Social Icons

Saturday, 24 January 2015

Hadithi: Familia tata. 2


Tonny alikuwa amevaa kinyago cha kishetani akiwa chooni katika nyumba ya mzee Linus, swahiba mkubwa wa familia yao nyumba ya pili. Akionekana kama shetani, alitoka na kuanza kutembea taratibu kuelekea uani kulikokuwa na shamrashamra za sherehe za kumuaga Juddy…

sasa Endelea...UDDY aliondoka meza kuu na kwenda katika jukwaa lililotayarishwa tayari kwa sherehe. Pale alipokaa, alisikia kama vile kuna mkwaruzo kwenye kipaza sauti, akasogea ili kumwelekeza fundi mitambo arekebishe kasoro hiyo.
Wageni wengine wote walikuwa tayari kwenye viti vyao na wahudumu waliifanya vizuri kazi yao, vinywaji mfululizo viliendelea kutolewa na stori za hapa na pale zikipamba moto miongoni mwa wageni.

Watoto wadogo waliokuwa wakicheza muziki wa msanii Mr Nice, uitwao Kidali Poo, ndiyo waliokuwa wa kwanza kumuona Tonny katika mavazi yake ya kishetani. Walipiga kelele kubwa na kukimbilia upande wa watu. Kelele zile ziliwashtua watu wote akiwemo Juddy aliyekuwa akizungumza na fundi mitambo, alipotazama mlangoni, akamuona mtu aliyeamini ni shetani…!

“Mamamaaaaaa,” Juddy alipiga kelele na kuanza kukimbia jukwaani. Akitafuta sehemu salama ya kukimbilia, kwa bahati mbaya akakanyaga waya, akaanguka na bila kutarajia, kichwa chake kikaenda kuangukia kwenye maungio ya nyaya za umeme!
Waya mmoja ukachomoka, ukaishia kwenye shingo yake. Ndani ya sekunde chache, mwili wake ukabadilika rangi….

Kelele za kukimbia kwa watoto na vijana  wengine zilidumu kwa muda kadhaa kabla Tonny hajavua kinyago kile na kuanza kucheka. Shughuli ilishaharibika. Wakati watu wanaanza kurejea katika hali ya kawaida, wakagundua mtu aliyelala kimya ametulia chini, pembeni ya jukwaa.

Ni Juddy!
Haraka watu wakakusanyika, wakaogopa kumsogelea. Fundi mitambo alijua kilichotokea. Akazima umeme wa jukwaani, akamsogelea na kumgusa, akawatazama watu kwa huzuni.
“Jamani tumbebe, mambo yameshaharibika,” alisema fundi mitambo.
“Hebu subiri, nini?” Mzee Komba aliuliza baada ya kubaini utulivu aliokuwa nao Juddy, moyoni mwake akajua mambo hayako sawa.

“Hebu watoto tokeni hapa, sogeeni kule,” alisema mzee huyo na watoto, wakiwa kimya, wakasogea pembeni. Mzee Linus akasogea, mama Juddy alikuwa amesimama mbali, mwili ukimtetemeka!
Mmoja kati ya wageni waalikwa alikuwa daktari, Dr Junior. Akasogea na kwenda kumgeuza Juddy, akamshika moyo, akaonyesha uso wa huzuni pia. Akatoa ishara ya kumbeba msichana huyo. Akabebwa na kupelekwa kwenye gari kwa safari ya kuelekea hospitalini.

Wakati magari yanafuatana kuelekea hospitali ili kupata uhakika wa nini kimetokea, wageni waliokuwa hapo wakaonekana wamejipanga makundi makundi, mama Juddy alikimbilia chumbani kwake kujifungia, akilia kwa uchungu.
“Sijui kama atapona, ”fundi mitambo aliwaambia watu waliomzunguka kutaka kujua nini kimetokea. “Alikanyaga waya wakati anakimbia, bahati mbaya alipoanguka akaangukia hapa, hizi nyaya zikachomoka moja ikamgusa mwilini na bahati mbaya akailalia,” alisema fundi huyo na kusababisha vilio kutoka kwa watu waliokusanyika eneo hilo.

Mzee Linus, Komba, Dr Junior na majirani wengine kadhaa walikuwa nje ya Hospitali ya IMTU, eneo la Mbezi jijini Dar es Salaam wakisubiri ripoti ya daktari, ingawa wote walitambua kwamba Juddy alishafariki. Hakuna aliyekuwa akisema chochote, wote walionekana kujiinamia kwa huzuni. Aliyekuwa na hali mbaya zaidi, alikuwa ni mzee Komba. Kijana wake ndiye aliyesababisha tafaruku yote, hakuelewa nini hatima yake.

Baada ya nusu saa, daktari wa hospitali hiyo aliyetambulika kwa jina la Rama, alitokea kwenye ukumbi waliokuwa wamejazana watu, akaomba wahusika wa karibu kumfuata ofisini kwake.
“Poleni sana, mpendwa wetu amefariki dunia. Inaonekana ameunguzwa vibaya na umeme, poleni sana,” Dk. Rama aliwaambia mzee Linus na mzee Komba waliokuwa wamekumbatia mikono vifuani mwao!


inaendelea

No comments:

 
 
Blogger Templates