Social Icons

Sunday, 25 January 2015

Hadithi: Familia tata - 7


“Tumekukuta umeanguka pale mlangoni kwako, ndiyo tukakubeba na kukuingiza ndani,” alijibiwa!
“Mmenikuta nimeanguka?” aliuliza tena na kuanza kuvuta kumbukumbu…!!!
Sasa endelea...

Baada ya kumfikisha hospitalini alikopokelewa, Baptist akachukua simu yake na kumpigia baba yake mzazi, mzee Linus.
“Shikamoo baba,” Baptist aliongea mara tu ilipopokelewa.
“Marahaba, tunakaribia hapa hospitali, vipi hali yake,” mzee Linus alijibu, kauli ambayo ilimshangaza sana Baptist, hakutegemea kama mzee wake alishataarifiwa. Ukweli ni kwamba mama yake, alimpigia simu na kumweleza kilichotokea mara tu walipoondoka nyumbani kuelekea hospitali.

Naye mzee Linus aliwasiliana na rafiki yake. Bahati nzuri, mzee Komba alikuwa Bahari Beach Hotel alikokuwa na kikao cha kikazi na washirika wake kibiashara, wakati mzee Linus alikuwa akirejea kutoka shambani kwake Mapinga, alikuwa akikaribia Bunju, njia ya kuelekea Bagamoyo!
Wakakubaliana kukutana hospitali.

***
Mama Tonny alivuta kumbukumbu zake vizuri akiwa amejiinamia chini. Kwa mbali akakumbuka kuhusu kilichotokea. Kishindo cha kugongwa na gari mtoto wake kikajirudia tena akilini mwake, akapiga ukulele..
“Mamaaaaaa!”
Watu wote waliokuwa sebuleni hapo wakashtuka, mama yake Juddy akawahi kumshika mkono na kumtuliza.
“Vipi mwenzangu?” aliuliza

“Santoo, Santooo, mwanangu Santooo jamani,” mama Tonny alianza kuangua kilio, Mama Juddy akamshika vizuri na kumtuliza, akazidi kupiga kelele na kuuliza alipo mwanae.
“Amepelekwa hospitali.”  
“Wamempeleka yeye au maiti yake?” aliuliza huku akiuma meno kwa uchungu, hakuamini kama mwanae alikuwa mzima.
“Mzima kabisa dada, wala usiogope,” mama Juddy alijitahidi kumfariji.

“Nataka kwenda, nataka kwenda, sasa hivi,” alisema na kuinuka, wanawake wenzake walijaribu kumzuia, lakini akawashinda nguvu, asijue hospitali waliyokwenda, akatoka nje ya geti na kuanza kutimua mbio akiwa pekupeku bila viatu. 
Bahati nzuri kulikuwa na vijana wa kiume mtaani hapo ambao bado walikuwa katika vikundi wakijadili tukio hilo, wakaambiwa wamkamate asije kupata madhara zaidi.

Zoezi lile halikuwa kubwa, vijana kadhaa wenye ubavu walimkimbiza mama kidogo, na kumkamata na kumsihi atulie, kwani tayari akina baba walikuwa wameshafika hospitalini, na taarifa zilizoletwa muda huo zilisema Santo alikuwa bado chumba cha upasuaji.
Kwa unyonge mama akakubali kurudi nyumbani, lakini akiwa anatoa kilio kikubwa. Vijana wale walimuongoza nyumbani wakijaribu kumpa matumaini.

***
Baptist aliwafuata mzee Komba na baba yake waliokuwa wamekaa kwenye benchi wakizungumza kwa huzuni.
“Inabidi niende polisi kutoa taarifa za ajali,” aliwaambia huku naye akionekana kuwa mwenye huzuni kubwa.
“Sawa, nenda kituo cha Wazo, halafu kitakachotokea utatuambia,” alisema mzee Linus.

Baptist akaendesha gari kwa kasi kama kawaida yake hadi Kituo Kidogo cha Polisi Wazo. Alijua haitakuwa rahisi kutoka wakati ule, akatafuta sehemu nzuri na kuegesha, akasogea kaunta ya polisi na kueleza tatizo lake kwa askari aliyekuwa zamu.
“Zunguka, vua viatu, saa, mkanda, afande, mfungulie mlango huyu, kaua,” askari aliyekuwepo kaunta alisema kwa sauti kubwa, hali iliyosababisha watu wote waliokuwa jirani kumtazama Baptist aliyekuwa sasa anazunguka kuingia kaunta.

“Kwani imekuaje?” alisema askari mwingine aliyekuwa ndani, ambaye alionekana kama ndiye mkubwa, kuliko yule aliyekaa kaunta. Akataka kijana yule aingie ofisini kwake.
Baptist akaingia, akakisogelea kiti kilichokuwa kinatazamana na kile cha ofisa wa polisi, akakaa. Ofisa huyo akataka kupata maelezo ya nini hasa kimetokea.

Baptist akamuelezea kuanzia mwanzo hadi mwisho. Askari akatingisha kichwa. Akachukua mkono wa simu ya mezani, akabonyeza namba kadhaa kisha akauweka sikioni.

itaendelea

No comments:

 
 
Blogger Templates