Lakini sifa yake kubwa ilikuwa ni tabia yake ya kuendesha magari kwa mwendo kasi. Hata kama alikuwa akienda sehemu ya karibu, alipenda kulikimbiza...
Sasa Endelea...
Mama yake Tonny alikuwa uani kwake akifua nguo za mtoto wake wa mwisho, Subby wakati akitaniana na kaka yake Tonny aliyeitwa Santo. Santo alikuwa akisoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Bunge na siku hiyo ya Jumamosi, hakwenda shule.
Mama Tonny alikuwa akimpenda sana Santo na mara nyingi walikuwa wakitaniana. Leo, wakiwa hapa, mama alikuwa akimshambulia Tonny kwamba ni lazima atafeli kwa sababu ya kupenda sana filamu. Na kweli, Santo alikuwa shabiki mkubwa wa filamu, hasa za Kizungu, ingawa pia alivutiwa na zile za Kihindi na Kibongo.
Baada ya kuzidiwa utani na mama yake, Santo akaamua kuondoka lakini akamvizia akiwa amejisahau, akamtekenya kwenye mbavu. Mama alipata mshtuko mkubwa na akiwa na hasira, aliinuka na kuanza kumfukuza kijana wake aliyekuwa anakimbilia nje ya geti!
***
Baptist alikuwa anakata kona maarufu mtaani kwao iitwayo Kwa Kipira, akiwa katika mwendo wa kasi kama kawaida yake. Mtaa ulikuwa kimya na hakukuwa na mtu barabarani. Akiwa anakaribia kwenye geti la nyumba ya Mzee Komba, ghafla akamuona mtu akitokeza kwa kasi na kuingia barabarani.
Hakuweza kujizuia, hakuweza kulizuia gari, kishindo kikubwa kikasikika na mtu mmoja alionekana akirushwa juu na alipoanguka chini, akabakia kuwa mtulivu pale chini alipofikia.
Alikuwa ni Santo!
Kishindo kile kilileta kelele kubwa mtaani na mara moja, kila mtu aliyekuwepo alitoka nje ya nyumba ili kushuhudia kilichotokea. Bap alifanikiwa kusimamisha gari mita chache mbele, akatoka nje ya gari na kumkimbilia mtu aliyemgonga!
Kishindo kile kilikuwa kama nyundo iliyopiga katika kichwa cha mama yake Tonny, alitambua kabisa kwamba aliyegongwa ni mtoto wake. Naye pasipo kutarajia alianguka na kupoteza fahamu muda uleule mwanaye alipogongwa.
Ndani ya dakika moja, watu wengi walijazana pale alipokuwa amelala Santo, mwili wake ulijaa damu na watu wakawa kama waliochanganyikiwa. Kwa muda wakawa hawajui wafanye nini hadi akili zilipowarejea.
Baptist alikuwa wa kwanza kumshika Santo, akamgeuza vizuri na kumtazama, akatoa ishara kwa wenzake wambebe, wakampakia kwenye gari alilomgonga nalo. Watu wengine wawili wakaingia ndani ya gari lile, kwa kasi ya ajabu, likaondoka kuelekea hospitalini!
Watu wengine nao mtaani wakawasha magari yao na kulifuatilia gari lililombeba Santo. Baptist aliendesha gari kwa kasi hadi alipofika katika Hospitali ya Mico iliyopo Tegeta Basihaya. Madaktari wakampokea haraka mgonjwa na moja kwa moja akapelekwa chumba cha upasuaji!
Nyumbani kwa akina Santo, baadhi ya majirani walishtuka baada ya kumuona mama yake Santo akiwa amelala chini, tena kwa namna ya kutisha. Walipomchunguza, wakagundua kwamba alikuwa amepoteza fahamu.
Wakamfanyia huduma ya kwanza, kisha wakambeba na kumwingiza ndani kwake. Alirejewa na fahamu baada ya nusu saa, akashangaa kuona watu wamemzunguka sebuleni alipolala kwenye kochi.
“Vipi?” aliwauliza wanawake wawili waliokuwa karibu yake, akiwemo mama yake Juddy.
“Tulia, tuliza akili kwanza, upo salama?” mama Juddy alimwambia mwenzake huku akimtengeneza vizuri kanga zake alizojifunga.
“Kuna nini kimetokea dada, niambie haraka,” mama yake Santo alimwambia mama Juddy huku akimshika mikono yake kwa nguvu kubwa.
“Tumekukuta umeanguka pale mlangoni kwako, ndiyo tukakubeba na kukuingiza ndani,” alijibiwa!
“Mnenikuta nimeanguka?” aliuliza tena na kuanza kuvuta kumbukumbu.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii katika toleo lijalo.

No comments:
Post a Comment