Social Icons

Wednesday, 18 February 2015

Ghasia ndani ya Bunge la Afrika Kusini

Wachambuzi wa siasa za Afrika Kusini wamesema demokrasia nchini humo ndio mhanga mkuu wa vurugu zilizoibuka katika bunge la nchi hiyo wakati rais Jacob Zuma alipokuwa akijiandaa kutoa hotuba yake kuhusu hali ya nchi.

Wabunge wakuvutana mashati ndani ya bunge

Wabunge wakuvutana mashati ndani ya bunge

Usiku wa Alhamisi wabunge wa chama cha upinzani chenye siasa kali za mrengo wa kushoto waliivuruga hotuba hiyo ya rais, wakimtaka aeleze wazi namna atakavyolipa fedha za umma ambazo zilitumiwa kuyakarabati makazi yake binafsi.

''Ghasia bungeni ni ishara ya kuporomoka kwa demokrasia ya Afrika Kusini'' ndivyo lilivyosema gazeti la Business Day ambalo linaheshimika nchini humo. Gazeti hilo limeendelea kuandika kwamba vurugu za jana jioni ndani ya jengo la bunge na katika viwanja vyake, ambazo hata hazikufikirika miaka mitano iliyopita ni sababu tosha kwa Afrika Kusini kukaa chini na kutafakari jinsi taifa lilivyofikia hali hiyo.

Na gazeti hilo linaunyooshea kidole utawala wa rais Jacob Zuma kuwa kigezo muhimu katika kuchuja kwa demokrasia nchini humo.

Zuma asakamwa

Rais Jacob Zuma. Anatuhumiwa kutumia vibaya fedha za umma

Rais Jacob Zuma. Anatuhumiwa kutumia vibaya fedha za umma

Sokomoko lilitokea wakati rais Zuma alipokuwa akitoa hotuba yake kuhusu hali ya nchi, ikiwa mara ya kwanza kufanya hivyo baada ya kuchaguliwa tena kuiongoza nchi mwezi Mei mwaka jana. Alipokelewa kwa ghadhabu ya wabunge wa chama cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters, au, Wapiganaji wa Uhuru wa Kiuchumi, kwa kifupi, EFF. Chama hicho kinaongozwa na Julius Malema, mwanasiasa mwenye lugha kali ambaye zamani alikuwa mwenyekiti wa tawi la vijana wa chama tawala, ANC.

Wabunge hao walipaza sauti, wakimtaka aeleze ni lini atakapolipa dola milioni 23, fedha za umma ambazo zilitumika kuyakarabati makazi binafsi ya rais huyo. Mwendeshamashtaka wa serikali alikwishasema kwamba baadhi ya fedha hizo zilitumika kwa njia zisizo halali, na kumtaka rais Zuma kuzirejesha. Lakini rais huyo amesema hana kosa lolote.

Bunge lageuka ulingo wa masumbwi

Spika wa Bunge Baleka Mbete ambaye alionekana kukerwa na vitendo hivyo, alitishia kutumia nguvu za vyombo vya usalama kuwaondoa bungeni wabunge hao wa EFF, ikiwa hawatatulia. Kitisho hicho kilizusha urushianaji wa ngumi, ambao kwa mujibu wa mashahidi, uliwaacha watu kadhaa na majeraha.

Mshikemshike miongoni mwa waheshimiwa, demokrasia au otovu wa nidhamu?

Mshikemshike miongoni mwa waheshimiwa, demokrasia au otovu wa nidhamu?

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuburuzwa kutoka ndani ya bunge, huku nguo yake ikiwa imechanwa katika tafrani hizo, alisema walichokishuhudia ni sura ya nchi inayoendeshwa kwa mikwaju ya polisi.

Kufuatia ghasia hizo hata wabunge wa chama kingine cha upinzani cha Democratic Alliance, DA walitoka nje, wakilalamikia uamuzi wa spika kuwaingiza askari polisi ndani ya bunge.

Wachambuzi wengi kuhusu hali hiyo iliyojiri bungeni wamesema hali hiyo ilitokana na mwenendo wa bunge kuridhia matakwa ya serikali, bila kuzingatia umuhimu wa kuhakikisha mambo yanafanywa kwa uadilifu.

Wengine walikosoa hatua ya kuvuruga mawasiliano ya simu za mkononi ndani ya jengo la bunge wakati wa hotuba ya rais Zuma, ambako kuliwazuia waandishi wa habari kufanya kazi yao, kama uthibitisho wa namna serikali ya Afrika Kusini isivyojali uhuru wa vyombo vya habari.

Kifo cha demokrasia!

Mwandishi wa gazeti la uchambuzi la Daily Maverick alisema katika makala yake kwamba sehemu kubwa ya demokrasia ya Afrika Kusini ilikufa usiku wa Alhamisi, akisisitiza kuwa baada ya hapo, chama cha ANC hakiwezi tena kudai kuwa kinatawala kwa maslahi ya raia wote wa nchi.

''Hatua ile ya bunge kujaribu kulidhibiti bunge zima kwa manufaa ya chama kimoja, imewasukuma wengine wote katika upande wa uasi'', aliongeza mwandishi huyo, Stephen Grootes.

Katika mvutano huo lakini baina ya rais Zuma na chama cha EFF, hakuna anayeelekea kulegeza kamba. Mwenyekiti wa chama hicho, Julius Malema alesema baadaye kuwa jana ulikuwa ni mwanzo tu. ''Tutaendelea kuuliza maswali kuhusu wahalifu wengi'', alisema.

Rais Zuma naye kupitia mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha taifa cha televisheni, alisema kwa maoni yake wabunge waliozusha ghasia ni tatizo kubwa, na kulitaka bunge kuweka sheria kali kuliko zinazotumiwa kwa wakati huu.

Chanzo: Dw.de

No comments:

 
 
Blogger Templates