Dar es Salaam. Siku moja baada ya Bunge Maalumu la Katiba kupitisha Katiba inayopendekezwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Katiba hiyo bado ina maswali mengi kuliko majibu, hasa katika muungano na mgombea binafsi.
Amesema licha ya Zanzibar kuridhia mambo kadhaa kuwekwa katika orodha ya mambo ya muungano, hali inaweza kuwa tofauti ukifikia wakati wa Zanzibar kubadili Katiba yao ili kuwezesha utekelezaji wa mabadiliko hayo.
Juzi Bunge hilo lilipitisha Katiba inayopendekezwa kwa tofauti ya kura mbili na kuhitimisha kwa sasa mchakato wa kuandika Katiba hadi mwaka 2016 ambapo litafanyika zoezi la upigaji wa kura ya maoni.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi jana, Jaji Warioba alisema, “Wasiwasi wangu ni juu ya muungano kwa sababu katika masharti ya mpito ni lazima Zanzibar ifanye marekebisho ya Katiba yake. Rasimu inayopendekezwa inasema Tanzania itakuwa nchi moja pamoja na madaraka ya rais kugawa nchi. Kwa maana hiyo lazima Katiba ya Zanzibar ibadilike.”
Alisema katika mambo ya muungano, Katiba inayopendekezwa imeliweka suala la kodi ambalo halikuwamo katika rasimu iliyotolewa na Tume ya Katiba, kusisitiza kuwa kitendo hicho hakitajibu swali la ‘Tanganyika kuvaa koti la Muungano’.
“Wameongeza kodi ya mapato, ushuru wa forodha na bidhaa katika mambo ya muungano. Maana yake ni kwamba kodi yote inayokusanywa, ikiwamo ya kutoka Zanzibar itaingizwa kwenye mfuko wa muungano,”alisema.
Aliongeza, “Wakati huo huo Zanzibar imepewa uwezo wa kusimamia mambo yake yenyewe na ili iweze kulitekeleza hilo ni lazima iwe na vyanzo vyake vya mapato. Sasa watasimamiaje wakati mapato yote yanaingia kwenye mfuko wa muungano.”
Alisema ili suala hilo liweze kutekelezwa ni lazima Zanzibar ibadili Katiba yake na kusisitiza kuwa utakapofika wakati wa kubadili Katiba ya Zanzibar, jambo hilo linaweza kukwama.
“Sioni kama Wazanzibar watakubali suala hili. Kama mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yatakwama, ni wazi kuwa Katiba inayopendekezwa haitatekelezeka. Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yanategemea maridhiano ya Wazanzibari wenyewe na kumbuka kuwa CUF na CCM wanavutana sana,” alisema Jaji Warioba.
Akifafanua hilo, alisema mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar lazima yapate theluthi mbili ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kusisitiza kuwa kwa mvutano wa vyama hivyo viwili visiwani Zanzibar, itakuwa kazi ngumu kupitisha jambo hilo.
“Katiba ya Zanzibar isipobadilishwa kero za muungano zinazozungumzwa zitaendelea. Kazi iliyopo sasa ni kufikiria maridhiano kuhusu muungano, lazima tuhakikishe Zanzibar imekubali kubadili katiba yake na kuridhia mapato yake kuingizwa katika mfuko wa muungano,” alisema.
Aliongeza, “Kama ambavyo Tanzania Bara waliitegemea Zanzibar kupitisha Katiba inayopendekezwa, ni lazima pia ihakikishe kuwa Zanzibar inakubali kubadili Katiba yake.”
No comments:
Post a Comment