Social Icons

Saturday, 24 January 2015

Hadithi: Familia tata. 3


...Juddy aliyeangukia katika nyaya za umeme wakati akikimbia kumuogopa mtu aliyekuwa amevaa kinyago.

Wakiwa hospitali, waliitwa ofisini kwa daktari kupewa matokeo ya uchunguzi wa Juddy na kuambiwa kuwa alikuwa amefariki dunia. 
Sasa Endelea...

Taarifa rasmi ya kifo cha Juddy ikatolewa kwa watu waliokuwepo pale uani nyumbani kwa mzee Linus. Vilio vikaongezeka na ghafla sherehe ikageuka na kuwa msiba mkubwa. Hata hivyo, vinywaji vilivyokuwa vimetayarishwa kwa ajili ya mnuso huo, vikaendelea kuteketea.

Mzee Linus, Komba na majirani wengine wakaingia ndani kuuchukua mwili wa Juddy hospitalini IMTU na safari ya kuupeleka katika Chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Mwananyamala ilianza.
Hospitalini Mwananyamala, mtu wa chumba cha maiti aliwapokea. Taratibu zikaanza kufanywa ili mwili huo uhifadhiwe.
“Poleni sana, marehemu amefariki katika mazingira gani?” aliwauliza. Dr. Junior akajitokeza na kumwelezea kwa kifupi kilichotokea.

“Aisee, sasa hii ni lazima tupate karatasi kutoka polisi kwa sababu hili ni tukio linaloweza kufananishwa na jinai,” mtu yule aliwaambia. 
Walitakiwa kwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi kilichopo karibu na eneo la tukio, jambo lililomaanisha walitakiwa kwenda kituo cha Wazo au Kawe.

Mzee Komba akachukua simu yake ya kiganjani, akabonyeza namba kadhaa na kuiweka sikioni. Upande wa pili ulipokea, naye akatoa maelezo mafupi ya tukio lao.

Akatoa ishara ya kumtaka mhudumu wa chumba cha maiti kusubiri. Dakika mbili baadaye, simu ya mezani ya chumba cha maiti iliita, mhudumu aliipokea. Alionekana akipewa maelekezo kwani muda wote alikuwa akiitikia ‘ndiyo’ huku akitikisa kichwa.
“Nimeambiwa niipokee maiti lakini nyinyi lazima muende mkapate karatasi ya Polisi na muilete hapa ili tuweze kuandikisha maelezo yake kama ulivyo utaratibu,” aliwaambia baada ya kumaliza kuzungumza na simu, iliyotoka kwa mganga mkuu wa hospitali hiyo.

Wote waliitikia na kusaidia kuihifadhi maiti katika jokofu. Kisha wakaondoka kuelekea Kawe ambako baada ya maelezo, walipewa askari mmoja na kuambiwa watakutana na wenzao wa Wazo tayari kwa safari ya kwenda eneo la tukio.
Saa nane za usiku msafara wa watu waliokwenda hospitalini uliwasili nyumbani kwa mzee Linus, wakiwa wameongozana na gari mbili za polisi aina ya Difenda.

Baada ya kuzungumza na wenyeji na kupata maelezo ya jinsi tukio hilo lilivyotokea, askari aliyeonekana kuwa kiongozi wao alisema.
“Yuko wapi kijana aliyesababisha hali hii?” 
Kwa mara ya kwanza watu wakamkumbuka Tonny, hakukuwa na yeyote aliyemfikiria.
“Tonny, Tonny…..” watu wakaanza kuliita jina lake, lakini hakuonekana.

“Ni lazima apatikane,” askari huyo alisema, hali iliyoanza kuzua hofu miongoni mwa waombelezaji waliojazana ndani ya nyumba hiyo.
Akatafutwa nyumba nzima hakuonekana, nyumbani kwa mzee Komba pia hakuwepo.
“Anaweza kuwa amekimbia?” askari huyo aliuliza tena na mzee Komba akasema hadhani kama kijana huyo anaweza kukimbia, hasa kutokana na udogo wa umri wake, haonekani kuelewa lolote.

Polisi wakaagiza kufunguliwa kwa vyumba vyote ndani ya nyumba ya mzee Komba. Wakaanza chumba cha wazazi, kisha watoto, stoo, jikoni na kila mahali, Tonny hakupatikana.
Wakafikia vyoo vya ndani, mlango ulionekana umefungwa kwa ndani. Wakagonga, wakaita haukufunguliwa wala kusikika sauti yoyote.

“Antony, Antony, fungua mlango, Antony!!!” Mzee Komba aliita kwa sauti huku akigonga kwa nguvu mlango, hakukuwa na majibu.
“Inabidi uvunjwe,” askari alisema. Mzee Komba akatikisa kichwa kukubali. Kazi hiyo ikafanyika, kitasa kikavunjwa na mara mlango ukawa wazi.
Tonny alionekana akiwa amelala sakafuni!!!!!!

Je, nini kimempata Tonny? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

No comments:

 
 
Blogger Templates