” akauliza.
“Sijakuelewa vizuri.”
“Unataka kuendelea kuishi masikini?”
“Hapana.”
“Unataka mimba za mkeo ziendelee kuharibika?”
“Hapana.”
“Sasa kama ndivyo unatakiwa kuwa tayari kwa maelekezo yetu.”
“Maelekezo gani?”
“Unatakiwa kujiunga nasi, uwe kama alivyokuwa marehemu baba yako lakini lazima uwe makini na usivunje masharti yetu.”
“Ni nini?”
“Unatakiwa uingie kwenye chama chetu cha wachawi.”
“Mh!” niliguna.
“Paaaaaaa!” kitu kizito kilitua mgongoni mwangu.
“Pumbavu! Unadhani kuna kubembelezana hapa? Kwa nini unataka kutuzungusha? Au unataka kufa? Sawa...tutajua cha kufanya. Toweka!” Mkuu alisema kwa sauti ya ukali, yenye muungurumo mkali.
Nikapoteza fahamu.
***
Nilijikuta nipo nje ya chumba changu, mlangoni tena nikiwa nimeshika kitasa cha mlango wa chumba chetu. Bila kuelewa ilivyokuwa, nikajikuta nimefungua mlango. Nikaingia na kukutana na kitu cha ajabu sana. Damu zilikuwa zimetapakaa chumba kizima! Rita mke wangu kipenzi, alikuwa akigaragara kitandani!
Inaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment