Social Icons

Friday, 23 January 2015

Hadithi: Familia tata 1


NI saa moja na nusu usiku!
Nyumbani kwa mzee Linus, Nakasangwe, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ndani ya ua mkubwa wa nyumba yake, mapambo yamepambwa vya kutosha na wageni waalikwa wakianza kuingia.

Katika meza kubwa, pamoja na watu wengine, mzee Komba, jirani na rafiki yake wa muda mrefu, amekaa. Juddy mwenye umri wa miaka 23, mtoto wa pili wa mzee Linus alikuwa anafanyiwa sherehe ya kuagwa. 
Kesho yake asubuhi, alitarajiwa kupanda ndege kuelekea Uingereza masomoni baada ya kufanya vizuri katika miaka yake mitatu ya kusomea Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Familia ya Linus na Komba ni marafiki wa muda mrefu, urafiki wao una historia ndefu. Walifahamiana shuleni, walipokutana katika michezo ya umisseta miaka ya sabini, lakini walijikuta wakiwa karibu zaidi walipokutana Dar es Salaam kikazi, mwanzoni mwa miaka ya themanini.

Ingawa walifanya kazi ofisi tofauti, lakini walifanikiwa kupanga sehemu moja, Kigogo. Baadaye, Linus katika pitapita zake, akasikia kuhusu kuuzwa kwa viwanja eneo la Nakasangwe, pembezoni mwa Kiwanda cha saruji cha Wazo, Tegeta, Dar. Viliuzwa kwa bei rahisi, akamshawishi rafiki yake, wakanunua jirani na mara moja wakaanza kujenga!

Ingawa wote sasa ni wastaafu, lakini wamejenga makazi bora na familia zao zinaendelea vizuri, wote wakibarikiwa kuwa na watoto wanne kila mmoja. Familia zao ni zaidi ya marafiki, shughuli ya kila mmoja wao, ni shughuli ya wote. Ndiyo maana leo mzee Komba ni mgeni rasmi, mke wake, ndiye anawaongoza akina mama katika masuala ya mapishi na vijana wa pande zote mbili, ndiyo wasimamizi wakuu wa mambo ya muziki, burudani na usafiri.

Shamrashamra ni nyingi kweli katika mtaa huu, muziki unasikika kwa sauti ya chini lakini ya kupendeza, majirani na wageni wengine kutoka mbali wanaendelea kumiminika katika nyumba hii yenye eneo kubwa kwa ndani. 
Katika eneo la jukwaa, lililotayarishwa rasmi kwa ajili ya watu kucheza wakati wa burudani ukifika, mafundi walikuwa wanamalizia kufunga vyombo, huyu akijaribu kile na huyu akijaribu kile.

Juddy, licha ya kwamba ilikuwa ndiyo siku yake, naye alikuwepo uani hapo kuwapokea ndugu, jamaa na marafiki waliojitokeza kwenye shughuli hiyo.
Hadi ilipofika saa mbili na nusu za usiku, ukumbi ulionekana kujaa, kwani maeneo machache tu ndiyo yaliyoonekana kuhitaji watu. Juddy alishaingia ndani kubadili nguo na tayari alisharejea akiwa amekaa meza kuu.

Antony, kijana mwenye umri wa miaka 14, mtoto wa tatu wa mzee Komba, alionekana akiingia ndani ya nyumba ya mzee Linus akiwa amebeba mfuko mweusi wa rambo, ndani yake kukionekana kuwa na kitu kisichofahamika. Mama yake Juddy, aliyekuwa akitokea jikoni alimuona.

“Nini hicho Tonny?” alimuuliza Antony, ambaye alifahamika zaidi kifupi kama Tonny, kijana wa jirani yao.
“Mama, wee subiri, kuna sapraizi nataka kuifanya hapa,” alisema Tonny huku akielekea chooni.
Mama yake Juddy akaguna na kutikisa kichwa, kisha akasema: “Mambo ya watoto bwana…” huyoo akaenda zake uani kuungana na wageni wengine!

Tonny akaingia chooni, akaufungua mfuko wake wa rambo. Akatoa sanamu ya kishetani sehemu ya kichwa, akaitazama, akatabasamu. Akaijaribu kuivaa na kwenda kujiangalia kwenye kioo. Yes, alifanana na shetani kabisa!
“Sasa subiri uone moto wake hapo uani,” alijisemea kimoyomoyo, akafungua mlango na kutoka nje ya choo, akaanza kutembea taratibu kuelekea uani…!!!!

Nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua.


chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates