Tanga. Vikosi vya majeshi vilivyokuwa vimeungana kukabiliana na tishio la majambazi katika Mapango ya Amboni, jijini Tanga vimekamilisha siku ya tatu za operesheni maalumu ya upekuzi ndani ya mapango hayo.
Hivi sasa askari wa majeshi mengine wameondoka katika pango hilo na kubaki wa polisi wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) ambao wataendelea kufanya doria eneo hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Freisser Kashai alisema wameamua kupunguza askari katika operesheni hiyo baada ya kujiridhisha na hali iliyopo sasa.
“Doria inaendelea kufanyika katika eneo hilo, lakini tumepunguza idadi ya askari ili waweze kwenda kufanya majukumu mengine,” alisema Kashai.
Kuhusu majeruhi (majina yanahifadhiwa), alisema askari wote watano wameruhusiwa kutoka hospitalini.
Wakati Kashai akitoa maelezo hayo, kamatakamata ya watu imeendelea kufanywa.
Kashai alithibitisha kukamatwa kwa baadhi ya watu na kwamba wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano
Utalii
Hali imezidi kuwa mbaya katika mapango ya utalii ya Amboni mkoani Tanga, baada ya tukio la mapigano ya kurushiana risasi baina ya majambazi na polisi lililotokea katika Kijiji cha Mleni kilometa tano kutoka katika vivutio hivyo vya utalii.
Akizungumza na waandishi wa Mwananchi juzi, Mhifadhi Msaidizi wa Mapango ya Amboni, Tabu Mtelekezo alisema tangu mashambulizi hayo yafanyike, hakuna wageni wanaofika eneo hilo kutokana na vyombo vya habari kupotosha eneo halisi lililokuwa na mapigano.
Mtelekezo alisema kwa wiki nzima sasa wamepata wageni 16 tu, idadi ambayo ndogo ikilinganishwa na wastani wa wageni 300 kabla ya tukio.
Chanzo: Mwananchi
 
 

 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment