Wakiwa katika bia yao ya nne, mlango wa nyumba hiyo ulisikika ukifunguliwa, gari likaonekana likitoka, Beka akainuka na kuifuata pikipiki waliyoipaki pembeni, Shosi alijua anakoenda, hivyo akabaki kimya pale alipokaa.
Sasa endelea...
Wakati akipanda juu ya pikipiki na kuiwasha, gari lililokuwa likitoka kwa mzee Komba lilishaingia barabarani likielekea kusikojulikana. Beka alivuta mafuta na kulisogelea gari hilo, alipotupa macho ndani, akakuta aliyekuwa akiliendesha ni mwanamke, mama yake Stone, akapunguza mwendo na kugeuza, akarejea kwenye kijiwe chao.
Hakuna mtu mwingine aliyetoka ndani ya nyumba hiyo hadi gari lililotoka liliporejea. Saa kumi na moja jioni, wakapata wazo jipya.
“Nina uhakika huyu fala atakuwepo ndani, kwa nini tusiwalipue tu kwa petrol nyumba yote wafe?” Beka alimwambia Shosi, ambaye alikubaliana naye, lakini akamtaka kwanza wafanye mawasiliano na bosi wao Dayani.
Walipoongea na Dayani kuhusu mpango huo, naye aliunga mkono na kusema hilo litakuwa jambo zuri zaidi kwani alitaka kuwapa fundisho watu hao wanaomsumbua rafiki yake. Wakamalizia bia zao na kuondoka huku wakiitazama vizuri nyumba ya akina Stone.
***
Mara tu alipomaliza kuzungumza na vijana wake, Dayani alimpigia simu mzee Linus na kumweleza kuhusu mpango mpya, akimtaka kuondoka nyumbani hapo na kuelekea sehemu yoyote, ambako angekaa kwa siku moja au mbili, ili wakati wa tukio hilo, yeye asiwepo karibu.
Mzee Linus akajaribu kuupinga mpango huo, akisema lisingekuwa jambo jema kuwaua wote kwa mara moja, lakini rafiki yake akamsisitiza umuhimu wa kufanya vile, hasa kwa kuwa wangeondoa kabisa matatizo siku za mbele.
Kwa shingo upande akakubaliana naye, lakini moyoni mwake akasikitika sana kwa tukio linalokwenda kutokea. Hakutaka kumwambia jambo lolote mkewe kuhusu mpango huo, lakini akahakikisha watoto wake wote waliokuwepo nyumbani, wakiondoka na kwenda kulala nje ya nyumba yao.
Kulikuwa na watoto watatu nyumbani kwa mzee Linus, Tonny, Brown ambaye alikuwa kaka yake aliyekuwa na umri sawa na Stone na Mwasi, dadake aliyemuachia ziwa. Walipoambiwa kuhusu kuondoka nyumbani kupisha kupigwa dawa ya wadudu usiku, kila mtu kwa nafasi yake walijawa na furaha kubwa.
Mzee Linus na mkewe, wakaamua kwenda kulala hotelini eneo la Tegeta. Kichwani mwake alikuwa na simanzi kubwa, kwani alijua dhambi anayokwenda kuipata.
Mkewe aliona sura ya mumewe, akataka kujua sababu hasa ya kuwaondoa nyumbani, kwani suala la kupigwa dawa halikuwahi kuwa katika mipango yao. Alijua ataambiwa. Lakini mumewe alimsihi kumuacha kwanza apumzike, mambo mengine wangeongea baadaye.
***
Saa sita za usiku, Beka na Shosi wakiwa katika pikipiki mbili walikuwa wanaendesha taratibu kuingia katika eneo la Nakalekwa, ramani yao iliwaongoza vizuri kabisa hadi kwenye nyumba moja hivi ambayo haijamalizika kujengwa, wakasimama.
Wakashusha dumu la petrol lililokuwa kwenye pikipiki ya Beka, wakaliweka chini. Kwa tahadhari kubwa, Shosi akaenda hadi kwenye nyumba waliyoilenga, akaichunguza vizuri, akarudi hadi alipokuwa mwenzake, wakapeana ishara wakaondoka taratibu huku wakitupa macho huku na kule.
Wakafika walipokusudia, wakausukuma mlango wa geti, ulikuwa umefungwa, wakatoa ufunguo Malaya, wakaufungua ukafunguka, wakaingia kimya kimya. Wakaanza kumwaga petrol kupitia kwenye mlango wa mbele wa nyumba, mafuta hayo yakaingia ndani ya nyumba hadi dumu lilipokuwa tupu.
Licha ya ukali wa harufu ya petrol, walishangaa watu waliokuwepo ndani kushindwa kushtuka. Wakarudi mlangoni, wakachukua gazeti walilokuja nalo, wakalikunja vizuri, wakaliwasha moto kisha wakalitupa kwenye mlango wa mbele wa nyumba hiyo na mara moja, ukalipuka ndani.
Wakaanza kukimbia kuzifuata pikipiki zao na walipoziwasha tu, mayowe ya moto, moto, moto yakaanza kusikika, kwani moto ulishakuwa mkubwa na nyumba ilionekana kuteketea.
Simu zikaanza kupigwa huku na huku ili kuwanusuru watu waliokuwa ndani, zimamoto, polisi na kila mahali. Haikusikika kelele ya kitu chochote tokea mle ndani isipokuwa sauti ya moto uliokuwa ukiteketeza vitu.
Sasa watu walishajaa, walijitahidi kuuzima kwa mchanga na maji kwenye ndoo, lakini walionekana kama watu wanaofanya mchezo, moto ulizidi kuteketeza vitu, vilivyosikika vikipasuka kila mara!
Je, nini kitaendelea? Mbona hakukusikika hata mayowe kutoka ndani? Usikose kufuatilia katika toleo lijalo.
Chanzo: globalpublishers
No comments:
Post a Comment