Ilipoishia wiki iliyopita..
Ni saa moja usiku.
Akachukua simu yake, akatafuta jina flani, akabonyeza, ikaanza kuita, wimbo mzuri wa Injili ukisikika!
“Kaka Festo mambo?” Asfat alizungumza.
Sasa endelea..“Aaah Asfat upo? Long time, niambie,” Festo, akiwa anarejea nyumbani kutoka kwenye mishemishe zake, aliipokea simu hiyo kwa mshangao mkubwa, ingawa kila mmoja alikuwa na namba ya mwenzake, lakini hawakuwahi kuwasiliana hata siku moja.
“Uko wapi, home?”
“Hapana ndo narudi, vipi?”
“Nataka tuonane, nina shida kidogo,”
“Wewe uko wapi?”“Niko home, tukutane basi kwa Mzee Mathias,” Asfat alisema na walipokubaliana akakata simu.
Hakukuwa na umbali mrefu kutoka nyumbani kwao hadi kwa Mzee Mathias, kama siyo kukingwa na nyumba kadhaa, mtu angeweza kupaza sauti na kusikika. Kulikuwa na baa moja kubwa na ukumbi maridadi, pia kulikuwa na michezo ya watoto, pool, televisheni kubwa iliyokuwa ikionyesha michezo mbalimbali ya soka la kimataifa.
Badala ya kuelekea nyumbani, Festo akaliongoza gari kuelekea eneo hilo, ambalo hata hivyo, ilikuwa ni uwanja wake wa nyumbani kwa vile kila disko la mwishoni mwa wiki, ilikuwa ni lazima ahudhurie na alifahamika vyema.
Mara tu baada ya kukata simu, Asfat aliinuka na kwenda kumuaga mama yake, akimwambia kwamba anakwenda kwa mzee Mathias kununua chips kwa vile hakujisikia kula ndizi na nyama zilizopikwa nyumbani.
Mama hakuwa na kinyongo, akamruhusu na kumuomba amchukulie kiroba cha konya, akidai alijisikia kama mafua kwa mbali na anadhani akinywa kinywaji hicho, atauondoa ugonjwa huo!
Festo alikuwa wa kwanza kufika kwa mzee Mathias, akalipaki gari vizuri na kuteremka, vijana wachache waliokuwepo eneo hilo, ambao wanamfahamu walimkaribisha kwa bashasha.
Akamwita mhudumu, akamtaka awape kiroba kimoja kimoja cha konya wale vijana wanne waliomzonga, mwenyewe akajiagizia mzinga mzima na kinywaji kisicho na kilevi.
“Vipi kaka Festo,” Asfat alimsemesha baada ya kuwasili na kuungana naye pale alipokaa, kijana huyo akaitika kwa kutingisha kichwa wakati akipeleka fundo la kinywaji kinywani kwa mkono wake wa kushoto, huku akimpa wa kulia kumsalimia!
Haraka, wahudumu wakitambua kuwa wale walikuwa ni kaka na dada, wakasogea kusikiliza nini ambacho msichana angetaka, naye aliagiza kilevi alichokipenda na kuomba aletewe chips kuku, kwani alikuwa anajisikia njaa.
“Niambie Asfat, Uingereza imekupenda sana, umeng’aa, bila shaka utarudi huko kufanya kazi,” Festo alimsemesha dada yake huku akimpa tabasamu la nguvu!
“Hata siendi, baridi kama nini Ulaya, watu hawajui tu wanakimbilia kwa sababu ya ushamba wao.
Mimi nitafanya kazi hapa hapa Bongo, ikibidi kutoka basi itakuwa Afrika, sitaki kabisa Ulaya, kwanza kodi kubwa sana, mshahara wote unaishia kwenye kodi,” Asfat alimwambia Festo.
“Halafu Wabongo bwana, sasa wewe hutaki ukatwe kodi, si ndo inasaidia matibabu na kwenye majanga, kwani mnavyosema sijui Ulaya mtu unatibiwa vizuri na watoto wanasoma bure elimu bora unadhani kwa nini, kwa sababu ya kodi. Huku hamtaki kukatwa kodi halafu mnalalamika huduma mbovu za jamii,” Festo alimchombeza Asfat.
“Kweli lakini kaka Festo unadhani, Ulaya unapiga simu ya dharura, dakika moja tu wamefika na huduma utadhani unalipia, kwa hilo lazima tuwasifu,” alisema msichana.Baada
ya stori mbili tatu za Ulaya na Bongo kutawala, hatimaye Asfat alibadili mazungumzo!“Kaka Festo nina shida kubwa na wewe na ndicho nilichokuitia,” Asfat alisema. Festo akabaki kimya, akiwa na hamu kubwa ya kusikia alichoitiwa, akatingisha kichwa kuashiria aendelee kuzungumza.
“Najisikia kukupenda, nataka uwe mpenzi wangu,” Asfat alisema, akiwa amemkazia sura Festo.
“Whaat?” Festo aliuliza kwa mshangao!
inaendelea
Chanzo Globalpublishers
No comments:
Post a Comment