Social Icons

Saturday, 21 February 2015

Ajenda 10 za mrithi wa JK


Dar es Salaam. Wakati mjadala wa majina ya watu wanaotaka kuwania urais umepamba moto, baadhi ya wasomi, wachambuzi na wasomaji wa gazeti hili wamesema badala ya kukimbilia majina, wagombea hao wanatakiwa kueleza jinsi gani watakavyokabiliana na ajenda 10 muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Ajenda hizo kwa mujibu wa wadau wa kada mbalimbali walioongea na Mwananchi kuhusu vipaumbele vya taifa kwa sasa, ni tatizo la ajira, changamoto za kuinua kilimo, kutoa elimu bora, kusimamia makusanyo ya kodi, rasilimali za taifa na kuboresha miundombinu ya usafiri.

Wagombea hao pia watatakiwa kueleza jinsi watakavyoondoa migogoro ya wakulima na wafugaji, matumizi sahihi ya ardhi, mapambano dhidi ya rushwa, uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya, kwa mujibu wa marejeo ya habari mbalimbali yaliyofanywa na gazeti la Mwananchi.

Kwa kawaida, vyama vya siasa huandaa ilani zake za uchaguzi ambazo ndiyo mwongozo wa kampeni za kutafuta kura kwa wananchi kwa ajili ya wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani, lakini watatakiwa kuzingatia hoja hizo muhimu.

Katika mahojiano na wadau mbalimbali, gazeti la Mwananchi lilitaka kujua ni mambo gani ambayo wananchi “wanataka yawe ajenda kuu kwenye kampeni za uchaguzi ili kuikwamua nchi” kutoka hapa ilipo, na majibu yao yalionyesha suala la ajira, kilimo, afya, rasilimali za taifa, usafiri, maji, rushwa na migogoro ya ardhi kuwa ndiyo mambo ambayo hayajafanyiwa kazi na hivyo wanataka kusikia wagombea watakavyokabiliana nayo.

“Kwanza tunahitaji utawala bora unaosimamia haki, Serikali inayofanya uamuzi sahihi,” alisema mwanasheria wa jijini Dar es Salaam, Felix Kibodya kabla ya kutaja mambo ambayo anaona yanafaa kupewa kipaumbele.

Usimamizi wa rasilimali

Kibodya, ambaye amewahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alisema rasilimali zikisimamiwa na kutumika vizuri, zitalinufaisha Taifa kwa kiasi kikubwa.

“Kuna viongozi katika nchi hii waliwahi kueleza wazi kwamba rasilimali zikibaki ardhini haziozi. Tukifanya mchezo rasilimali hizi zitakwisha. Suala hili linaenda sambamba na ubinafsishaji tulioufanya miaka ya nyuma, sasa ndiyo tunaaza kuona ubaya wake,” alisema.

Alikuwa akizungumzia rasilimali kama dhahabu, chuma, shaba, platinum, nickel, almasi, tanzanite, rubi, garnet, emerald, sapphire na maliasili nyingine kama gesi na mafuta.

Kati ya madini hayo, dhahabu na almasi ndiyo zimekuwa tegemeo kubwa kwa uchumi wa Tanzania, wakati kugundulika kwa gesi na uwezekano wa kupatikana kwa mafuta kumeinua matarajio ya maisha bora kwa wananchi na wakati fulani Rais Jakaya Kikwete aliwahi kunukuliwa akisema “atakuwa Rais wa mwisho kuiacha nchi maskini”.

Lakini kilio kikubwa cha wadau imekuwa ni mikataba, ambayo imeelezwa kuwa ni ya siri na hainufaishi Taifa na badala yake inanufaisha wawekezaji na wajanja wachache.

“Hatuna sababu ya kukopa kwa mataifa tajiri wakati tuna rasilimali za kutuingizia fedha nyingi. Tukiweza kusimamia vizuri vivutio vya utalii, gesi, mafuta na madini tutapiga hatua kubwa,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Idara ya Sayansi ya Siasa, Richard Mbunda.

Mbunda alitaja mambo matatu yanayotakiwa kusimamiwa kwa umakini kuwa ni matumizi bora ya rasilimali, miundombinu na kilimo.

Claudian Mutayoba mkazi wa Kigoma alisema: “Jambo la muhimu ninaloliona wazi kuwa linaweza kutusaidia ni rasilimali tulizonazo. Kama Serikali itaweka mikakati madhubuti ya kuzisimamia zinaweza kutufikisha mbali. Hilo halifanyiki na ndiyo maana madini yanaibwa na wanyama kusafirishwa nje ya nchi.”

Ajira Kwa data zaidi bonyeza hapa

Tatizo la ajira limekuwa likizungumzwa na wengi, wakiwamo waliotangaza na wanaotajwa kuwania urais, wote wakielezea kuwa ni bomu linaloweza kuibuka wakati wote. Kwa sasa takriban watu milioni 21 ni nguvu kazi iliyoko sokoni na kati yao, milioni 6.5 tu ndiyo walio na ajira, wakati watu 800,000 hadi 1,000,000 wanaingia kwenye soko la ajira kila mwaka.

Idadi hiyo ya watu wanaostahili kuajiriwa ni kuanzia vijana wa miaka 15 ambao wakati wowote wanaingia sokoni kusaka ajira na kwa mujibu wa takwimu hizo za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) za mwaka 2012, idadi ya walio tayari kwenye soko la ajira ni takriban nusu ya idadi ya Watanzania.

“Maendeleo yanatakiwa kusimamiwa. Nchi yetu ina tatizo kubwa la ardhi na ajira. Tunatakiwa kujiuliza sababu za wanakijiji na mwekezaji kugombania ardhi. Iweje mwekezaji apewe ardhi na mwananchi ahamishwe,” alisema Profesa Penina Mlama, ambaye ni mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere.

“Tazama ajira. Ni tatizo kubwa ni vyema tukaweka utaratibu wa kila mwekezaji nchini kuajiri idadi fulani ya Watanzania, hiyo iwe lazima si ombi.”

Hoja hiyo iliungwa mkono na Tito Kisiya, mkazi wa jijini Dar es Salaam, ambaye alisema ajira ni ajenda namba moja.

“Kipaumbele namba moja ni ajira. Huwezi kukuza uchumi wa nchi kama rasilimali watu haitumiki inavyotakiwa. Pia, msisitizo mkubwa uwekwe katika viwanda kwa kujenga vipya, kufufua vilivyokuwapo ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisema akiungana na wengi waliozungumza na Mwananchi.

Desmund Mgongolwa pia alikuwa na maoni kama hayo aliposema: “Ajira zipewe kipaumbele. Kuna haja ya kuunda mfuko wa kukopesha vijana wasio na ajira ili waunde vikundi vya kufanya biashara.”

Suala la kuboresha kilimo ili kiwanufaishe wakulima pia lilikuwa midomoni mwa wengi na walisema kilimo sasa hakina usimamizi na hivyo kupoteza umuhimu wake.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanaishi vijijini ambako kilimo kilikuwa kikielezewa kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi, lakini katika siku za karibuni makundi ya vijana yamekuwa yakimiminika mijini na kujishughulisha na biashara ndogondogo kutokana na kilimo kuonekana kutokuwa na manufaa kiuchumi.

Kilimo kinachangia asilimia 27.8 ya Pato la Taifa kutokana na mazao ya pamba, kahawa, chai, tumbaku, katani na karanga wakati mazao ya chakula ni mahindi, maharage, viazi na mihogo.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alizungumzia zaidi suala la kilimo akihusisha na dhana ya soko huria.

“Dhana ya soko huria ndiyo sababu ya kilimo kutowanufaisha wananchi na kutochangia Pato la Taifa kama inavyotakiwa,” alisema.

Akizungumzia mambo yanayotakiwa kuwa ajenda kuu katika uchaguzi alisema ajenda ya kwanza ni kukuza uchumi ambao ukuaji wake utatokana na kuboreshwa kwa sekta ya kilimo na viwanda.

“Jambo la pili ni kutokomeza umaskini ambalo litakwenda sambamba na kumaliza tatizo la ajira. Tatu ni kutokemeza ufisadi na rushwa na nne kujenga misingi imara ya demokrasia,” alisema.

“Serikali imejiondoa katika kusimamia na kudhibiti uchumi na hali hii inatokea karibu kila sekta nchini. Mfano, mapato ya wakulima ni madogo, hawana soko la kueleweka na hata likiwapo bado wanapangiwa bei za kuuza mazao yao,” alisema.

Alisema barani Afrika Tanzania ni kati ya nchi ambazo zinategemea jembe la mkono kwa kilimo, jambo ambalo haliwezekani kulikuta nchi nyingine zinazoendelea.

“Tuna sera ya kilimo kwanza lakini haijasaidia kuinua kilimo. Kilimo kikifanywa vizuri ni chanzo kizuri cha mapato na hata kuliletea Taifa letu maendeleo, zipo nchi nyingi duniani zimeendelea kwa sababu tu ya kilimo,” alisema.

Elimu

Wakati Serikali imezindua Sera ya Elimu bora, wadau wanaona kuwa bado Serikali ya Awamu ya Tano itatakiwa kufanya kazi kubwa kuboresha elimu.

No comments:

 
 
Blogger Templates