Social Icons

Monday, 6 October 2014

Kessy: Nimenusulika kupigwa na Wazanzibar mara mbili

Mbunge Ali Keissy akitolewa nje ya Ukumbi wa Bunge na walinzi. 


Dar es Salaam. Mbunge wa Nkasi Kaskazini mkoani Rukwa, Ally Keissy amesema kuwa katika uhai wake akiwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge la Katiba hawezi kusahau alivyonusurika kupata kipigo kutoka kwa wabunge wa Zanzibar.

Alizungumza hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyotaka kujua historia ya maisha yake kabla na baada ya kuwa mbunge, hali ya kisiasa na Mchakato wa Katiba ulivyokuwa.Keissy alisema kuwa alinusurika mara mbili kupigwa na wabunge hao, huku wakimtolea lugha za kejeli na matusi.

 “Kitu ambacho siwezi kukisahau nikiwa bungeni tangu mwaka 2010 mpaka sasa ni matukio mawili ya kutaka kupigwa. Moja ni katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na jingine katika Bunge Maalumu la Katiba; ...haya siwezi kuyasahau kamwe,” alisema mbunge huyo.

Keissy aliongeza: “Unajua unapokuwa bungeni, hakuna haja ya kuonyesha ubabe, unashindana kwa hoja na unajibiwa kwa hoja. Kama mimi nimetoa hoja, basi nanyi mjenge hoja kwa kunijibu, lakini kukimbilia kutaka kunipiga siyo suluhisho.”

Anakumbuka matukio hayo akieleza kuwa mosi ni lile lilitokea Mei 26 mwaka huu ambapo alinusurika kupigwa baada ya kutoa maneno yaliyodaiwa kuwa ya kashfa kwa wabunge wa Zanzibar wakati wa akichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

“Tukio la pili lililotokea mwezi uliopita (Septemba), wakati wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, nilinusurika kipigo baada ya kupinga Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano,”alisema Keissy.

Akichangia mjadala wa Katiba, mbunge huyo asiyeisha vituko alisema kuwa haiwezekani Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano kwa kuwa hakuchaguliwa na wananchi wa Tanzania Bara jambo lililozua tafrani bungeni.

Hata hivyo, Keissy alisema kuwa pamoja na matukio hayo na vitisho vingine, hatasita, wala kuogopa kusema analoamini kuwa ni kweli.

“Kamwe sitaogopa, nitaendelea kusema ukweli, nitaendelea kujenga hoja kwa kile ninachokifahamu na watu wanaotaka kunipinga wawe wakipinga kwa hoja, hapo nitakuwa tayari kuwasikiliza,”alisema.

Historia ya maisha yake

Keissy alizaliwa wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa 15-Oktoba-1954. Alihitimu darasa la nane, Sumbawanga Middle School mwaka 1965.

Baada ya kumaliza darasa la nane, alianza kufanya shughuli mbalimbali hasa biashara za magari ya kubeba mizigo, mabasi ya abiria na maduka ya kuuza bidhaa mbalimbali.

No comments:

 
 
Blogger Templates