Viongozi wa nchi za Afrika zilizoathirika na ugonjwa wa Ebola wanakutana leo na viongozi wa Umoja wa Mataifa,wa shirika la fedha duniani IMF na benki ya dunia kujadili kile kinachohitajika kukabiliana na ugonjwa huo
Rais wa Guinea Alpha Conde,Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na Ernest Bai Koroma wa Sierra Leone leo wanakutana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon,mkuu wa shirika la fedha duniani Christine Lagarde na Rais wa benki ya Dunia Jim Yong Kim.
Nchi hizo tatu za magharibi mwa Afrika zimeathirika vibaya na ugonjwa wa Ebola ambao umewaua takriban watu 3,900 na viongozi wa nchi hizo wametoa wito wa misaada zaidi kutolewa kwa nchi zao kwa kujengwa kwa vituo vya afya,vifaa vya kuvaliwa na wahudumu kujilinda dhidi ya kuambukizwa,fedha za kuwalipa wahudumu hao wa afya.
Marekani na Canada zachukua tahadhari
Mkutano huo unakuja huku Marekani na Canada zikitangaza kuwa zitaimarisha uchunguzi wa kimatibabu katika viwanja vikuu vya ndege unaowalenga abiria kutoka nchi za magharibi mwa Afrika zilizoathirika na Ebola.Naibu Waziri wa usalama wa ndani wa Marekani Alejandro Mayorkas amesema uchunguzi huo utajumuisha mambo kadhaa wa kadhaa
Hii ni baada ya raia wa Liberia Thomas Eric Duncan ambaye alisafiri kutoka Liberia yapata wiki mbili zilizopita akiwa ameambukizwa Ebola kuwasili mjini Dallas kufariki hapo jana baada ya kuugua kwa muda wa siku kumi na moja na kusababisha hofu jimboni Texas hofu kuwa visa zaidi vitaripotiwa baada ya kukutana na watu wengine katika jamii.
Hatua hiyo iliyochukuliwa na Marekani itaanza kutekelezwa Jumamosi hii huku waziri wa afya wa Canada Rona Ambrose akisema itabidi abiria kutoka nchi zilizoathirika na ugonjwa wa Ebola wafanyiwe uchunguzi wa kina zaidi katika viwanja vya ndege lakini hakusema hatua hiyo itaanza kutekelezwa lini.
Huko Uhispania, watu watano wamewekwa karantini na wengine kadhaa wanachunguzwa baada ya kutengamana na mhudumu wa afya aliyeambukizwa Ebola alipokuwa akiwahudumia wamisionari wawili walioletewa mjini Madrid kwa matibabu baada ya kuugua Ebola.
Nchi za magharibi pia zimeathirika
Huku maafisa nchini humo wakijaribu kuwatambua watu waliowasiliana na mhudumu huyo Teresa Romero,Waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ametaka kuwe na utulivu na kuahidi kutakuwa na uwazi kuhusu suala hilo.
Na hapa nchini Ujerumani, mgonjwa mwingine wa Ebola amewasili katika hospitali moja mjini Leipzig leo asubuhi. Mgonjwa huyo ni mfanyakazi wa umoja wa Mataifa kutoka Liberia na ni mgonjwa wa tatu kuletwa Ujerumani kwa matibabu.
Mwanamke mmoja raia wa Australia anafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu baada ya kupata homa baada ya kurejea kutoka Sierra Leone alikokuwa akiwahudumia wagonjwa wa virusi vya Ebola.
Uingereza nayo imetangaza inapanga kuwatuma wanajeshi 75,meli yenye vifaa vya matibabu na helikopta tatu nchini Sierra Leone.Wizara ya ulinzi ya Marekani pia imetangaza inawatuma wanajeshi 100 wa majini na ndege sita kuimarisha juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo nchini Liberia
chanzo dw.de
No comments:
Post a Comment